- KILA CHAMA CHAMVAA KWA STAILI YA AINA YAKE
- VYAMTAKA AACHE KULAZIMISHA KUTAFUTA UMAARUFU
Vyama vya siasa vya CCM, CUF na NCCR-Mageuzi vimemshukia Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, kutokana
na kauli yake ya kumtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Mstaafu
Francis Mutungi, kusitisha ruzuku kwa vyama hivyo kutokana na kushindwa kuwasilisha
hesabu za fedha tangu mwaka 2009.
Vyama hivyo vimemtaka Zitto aache kukurupuka na kulazimisha
kutafuta umaarufu kwa kuandikwa kwenye vyombo vya habari.Kauli ya vyama hivyo, imekuja baada ya kamati ya PAC kudai kuwa
kukutana na Jaji Mutungi na kushindwa kutoa ripoti ya ukaguzi wa hesabu wa
vyama vya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP na vyama vingine vya siasa.
Kutokana na hali hiyo, Zitto alishauri ruzuku ya vyama hivyo isitishwe.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alimtaka Zitto, atoe kwanza
boliti kwenye macho yake ndipo aweze kuona kibanzi kilichopo kwenye macho ya
mwenzake.
Alisema CHADEMA n i miongoni mwa wahusika ambao hesabu zao
hazijakaguliwa, kwani ndicho kimekuwa kikilalamikiwa kuwa na matumizi mabaya ya
fedha za umma.Alisema chama chake hakihusiki kwani kimekuwa kikitekeleza wajibu
wake kwa mujibu wa sheria.
Alisema kwa mwaka 2009 hadi 2011 mahesabu ya CCM yalikuwa
yakikaguliwa na wakaguzi wa nje (TAC) na kwamba Januari, mwaka huu, CCM
iliiandikia barua ofisi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ya kuwasilisha rasimu ya hesabu za fedha za mwaka 2011/2012 kwa lengo la
kumtaka apangie chama hicho mkaguzi.
Alisema CAG alipangia TAC akague hesabu za chama hicho ambaye
alifanya kazi hiyo, hivyo chama hicho akihusiki."Hesabu zote
zilizokaguliwa zimewasilishwa kwa CAG, hivyo CCM haihusiki na agizo hilo na muda wowote PAC
akizihitaji itazipata," alisema Nape.
Alishauri vyama ambavyo PAC itabaini havikuwasilisha mahesabu yake
viongozi wake wawajibike.Kwa upande wa CUF, chama hicho kimesema Zitto
amekurupuka kwa kuwa hana taarifa za kutosha na hajui kinachojiri. "Mwenye
jukumu la kufuatilia hesabu hizo ni CAG ambaye hatujawahi kumsikia
akilalamika," alisema Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro.
Alisema CUF kila mwaka imekuwa ikifunga mahesabu kwa kukaguliwa na
wakaguzi wa ndani na nje, lakini hawajawahi kuona watu wa Serikali wakienda
kukagua hesabu hizo.Mtatiro alisema kuwa mwaka 2011 Serikali iliiandikia barua CUF ya
kupelekewa mkaguzi ambaye chama hicho kilitakiwa kumlipa, lakini walikataa.
"Tulijibu kuwa hilo
haliwezekani kwa kuwa hilo
ni jukumu la Serikali, kuanzia hapo hatukuwaona tena... hivyo Serikali imeshindwa
kutimiza wajibu wake," alisema.Mmoja wa viongozi wa NCCR-Mageuzi, aliyezungumza kwa sharti la
jina lake kutochapishwa gazetini, alisema kauli ya
Zitto ni ya kutafuta umaarufu kupitia vyombo vya habari na inaonekana haelewi
kinachoendelea.
Awali vyama vilikuwa vikifanya mahesabu vyenyewe na kupeleka
taarifa serikalini, lakini baada ya sheria kubadilishwa jukumu hilo (ukaguzi) alipewa CAG. Alisema CAG ndiye
anabidi aende kufanya ukaguzi huo, lakini tangu sheria hiyo ibadilishwe
hawajawahi kumuona.
Alisema baadaye Msajili wa vyama wakati huo
(John Tendwa) aliandikia vyama vya siasa barua ili viwe vinamlipa CAG kwa kazi
hiyo ya ukaguzi, lakini vilikataa kwani kufanya hivyo ni sawa na kumlipa
mshahara mara mbili, wakati analipwa na Serikali kwa kazi hiyo.
"Tulihoji iweje anapoenda kufanya ukaguzi
kwenye halmashauri alipwe na Serikali, lakini kwenye vyama alipwe na vyama
wakati Serikali inamlipa," alisema na kuongeza; "Tangu wakati huo
hatujawahi kumuona."
Alisema sio kweli kwamba vyama vinashindwa kuwasilisha mahesabu, bali
CAG ndiye hajafanya hivyo.Alitoa mfano kuwa mahesabu ya NCCR-Mageuzi yapo
tayari na kwa kawaida huwa yanakaguliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama
hicho. "Kwa hiyo kamati ya Zitto imekurupuka anatafuta umaarufu kupitia
kwenye vyama," alisema.
No comments:
Post a Comment