Na
Mwandishi Wetu
Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), limepinga
hatua ya Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi (siku 14) na Mtanzania
(miezi mitatu) na kudai adhabu hiyo imetolewa kutokana na sheria kandamizi ya
magazeti ya mwaka 1976 inayolalamikiwa na wadau kwa miaka mingi.
Tamko hilo limetolewa kwenye kikao chao kilichofanyika Dar es Salaam jana ili
kujadili uamuzi huo wa Serikali na kudai kuwa, hiyo ni moja ya sheria ambazo
Tume ya Jaji Francis Nyalali, ilipendekeza ifutwe kwa sababu mbalimbali.
Sababu hizo ni
pamoja na kukiuka misingi ya haki za binadamu, utawala bora, kwenda kinyume cha
Katiba ya nchi pamoja na maazimio ya kimataifa ya haki za binadamu."Tunaungana na
taasisi nyingine kupinga adhabu hii kwa magazeti ya Mwananchi, Mtanzania pia tukikumbushia
kifungo cha gazeti la Mwanahalisi kwa sababu sheria iliyotumika haifai.
"Hili si jambo la kuendelea kufumbiwa
macho na jamii ambayo inafuata misingi ya kidemokrasia na utawala bora hivyo
tunalaani kwa nguvu hatua hizi ambazo zimekiuka misingi hii ukizingatia
Serikali ndiyo inayosimamia makubaliano ya kimataifa kuhusu uwazi katika
uendeshaji wa Serikali," ilisema taarifa hiyo.
Jukwaa hilo liliongeza kuwa, wanafahamu kuwa
kuna kesi ya kupinga Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 iliyofunguliwa mwaka 2009
lakini ni jambo la bahati mbaya na kusikitisha sana kuwa hadi sasa, kesi hiyo
haijaanza kusikilizwa kwa sababu ya kutopangiwa majaji.
"Tunapenda kutoa
mwito kwa Mhimili wa Mahakama, kurekebisha kasoro hii na kupanga majaji wa
kuisikiliza ili haki iweze kutendeka...kuchelewesha haki ni sawa na kunyima
haki," iliongeza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Kampuni ya Mwananchi
Communications Limited (MCL) , imedai kusikitishwa na uamuzi wa Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuchukua hatua kali ya kulifungia
gazeti lao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Tido
Mhando, alisema kampuni hiyo ilionesha ushirikiano wa hali ya juu pale
ilipoandikiwa barua ya kujieleza na kutoa ufafanuzi wa kweli juu ya habari
zilizoandikwa na gazeti hilo.
Habari hizo ni ile iliyohusu mishahara mipya ya watumishi wa Serikali na
"Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi".
No comments:
Post a Comment