29 October 2013

WANAOMPINGA JK WAKAMATWA



  •  WALIKUWA NA BUNDUKI TATU, MAPANGA 18 NA VISU
  • WAKUTWA MSITUNI, WAPO WATUMISHI WA SERIKALI

 Na Yusuph Mussa, Handeni
  Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, amesema watu waliomuua askari mgambo Salum Mgonje na kumpiga risasi Mkuu wa Kituo cha Polisi Songe, wilayani Kilindi Edward Lusekolo ni kikundi kilichokuwa kinaishi msituni.

Alisema kikundi hicho kinaipinga Serikali ya Rais Jakaya Kikwete na kudai ni ya kikafiri kikiwa na mipango ya kutaka Tanzania isitawalike.Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Handeni, Bi. Gallawa alisema kikundi hicho kiliweka kambi tatu wilayani humo kikifanya mafunzo mbalimbali yakiwemo ya kijeshi.
“Pia kikundi hiki ndicho kilichokuwa kikipinga mchakato wa sensa mwaka 2012, kambi zao tatu zilikuwa katika Kata ya Lwande na Negero kwenye Kijiji cha Madina.“Katika kambi ya Madina, wafuasi wao wawili wameuawa baada ya kupinga kitendo cha kukamatwa na askari Oktoba 26 mwaka huu wakijiita wafuasi wa Sunni,” alisema.
Aliwataja wafuasi waliouawa kuwa ni Ramadhan Hamis, ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mwingine jina lake halikufahamika mara moja lakini inasemekana ni mwalimu wa dini ya Kiislamu (ustaadh) Kijiji cha Lwande.
Aliongeza kuwa, kikundi hicho kimekutwa na bunduki tatu aina ya gobore, shortgun moja, bastola mbili zilizotengenezwa kienyeji, mapanga 18 na visu 10.  Bi. Gallawa alisema wafuasi 46 wa kikundi hicho tayari wamekamatwa lakini jambo la kushangaza wamo watumishi wa Serikali ambao ni walimu wa shule za msingi na watafikishwa mahakamani wakati wowote.
  Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, ambayo inaongozwa na Bi. Gallawa, imeamua kuweka kambi Kilindi kwani hivi sasa hali ya usalama si nzuri hadi itakapotulia. Akizungumza na Majira hivi karibuni, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Constantine Masawe, alisema askari mgambo Salum Mgonje aliuawa Oktoba 22 mwaka huu ambapo Edward alipigwa risasi za mbavu na mkononi Oktoba 23, saa mbili usiku.
  Kikundi hicho kinajumuisha wakazi wa vijiji mbalimbali wilayani humo ambao wamefukuzwa na wenzao kutokana na tabia zao za kupinga mambo mbalimbali ya maendeleo. Chanzo cha kuanzishwa kikundi hicho ni baada ya mwenzao mmoja ambaye ni mfanyabiashara kutakiwa kulipa ushuru katika Kijiji cha Lwande na kukataa hivyo mgambo waliingilia kati ndipo wafuasi wao walichukua uamuzi wa kwenda kuwakata mapanga mgambo ambao mmoja alijeruhiwa na mwingine kuuawa.

No comments:

Post a Comment