22 October 2013

MAWAKILI: PINDA ANA KINGA YA BUNGE



 Mawakili katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, jana waliendelea kuvutana mahakamani, anaripoti Grace Ndossa.


Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo Wakili wa Serikali Sara Mwaipopo alisema mashtaka dhidi ya Pinda hayana msingi wowote kwa kuwa kauli aliyoitoa bungeni inalindwa na sheria ya haki na mamlaka ya kinga za bunge.

“Alisema taasisi au mtu yeyote haruhusiwi kufungua mashtaka mahakamani kwa jambo lolote la jinai au madai lililotolewa ndani ya bunge.

Kwa mujibu wa katiba, bunge kama mhimili wa Dola ni chombo kimepewa Mamlaka ya kusimamia na kudhibiti shughuli zake , chini ya ibara 89 imeipa mamlaka bunge kutunga na kuweka kanuni zake kwa ajili ya kuendesha na kusimamia shughuli zake zinazofanyika ndani ya bunge.

“Kanuni hizi zimeweka bayana mambo yatakayosimamiwa na bunge lenyewe na pia zinaeleza hasa ni nani anayetakiwa kupeleka maneno au kauli bungeni,”alieleza Mwaipopo.

Hata hivyo alieleza kanuni ya 71 (c) inaeleza wazi ni mtu binafsi raia wa Tanzania ndiye anayeweza kupeleka malalamiko bungeni, si makundi, shirika au taasisi yoyote ile kumwakilisha mtu binafsi.

“Kutokana na kuwepo kwa sheria ya Haki na Mamlaka ya Kinga ya wabunge kitu chochote kinachotolewa bungeni kina kinga hivyo sioni sababu ya mahakama kuendelea kusikiliza madai hayo,” alisema.

Mwaipopo aliomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo yaliyowasilishwa na Taasisi hizo kama mahakama itakubali maombi hayo kesi zitafunguliwa nyingi.

Wakili wa serikali Alice Mbuya alieleza mahakama kuwa kwa kuwa walalamikaji walielewa kabisa hawakutakiwa kuwasilisha maombi yao mahakamani wanaendelea kupeleka shauri mbele ya mahakama ili iingilie sheria za bunge wakati wanajua bunge lina taratibu zake kisheria.

Pia alieleza kuwa Mahakama inatambua kuwa kuna mgawanyiko wa madaraka mambo hayo hayakupaswa kuwepo mahakamani.

Alidai shauri hilo lipo mahakamani hapo isivyo halali kwa kuwa wadai hao walifungua madai yao kwa kueleza maoni yao badala ya kufafanua msingi wa madai.

Wakili wa upande wa walalamikaji, Mpale Mpoki, alisema alichokisema Bw. Pinda, bungeni Mjini Dodoma, kinavunja haki za binadamu jambo ambalo ni kinyume cha kinga inayodaiwa kuwepo dhidi ya wabunge.

Shauri hilo liliwasilishwa Mahakama Kuu mbele ya Majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo ambao ni Jaji Kiongozi Fakhi Jundu, Augustine Mwarija na Dkt. Fauz Twaib.

Mpoki alieleza Mahakamani kuwa mahakama ina mamlaka na uwezo wa kuhoji sheria za bunge yoyote inayoelekea kuvunja sheria za kibinadamu.

Pia alieleza mahakama hiyo kuwa japo kuna mgawanyiko wa madaraka sheria hizo hazimfanyi mtu kuvunja sheria za kibinadamu.

Kesi hiyo iliyofunguliwa na LHRC na TLS walimfungulia Waziri Mkuu kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni ya kuruhusu vyombo vya usalama kuwapiga watu wanaokataa kutii sheria zinazotolewa na vyombo hivyo.

Mbali na Pinda mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye ni mdaiwa namba mbili.

Akiwa katika kipindi cha maswali ya hapo kwa hapo Bw. Pinda alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini Murtaza Mangungu (CCM) aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu malalamiko dhidi ya vyombo vya dola katika baadhi ya maeneo kama Mtwara juu ya kuwapiga wananchi.

Katika majibu yake Waziri Pinda alisema ukifanya fujo umeambiwa usifanye hivi ukafanya utapigwa tu maana hamna namna nyingine lazima tukubaline kwamba nchi inaongozwa kwa misingi ya kisheria.
Wakati huo huo, Kesi inayopinga kupanda tozo ya sh 1,000 za laini za simu imeahirishwa hadi Octoba 31 mwaka huu ambapo itaendelea kusikilizwa

2 comments:

  1. sheria ichukue mkondo wake pindi akibainika ana kosa...swala la kuvunja sheria halina mkubwa wa mdogo..na mahakama ifanye kazi yake si kuonea uruma kwa umaarufu wa mtu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Wewe vipi? Mbona unatishia mahakama. Huo ni ubishi wa kisheria mahakamani. Tayari waziri mkuu yuko mahakamani. Sheria tayari iko kwenye mkondo wake. sasa unataka hata sheria isifanye kazi! Nani kakuambia ni mjadala nje ya mahakama?

      Delete