19 November 2010

Azam yatamba kuikomalia Simba kesho.

Na Shaban Mbegu

KOCHA Msaidizi wa timu ya Azam FC, Habibu Kondo amesema kikosi chake kinatarajia kutoa upinzani mkali katika mchezo wa kirafiki utakaopigwa kesho
kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam dhidi mabingwa wa Tanzania Bara Simba.

Timu hizo mara ya mwisho zilikutana Septema 11, mwaka huu katika mchezo Ligi Kuu mzunguko wa kwanza, ambapo Simba ilishinda mabao 2-1. Mechi hiyo ni maalumu ambalo litapamba tamasha la Amka Kijana.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kondo alisema japokuwa mchezo huo ni wa kirafiki, lakini amepanga kutoa upinzani mkali kwa mabingwa hao, kulipa kisasi cha kufungwa kwenye ligi..

Alisema licha ya wachezaji wake wanne kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzan Bara 'Kilimanjaro Stars' na wawili walioitwa 'Zanzibar Heroes' bado timu yake itatoa ushindani wa kweli kwani wachezaji waliopo pia ni wazuri.

"Japokuwa huu ni mchezo wa kirafiki, lakini nimepanga kutoa upinzani mkali kwa mabingwa hao watetezi na nimepanga kuwaonesha maajabu ambayo hawatayatarajia kutoka katika timu yangu", alisema.

Tamasha hilo ambalo limedhaminiwa na kituo cha redio cha Times FM na Clouds FM kwa lengo la kuhamasisha vijana kubadilika na kufanya kazi.

Pia katika tamasha hilo kunatarajiwa kuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii Omari Omari, Berry Black, AT, makundi ya TMK Wanaume Family na Tip Top Conection pamoja na bendi ya Bwagamoyo Sound.

No comments:

Post a Comment