Na Mariam
Mziwanda
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC),
kimemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ajiuzulu
kutokana na agizo alilotoa kwa vyombo vinavyohusika kulinda maliasili za nchi
kuwapiga risasi na kuwaua watu wote ambao watakutwa au kujihusisha na biashara
ya nyara za Serikali.
Mwanasheria wa LHRC, Bw. Harold Sungusia,
aliyasema hayo Dar es Salaam
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji
wa kituo hicho, Dkt. Helen Kijo-Bisimba.
Alisema ni kawaida ya viongozi wengi nchini
kutopenda kuwajibika hivyo ni muhimu wakafahamu kuwa, hakuna aliye juu ya
sheria ambapo kituo hicho kitapambana kulinda matakwa ya sheria za nchi si
vinginevyo.
"Wote waliohusika
kuvunja haki za raia kwenye "Operesheni ya Tokomeza Ujangili"
hawataachwa... operesheni hii ilikuwa ya mateso makubwa kwa watu mbalimbali kuumizwa
vibaya, kupoteza maisha, nyumba za watu kuchomwa moto pamoja na kuuawa kwa
mifugo.
"Kituo kimepokea taarifa za vifo kutoka
sehemu mbalimbali nchini... kimsingi hatutaogopa kumchukulia hatua za kisheria
kiongozi yeyote ambaye atatumia nafasi aliyonayo kuvunja katiba ya nchi na haki
za raia," alisema Bw. Sungusia.
Aliongeza kuwa, mbali ya mauaji ya watu
mbalimbali katika operesheni hiyo pia mifugo 190 ilipigwa risasi katika Kijiji
cha Kegonga, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Bw. Sungusia alisema operesheni hiyo
ilifanyika kwa mfumo wa kutengeneza makambi maalumu ya kutesa watuhumiwa wa
makosa ya ujangili ambapo kutokana na hali hiyo, kituo hicho wamelazimika kuwachukulia
dhamana watuhumiwa 13.
"Watu hawa walifikishwa katika Mahakama
ya Bunda ambao walikamatwa na kuteswa katika kambi maalumu inayosimamiwa na
Ofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye alisaini
hati ya kiapo cha kuwapeleka watuhumiwa mahakamani," alisema Bw. Sungusia.
Aliongeza kuwa, watuhumiwa hao wameeleza
walivyokamatwa kutokana na orodha iliyowasilishwa kwa Mkuu wa operesheni na
kujikuta wametumbukia katika mateso ambayo yaliambatana na kumwagiwa pilipili
na kutishiwa bunduki ili wakiri makosa.
Alisema kituo hicho kinataka baadhi ya
madaktari ambao kwa kiasi kikubwa wameonekana kupotosha ukweli wa sababu za
vifo vya watu walioteswa kwa madai ya kuhusika na ujangili, kuchunguzwa na
kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Alifafanua kuwa, ipo haja ya Balozi Kagasheki
kujiuzulu, Serikali kuizuia operesheni hiyo na watu walioathirika kulipwa
fidia.
"Tunatoa wito kwa
viongozi kuongoza kwa kuzingatia misingi ya katiba, utawala wa sheria, haki za
binadamu na kuepuka kutoa matamko ambayo yanakiuka haki za binadamu,"
alisema
No comments:
Post a Comment