Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pianiMakamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Zanzibar, akifungua semina ya sikunneya watendaji na viongozi wa chama
hicho ngazi ya wilaya na mikoa Mjini Dodoma
jana
- ASEMA CCM HAINA NIA YA KUHODHI MCHAKATO
- ATOA AGIZO ZITO KWA MAKATIBU WILAYA, MIKOA
Chama Cha Mapinduzi ( C C M ) , k i m e s e m a hakijahodhi wala
hakina nia ya kuhodhi mchakato wa Mabadiliko ya Katiba unaoendelea kama inavyosemwa na baadhi ya vikundi.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, aliyasema hayo
Mjini Dodoma jana wakati akifungua semina ya siku nne ya watendaji na viongozi
wa CCM ngazi za wilaya na mikoa nchini.
Alisema kilichofanywa na CCM katika mchakato huo ni kutoa maoni kama ilivyoelekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na si
vinginevyo.
Aliongeza kuwa, baadhi ya watu wanasambaza maneno ya uzushi
wakidai CCM inafanya hivyo kutokana na hofu ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu
2015 akiwafananisha na mfa maji ambaye haachi kutapatapa.
“Hayo ni mawazo ya mfa maji ambaye haachi kutapatapa. CCM haina
nia hiyo wala hatuna hofu,” alisema Dkt. Shein na kusisitiza kuwa, chama hicho
kilitoa maoni yake kama ilivyoelekeza tume
wakitarajia vyama vingine navyo vingefanya hivyo.
Alisema katika mapendekezo yao
ambayo yaliwasilishwa kwa tume hiyo, yamo yaliyotofautiana na yale yaliyomo
katika rasimu, lakini CCM imefanya hivyo kutokana na dhamira yake ya kweli
kuhakikisha nchi inapata Katiba Mpya yenye kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.
“CCM itaheshimu maoni ya Watanzania kupitia kura ya maoni wakati
ukifika...sisi hatujawahi kutamka na kudai maoni yetu ndio yachukuliwe na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema.
Aliwataka watendaji hao kufuatilia kwa makini mafunzo ambayo
watapewa ambapo mada 12 zitawasilishwa zikiwemo za maandalizi ya uchaguzi ili
kuwajengea uwezo wa kiuongozi na kiutendaji waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Taratibu za
kiutawala ni kwamba, Makatibu kazi yenu ni utendaji na kutoa ushauri wa
kitaalamu kwenye vikao vyenu. Haipendezi na haileti sura nzuri kama shutuma za kuvuruga mchakato wa uchaguzi kwenye
mikoa na wilaya zielekezwe kwenu.
“Msijihusishe na makundi yenye nia ya kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi kwani muda wa kufanya hivyo bado haujafika...muwe
nao kwa kuwa ni wanachama wenzetu katika chama lakini si kushirikiana nao
katika nia yao
ya kugombea,” alisema Dkt. Shein.
Dkt. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza
suala la maadili katika uongozi na utumishi wa chama akisema kuwa, kiongozi wa
CCM lazima awe kioo cha uadilifu mbele ya umma.
“Kiongozi wa CCM popote alipo, lazima awe
mfano wa mtu mwema mwenye kufuata maadili, uadilifu, maelekezo ya Sera za chama
chetu na kuzingatia sheria za nchi,” alisema.
Alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa CCM
ambao wamekuwa wakifanya vitendo kinyume na maadili na uadilifu, wajirekebishe
vinginevyo waachie ngazi.
Alisisitiza uadilifu, uaminifu na nidhamu ni
mambo muhimu katika kufanikisha ushindi wa chama chao ambacho hakiwezi
kuwavumilia watu wanaoharibu taswira ya chama mbele ya jamii.
Awali, akimkaribisha Makamu Mwenyekiti
kuyafungua mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Abdulrahman Kinana, alisema
miongoni mwa malengo ya mafunzo hayo ni kuimarisha chama hasa ngazi ya wilaya,
matawi na mashina.
Lengo jingine ni kuwajengea
uwezo wa kiuongozi na kiutendaji watendaji hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi
zaidi ambapo mafunzo hayo yatawapa fursa watendaji hao kujadiliana na
kushauriana namna ya uendeshaji shughuli za chama katika mazingira ya sasa.
No comments:
Post a Comment