Na Mwandishi Wetu, Korogwe
Wananchi wa vijiji vya
Kwagunda na Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga,
wameaswa kuwa makini na kutolaghaiwa kuuza ardhi yao mara baada ya kazi ya
kupanga matumizi bora ya ardhi, kupimwa na kugawiwa hatimiliki katika maeneo
yao kukamilika
. Rai hiyo imetolewa juzi na Meneja Mpango wa Kurasimisha Rasilimali
na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Makame Juma Pandu wakati
akifungua mafunzo ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa wananchi wa vijiji hivyo
vitakavyoshiriki kuandaa mpango na kufanya kazi ya upimaji wa ardhi za vijiji
vyao yaliyofanyika kwa pamoja katika Kijiji cha Mnyuzi.
Pandu aliwaeleza wananchi hao kuwa ardhi ikishapimwa na kupatiwa
hati huongezeka thamani maradufu; na hivyo wapo wajanja ambao wakisikia ardhi
ya Kwagunda na Mnyuzi imepimwa na kutolewa hati watafika katika vijiji hivyo
kwa lengo la kuinunua ili waweze kunufaika nayo.
"Baada ya kupimiwa na kupatiwa hati wajanja watakuja kutaka
muwauzie ardhi, kuweni makini kwani tumekuja kupima ardhi hii ili iwanufaishe
ninyi wakazi wa vijiji hivi na watoto wenu kwani mkishakuwa na hati mtaweza
kuzifanyia matumizi mbalimbali kama kuweka dhamana benki na kuchukua mikopo,
hata watoto wenu kusomeshwa na mikopo ya vyuo vikuu kwa dhamana ya hizo
hati,hivyo kabla hamjauza jihakikishieni masilahi yenu na vizazi vyenu
kwanza," aliongeza Pandu.
Aidha, Pandu aliwaomba wadau hao kuzingatia mafunzo hayo na
kueleza kuwa vijiji vyao vimewaamini na kuwachagua wao kufanya kazi hiyo kwa
niaba yao; hivyo kwa kushirikiana na wataalamu wataandaa mpango wa matumizi
bora ya ardhi ambao ukipitishwa na vijiji vyao ndipo watafanya zoezi la upimaji
wao wenyewe kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi wa Halmahauri ya Wilaya ya
Korogwe.
Nao
wananchi wa kijiji hicho walieleza matumaini yao ya kupatiwa fursa hiyo ya
kupimiwa maeneo yao kwa kueleza kuwa ni kuondokana na umaskini kupitia mpango huo na wako tayari kushawishi wenzao wa vijiji jirani vya
Lusanga,Shambakapori na Kwamzindaha kuuomba mpango huo kupitia halmashauri ya
wilaya ili kwa pamoja waweze kunufaika.
"Sisi tumefurahi sana kupata mpango huu kwani tunajua gharama
za upimaji tusingeweza kumudu mwananchi mmoja mmoja,hivyo tunaishukuru sana
serikali kupitia MKURABITA na tutawashawishi wenzetu wa vijiji jirani waombe
mpango huu kwani wakazi wengi wa Mnyuzi wana mashamba katika vijiji
jirani," alisema Judith Muro mkazi wa kijiji cha Myuzi.
Halmashauri
ya Wilaya ya Korogwe ina vijiji 122 ambapo ni Kwagunda na Mnyuzi pekee ndivyo vilivyofikiwa na mpango wa kurasimisha rasilimali ardhi vijijini (MKURABITA)
ambao pia umekwishafanyika katika vijiji vingine vichache nchini.
No comments:
Post a Comment