Benki ya CRDB imeibuka mshindi wa jumla kutoka miongoni mwa waajiri
nchini wanaowasilisha michango ya wafanyakazi wake kwa wakati katika Mfuko wa
Pensheni wa PPF, anaripoti Reuben Kagaruki.
Kutokana na ushindi huo, benki hiyo
ilitunukiwa tuzo na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa, wakati wa ufungunzi
wa mkutano wa 23 wa mwaka wa wanachama na wadau wa PPF uliofanyika mjini
Arusha.
Mshindi wa
pili miongoni mwa waajiri wanaowasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ni
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA). Washindi wengine waliozawadiwa
zawadi hizo kulingana na makundi yao ni Bodi ya
Sukari Tanzania (Mshindi wa
Kwanza) na Bodi ya Kahawa Tanzania
(2) kwa upande wa sekta ya Kilimo.
Kwa upande wa
sekta ya madini mshindi wa kwanza alikuwa ni Barrick Bulyanhulu na kufuatiwa na
mgodi wa madini wa Geita, huku upande wa sekta ya usafirishaji na umeme mwajiri
aliyeongoza kwa kulipa michango ya wanachama kwa wakati EWURA ikifuatiwa na
Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania.
Upande wa
waajiri wa sekta ya fedha, Benki ya CRDB iliibuka kinara ilifuatiwa na Benki ya
NMB wakati kwa upande wa waajiri wa sekta ya elimu na mafunzo mshindi ni Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi Bugando. Mshindi wa upande wa sekta ya afya alikuwa
Research Triangle Institute na HJF Medical Research International, upande wa
ujenzi mshindi ni Bodi ya Usajili wa Makandarasi na Kampuni ya Ujenzi ya
Konoike, huku upande wa viwanda na biashara mshindi wa kwanza akiwa Kampuni ya
Sigara Tanzania (TCC) na Kampuni ya Saruji Mbeya.
Waajiri walioibuka
washindi kwa upande wa vyombo vya habari ni wachapishaji wa magazeti ya
serikali (TSN) akifuatiwa na Multichoice Ltd, wengine wakiwa Puma Energy
Tanzania Ltd na HakiElimu huku mwajiri wa kujitegemea aliyeibuka mshindi akiwa
ni Dkt. Shukuru Kawambwa
No comments:
Post a Comment