07 November 2013

MAPIGANO YA WAKULIMA, WAFUGAJI YAPAMBA MOTO



 Na Mwandishi Wetu
  Mapigano makali ambayo yanaripotiwa kusababisha vifo yametokea wilayani Mvomero, mkoani Morogoro yakihusisha wakulima na wafugaji, ambapo jana yaliingia siku ya pili mfululizo.

Habari za kuaminika kutoka eneo la tukio mjini humo jana, zilieleza kuwa mapigano hayo yalianza juzi katika eneo la Endeki baada ya sungusungu kuzuia makundi mawili ya ng'ombe wa wafugaji wanaodaiwa kula mazao.
Mmoja wa mashuhuda wetu kutoka eneo la tukio alisema kuwa baada ya ng'ombe hao kushikiliwa walitokea wafugaji wa jamii ya Wamasai wakitafuta mifugo hiyo, ndipo mapigano yalipoanza yakihusisha pande zote mbili.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, wakati wa mapigano hayo sungusungu 11 walijeruhiwa huku mmoja akiripotiwa kufa. Kwa upande wa wafugaji, iliripotiwa kuwa upande wao ulipata majeruhi saba akiwemo mmoja aliyejeruhiwa kwa mshale uliomchoma mgongoni na kutokea kifuani.
Mtoa habari wetu huyo aliyezungumza kwa sharti la jina lake kutochapishwa gazetini, alisema baada ya kutokea kwa mapigano hayo, makundi ya Wamasai na sungusungu yalizidi kukusanyika, huku Wamasai wakijaribu kukomboa mifugo yao bila mafanikio hali iliyosababisha mapigano hayo kupamba moto.
Mapigano hayo jana yaliingia siku ya pili, ambapo watu waliokuwa mstari wa mbele walidai kushuhudia miili ya watu watano ikiwa imelala chini, lakini haikujulikana mara moja kama walikuwa wamepoteza maisha au hapana.
"Kwa kweli hali ni mbaya hasa kwenye milima ya Kigurukilo, ndipo miili ya watu hao inaonekana na tayari sungusungu zaidi ya 1,000 wamejikusanya na kuingia kwenye kijiji cha wafugaji cha Kambala kwa lengo la kuwatia umaskini Wamasai kwa kuchoma nyumba zao," alisema mtoa habari wetu.
Alipoulizwa kama ng'ombe wamepatikana, alisema sungusungu wametokomea na mifuko hiyo porini. Kutokana na hali ya mapigano kuwa mbaya, wanawake na watoto wa jamii ya Wamasai walilazimika kuomba hifadhi kwenye Kituo cha Polisi Dakawa.
  Juhudi za kupata wasemaji wa Jeshi la Polisi kuzungumzia vurugu hizo zilishindikana baada ya simu zao kutopatikana

No comments:

Post a Comment