Na Heckton
Chuwa, Moshi
Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kiboriloni kwa
tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Vincent Rimoy, amefariki
dunia jana mchana.
Kwa mujibu wa
taarifa zilizothibitishwa na Meya wa halmashauri hiyo, Mstahiki Jaffari
Michael, alisema Rimoy alifariki wakati akikimbizwa hospitali baada ya
kudondoka akiwa shambani kwake eneo la Mandaka, Mjini Moshi.
"Mwili wa
marehemu umehifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye Hospitali ya Rufaa ya
KCMC," alisema Mstahiki Michael pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya
Moshi Mjini.
Akizungumza na
Majira, mmoja wa wafanyakazi wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe
gazetini, alisema Rimoy aliamka asubuhi na kwenda shambani kwake baada ya
kutoka safari ya Dar es Salaam Novemba 4, mwaka huu (juzi).
Naye mmoja wa rafiki zake na marehemu ambaye
naye hakutaka jina lake
liandikwe gazetini,
alisema kifo cha Rimoy kinaikumbusha familia yake machungu yaliyowakuta miaka
23 iliyopita.
"Rimoy aliwahi kupata ajali ya gari
Sikukuu ya Pasaka mwaka 1990 akiwa na familia yake... katika ajali hiyo
alimpoteza mkewe na watoto wote watano, hakika inasikitisha," alisema.
Mbali ya kuwa mwanasiasa, marehemu
alikuwa akijishughulisha na biashara
akimiliki hoteli maarufu Mjini Moshi inayoitwa New Castle, biashara ya ujenzi pamoja na
kumiliki Shule ya St. Patrick.
.
No comments:
Post a Comment