06 November 2013

RC: CHADEMA HAKINA HADHI



  • ASEMA NI CHAMA CHA JUZI,CCM KIKONGWE
 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Rehema Nchimbi, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hakina hadhi ya kuitwa mtani wa jadi dhidi ya chama tawala.


Dkt. Nchimbi aliyasema hayo Mjini Dodoma jana wakati akifungua semina ya mafunzo maalumu ya kikazi kwa Wenyeviti wa CCM kutoka kata zote za Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.Alisema watani wa jadi katika soka ambao ni Simba na Yanga, zote ni timu za miaka mingi zenye nguvu karibu sawa katika soka lakini CHADEMA ni chama cha juzi hivyo hakiwezi kuwa mtani wa jadi kwa CCM.

Aliongeza kuwa, CCM si chama cha kulinganishwa au kuwekwa kwenye ushindani na vyama vya upinzani bali ni chama kikongwe lakini si cha kizee ila kwa uwepo wake miaka mingi.Dkt. Nchimbi alisema, vyama vya upinzani bado vichanga kwa CCM ambacho ni chama kinachoongoza dola hivyo aliwataka Wenyeviti hao wafanye kazi ya kupanga safu za kuimarisha chama kama wafanyavyo magolikipa wa timu za soka.

  "Kazi kubwa ya Mwenyekiti ni kukaa nyuma, kupanga safu na kuangalia jinsi watendaji wanavyofanya kazi ili kuhakikisha yanafanyika marekebisho ya haraka pale utendaji unapokuwa unakwenda vibaya," alisema Dkt. Nchimbi.

  Aliongeza kuwa ni muhimu kuhakikisha kila kiongozi wa CCM na watendaji serikalini, wanatekeleza ilani ya chama kwa umahiri mkubwa pamoja na kuchukua hatua kwa watendaji au kiongozi yeyote ambaye itabainika anakwenda kinyume.

 "Utakuta Mtendaji au mtumishi wa Serikali, anasema yeye si mwana siasa wakati aliyekupa kazi ni CCM ambayo imepewa dhamana ya kuunda Serikali... najua tupo viongozi, watendaji na watumishi wa umma wenye tabia ya kujifanya hawana uhusiano kibisa na CCM, hakikisheni watu wa aina hii mnashughulika nao bila kuwaonea haya.

 "Msiwaache na mwisho wa siku kuilaumu Serikali, vinginevyo kama mnawaacha mambo yakienda kombo mjilaumu wenyewe kwa sababu mmeacha jukumu lenu la kusimamia utendaji na utekelezaji wa ilani ya chama," alisema Dkt. Nchimbi.Dkt. Nchimbi alisema anatambua kuwa uimara wa CCM ni wa muda mrefu na hakiwezi kufa kiurahisi kama wapinzani wanavyokitabilia

No comments:

Post a Comment