29 October 2013

MWIGAMBA AZIDI KUIBUA MAZITO

  • AMTOLEA UVIVUMBOWE,ASISITIZA MABADILIKO


 Pamela Mollel na Goodluck Hongo
  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Arusha, Bw. Samson Mwigamba, amesema kutokana na uadilifu wake na mapenzi mema aliyonayo katika chama, ameamua kuachia madaraka kwa muda ili kupisha uchunguzi dhidi yake.

Bw. Mwigamba aliyasema hayo Mjini Arusha jana wakati akizungumza na waandishi wa habari pamoja na kutoa tuhuma nzito dhidi ya viongozi wakuu wa chama hicho akiwataka waondoke madarakani.
Alisema viongozi hao wameonesha udhaifu katika mipango ya chama hicho kutaka kushika dola na kusisitiza kuwa, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. Freeman Mbowe, ameshindwa kazi ya kukiongoza chama hicho.
“Chama kimeshindwa katika mambo mbalimbali zikiwemo operesheni zake kutokana na uwezo wa Mbowe kufikia mwisho, kitendo cha mimi kutoa maoni ya kutaka Mbowe aondoke katika wadhifa alionao ili aweze kubaki na nafasi ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kinaonekana ni usaliti,” alisema.
Aliongeza kuwa, siku za nyuma akiwa katika Jimbo la Karatu, mkoani Arusha, Bw. Mbowe alimpigia debe Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Wilbrod Slaa akidai atakuwa mgombea urais wa chama hicho mwaka 2015 lakini hakuonekana msaliti wa kauli iliyozusha sintofahamu miongoni mwa wanachama.
  Akizungumzia sakata la kuenguliwa kwenye nafasi yake kwa madai ya kutoa siri mbalimbali za chama, alisema     Kikao cha Baraza la Uongozi Kanda ya Kaskazini hakina mamlaka ya kumuengua kwenye nafasi hiyo isipokuwa Kamati Kuu ya chama hicho.
 “Niliacha kazi yenye mshahara wa sh. milioni 1.9, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kutokana na mapenzi mema niliyonayo kwa CHADEMA.
  “Nimewahi kukumbana na misukosuko mingi pamoja na kukaa rumande siku saba kutokana na msimamo wangu wa kuhamasisha mageuzi ya kweli,” alisema Bw. Mwigamba.
  Hata hivyo, alisema yeye ndiye kiongozi pekee ndani ya chama hicho aliyeandika makala nyingi kuliko kiongozi yeyote kwa lengo la kuhamasisha mageuzi lakini hadi sasa anahukumiwa kwa msimamo wa kutaka mabadiliko ya viongozi wanaoonesha kushindwa kukiongoza chama hicho kimalengo.
  Kikao cha baraza hilo kilihudhuriwa na wabunge wote wa Kanda husika akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kilichofanyika Mjini Arusha.
  Alisema tuhuma dhidi yake ni kutumiwa na baadhi ya viongozi wa chama akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe ili kukisambaratisha chama na kufafanua kuwa, madai hayo ni fikra potofu za kisiasa.
  “Tukiwa ndani ya kikao, nilirushiwa tofali na Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema, baada ya hapo, red-briged (walinzi wa chama), walinikamata mbele ya Bw. Mbowe, Mwenyekiti wa chama Kanda ya Kaskazini, Mchungaji Israel Natse, alisimama na kusema kikao kinaahirishwa ili waweze kunijadili.
 “Mbunge Lema hana utu, anakosea sana kujiita mcha Mungu kwani amekuwa na tabia ya kuwachafua baadhi ya viongozi wa chama nikiwemo mimi wakati elimu yake ni ndogo,” alisema.
  Alisema alikijenga chama hicho kwa kutumia rasilimali zake bila kuitendea haki familia yake na kufafanua kuwa, Bw. Lema si mwanachama halisi katika chama.
  Aliongeza kuwa, yeye ni mwanachama hai na Mtanzania safi anayependa nchi yake na chama chake hivyo kama viongozi wa chama wataamua kumruhusu amwage mchele kwa mambo yaliyotokea, wamruhusu na hata shindwa.
CHADEMA wazungumza
  Akizungumza na Majira, Ofisa Habari wa CHADEMA, Bw. Tumaini Makene, alisema tukio lililotokea Mjini Arusha na kusababisha Bw. Mwigamba kusimamishwa uongozi, halina uhusiano wowote na Bw. Mbowe.
  Alisema baraza hilo la uongozi lilitoa uamuzi wa dharura kutokana na Bw. Mwigamba kuvunja kanuni, maadili na taratibu za kikatiba za chama hicho kwani mamlaka hayo wanayo.
 “Viongozi wa CHADEMA ndiyo walioita polisi ili kumuokoa Mwigamba baada ya kukiri makosa aliyokuwa akituhumiwa na alitia saini mwenyewe kwa dole gumba... katika kikao kilichomsimamisha Mbowe hakuwepo.
 “Huwezi kulifanya jiwe liwe kichuguu hivyo kinachoelezwa juu ya jambo hili ni propaganda tu dhidi ya Mwenyekiti wa chama kwani sisi tunaushahidi wa picha za mnato na video,” alisema.
  Aliongeza kuwa, katika kikao hicho hakukuwa na vurugu ila baada ya Bw. Mwigamba kuambiwa atoke nje na kushindwa kufanya hivyo, ndipo walipoitwa polisi kwa ajili ya usalama wake mwenyewe.

5 comments:

  1. Kinachoshangaza ni watoa maoni wengi wanadhani kuwa watu wenye shaka dhidi ya chadema hawajasoma, wana akili mgando, ni mafisadi ama wametumwa na ccm. Hawa hawajakaa wakachambua mtandao mzima wa uongozi wa chadema. Wkachambua kwa makini historia zao, viwango vyao vya elimu na utashi wao na uwezo wa kuchambua mambo
    Fikiri ccm imekufa na serikali yake haipo madarakani. Alafu panga baraza la mawaziri uweke viongozi wa chadema. Alafu bashiri kitakachotokea ukizingatia mahusiano yao na matendo yao ndani na nje ya chama

    Kazi kwako!

    ReplyDelete
  2. 1. Hata kama tuhuma zote alizotoa Mwigamba ni za ukweli kabisa, kwa nini alizipeleka kwenye mtandano asizipeleke kwenye vikao vya chama?

    2. Kama alijua Chadema ilichakachua katiba ili kuongeza urefu wa kipindi cha uongozi wa mwenyeketi, kwa nini hakusema hivyo hilo lilipofanyika zaidi ya miaka 5 iliyopita?

    ReplyDelete
  3. Hapo CHADEMA wamesau sera zao za NCHI ISITAWALIKE mpaka nani ya chama chao ni ngumi na vurugu kila sehemu walipo

    ReplyDelete
  4. CHADEMA ya leo sio chama kidogo ten.Kwa hiyo hakina budi kuendesha mambo yake kidemokrasia,kisasa na kiuwazi kwelikweli.Ilibidi Mwigamba apewe nafasi ajieleze ndani ya chama. Pia chama kijikite katika kuunganisha nguvu na vyama vya upinzani ndani na nje ya bunge.

    ReplyDelete
  5. Du!!! Kwa kweli kazi.

    ReplyDelete