- MAHAKAMA KUU YABAINI KASORO ZA KISHERIA
Na Grace Ndossa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewaachia huru wafuasi 52 wa
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda, waliokuwa
wakikabiliwa mashtaka matatu.
Hukumu hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Jaji Salvatory Bongole
ambaye alisema makosa yaliyowatia hatiani washtakiwa hao adhabu yake ilikuwa
kifungo cha miezi mitatu gerezani au kulipa faini ya sh. 50,000 kila mmoja.
Alisema kosa la kwanza ambalo ni kula njama
halikuwa sahihi, hivyo adhabu ya kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani
aliifuta.
Aliongeza kuwa, kosa la pili na tatu
anakubali kutiwa hatiani kwa washtakiwa, lakini alibadilisha adhabu ya kosa hilo inayowataka
washtakiwa kukaa gerezani mwaka mmoja badala yake watakaa miezi mitatu gerezani
au kulipa faini.
Hata hivyo, Jaji Bongole alisema makosa
yaliyowatia hatiani washtakiwa hao ni kula njama, kufanya mikusanyiko isiyo
halali na kukaidi amri iliyotolewa na Jeshi la Polisi juu ya zuio la kutofanya
maandamano.
Alisema kifungu cha 384 kinaeleza kosa la
kula njama na kuwatia hatiani, adhabu yake haikuwa sahihi. “Mlipewa adhabu
mbili katika kosa moja, kula njama pamoja na kuiba.
“Mlitiwa hatiani katika kosa la kuiba hivyo
kosa la kula njama linakufa lakini mlipewa adhabu kwa makosa yote
mawili...adhabu mliyopewa haikuwa sahihi,” alisema Jaji Bongole.
Aliongeza kuwa, kosa la pili baada ya kupata
ushahidi ameona upande wa Jamhuri ulithibitisha washtakiwa waliandamana wakati
wakipinga amri ya Jeshi la Polisi.
“Nakubaliana na umauzi ulitolewa na Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kuwatia hatiani kwa kosa la pili na tatu la kukaidi
amri iliyotolewa na Jeshi la Polisi kutoandamana.
“Wakili wa washtakiwa, Mohamed Tibanyendera,
alisema baada ya Mahakama ya Kisutu kuwatia hatiani, ilipaswa kuzingatia sheria
ya kupunguziwa adhabu hiyo,” alisema Jaji Bongole.
Alisema amefuatilia mwenendo wa kesi hiyo kwa
makini hivyo anakubaliana na upande wa utetezi kuwa sheria ya kupunguziwa
adhabu washtakiwa hao haikutiliwa maanani, adhabu ya kifungo haikufuata kifungu
cha 46 cha Sheria za Polisi.
Washtakiwa hao walihukumiwa kwenda jela Machi
21 mwaka huu ambapo hadi jana, walikuwa wamekaa gerezani kwa zaidi ya miezi
saba, hivyo mahakama iliwaachia huru washtakiwa wote.
Awali washtakiwa hao
walitiwa hatiani katika makosa matatu ambayo kila moja adhabu yake ni kukaa
gerezani mwaka mmoja na adhabu zote zilitakiwa kwenda kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment