Na Elizabeth Mayemba
Wakongwe
wa soka nchini, Simba na Yanga jana zimetoka sare ya mabao 3-3 katika mechi ya
Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ilionekana kujiamini
zaidi kipindi cha kwanza na kuwabana wapinzani wao, hasa katika sehemu ya
kiungo na kuwafanya wachezaji wa Simba kuutafuta mpira kwa muda mrefu.
Mpira ulianza kwa Yanga
kuliandama lango la Simba na kufanya mashambulizi mfululizo lakini
washambuliaji wake hawakuwa makini kutumbukiza mpira kimiani.Simba walizinduka dakika ya 14
ambapo, Said Nassoro 'Cholo' alikosa bao baada ya kuwapangua mabeki wa Yanga na
kupiga shuti, lililotoka nje.
Yanga ilipata bao dakika ya 16
baada ya beki wa Simba, George Owino kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa.Dakika ya 24, David Luhende
aliikosesha Yanga bao baada ya kuunasa mpira miguuni mwa Abdulhamud Humudi,
ambapo alipiga shuti lililotoka nje ya lango, huku Hamis Kiiza, naye akipiga
shuti lililodakwa na kipa Abel Dhaira.
Kiiza aliipatia Yanga bao la
pili, baada ya kuunganisha mpira uliorushwa na beki Mbuyu Twite.Ramadhan Singano 'Messi',
aliikosesha Simba bao dakika ya 44 baada ya kupata nafasi nzuri lakini shuti
lake likadakwa na kipa Ally Mustafa 'Barthez'.
Yanga ilipata bao dakika ya 45
kupitia kwa Hamis Kiiza, baada ya kuunganisha pasi ya Didier Kavumbagu.Kipindi cha pili Yanga iliingia
na kufanya mashambulizi ambapo dakika 62, Haruna Niyozima aliikosesha Yanga bao
la wazi baada ya kupokea pasi nzuri ya Kavumbagu lakini mabeki wa Simba
wakaokoa.
Simba ilipata bao la kwanza
dakika ya 64 kupitia kwa Patrick Mombeki, huku beki George Owino akifunga la
pili kwa kichwa akiunganisha kona ya Singano.Amis Tambwe aliisawazishia Simba
bao la tatu dakika ya 77 baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na
beki, Said Masoud 'Cholo'.
Dakika ya 40, Simba ilimtoa
Mombeki baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Zahoro Pazi.
Naye Fatuma Rashid, anaripoti
kuwa, baadhi ya mashabiki wa timu hizo walipoteza fahamu, kila bao lilipokuwa
likifungwa.Kipindi cha kwanza mashabiki wa
Yanga zaidi ya sita walipoteza fahamu baada ya timu hiyo kupata mabao 3.Lakini hali
ilibadilika kipindi cha pili ambapo mashabiki wa Simba zaidi ya saba, nao
walianza kupoteza fahamu kila ilipokuwa ikipata bao.
No comments:
Post a Comment