Vijana wakinawa uso baada ya polisi kupiga mabomu ya machozi
Wakazi wa Mbeya wakikimbia baada ya polisi kupiga mabomu ya machozi.
- WAFANYABISHARA WAZIPINGA MASHINE ZA TRA
Na Esther Macha, Mbeya
Vurugu kubwa zimeibuka mkoani Mbeya jana
baada ya Jeshi la Polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya
wafanyabiashara waliokuwa wakipinga agizo la Serikali linalowataka watumie
mashine za kieletroniki kutoa risiti kwa wateja wanaonunua bidhaa zao.
Polisi
walitumia mabomu hayo na maji ya kuwasha katika mitaa mbalimbali ya eneo la
Mwanjelwa hadi Viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe. Gari lililokuwa na
askari polisi, lilitoa matangazo ya hali ya hatari kuwataka wananchi wasitoke
nje katika nyumba zao.
Mabomu mengine
yalipigwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kagera, uliopo eneo la Soweto ambapo hali ya
taharuki ilijitokeza baada ya mabomu hayo kuwaathiri wanafunzi waliokuwa
darasani wakisoma ambao walianza kukimbia ovyo na wengine kuzimia.
Wafanyabiashara
hao wanapinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), kuwataka kununua mashine
hizo ili kukatia risiti kwa wateja wanaonunua bidhaa zao.
Vurugu hizo
zimetokea siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Abbas Kandoro, kukutana na
viongozi wa wafanyabiashara wa Soko la Sido ambapo katika kikao hicho aliwataka
viongozi hao kuwajulisha wenzao wasiitishe mkutano waliotaka kuufanya jana katika
Uwanja wa Shule ya Msingi Runda Nzovwe.
Bw. Kandoro
alilazimika kukutana na viongozi hao baada ya gari la matangazo kupita mitaa
mbalimbali ya jiji hilo likiwataka
wafanyabiashara kufunga maduka yao
siku ya jana na kufika katika uwanja huo ili kujadili matumizi ya mashine hizo.
Baada ya Bw.
Kandoro kusikia ujumbe huo, ilidaiwa dereva wa gari hilo alikamatwa na Jeshi la Polisi pamoja na
Mwenyekiti wa Soko la Sido ambao waliwekwa ndani kwa muda usiojulikana.
Wafanyabiashara
hao walikataa kusitisha mkutano huo hivyo kuendelea na maandalizi ambapo jana
asubuhi, walikodi gari lingine na kuwatangazia wenzao wajitokeze kwa wingi
katika mkutano kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi na Runda Nzovwe.
Kutokana na
msimamo huo, polisi walifika eneo hilo
ili kuwazuia wafanyabiashara hao wasifanye mkutano huo kwa kupiga mabomu ya machozi
na kutumia maji ya kuwasha.
Akizungumza na Majira, mmoja wa
wafanyabiashara hao, Bw. Alex Oswald, alisema waliamua kufunga maduka yao kwa hiari waweze
kufanya mkutano ili watoke na msimamo wa kuiomba Serikali itoe mashine hizo
bure kwa wafanyabiashara badala ya kuwauzia.
Mfanyabiashara mwingine wa Soko la Sido, Bw.
Peter Tweve, alisema wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wapewe
bure kwani si kila mfanyabiashara anayeweza kununua kwa sh. 800,000 kiasi
ambacho ni kikubwa ukilinganisha na mitaji yao.
Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Bw. Kandoro alisema
yupo katika kikao ambapo simu ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Diwani
Athumani, ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Vurugu hizo zimetokea wiki moja tangu
Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi Makao Makuu ya TRA, Richard Kayombo, kutoa taarifa
zinazosema kuwa, mwisho wa kununua mashine hizo ni Oktoba 14, mwaka huu.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa,
masoko yote ya Uyole na Mbalizi, hakuna duka lililokuwa limefunguliwa siku ya
jana na polisi waliendelea kupiga mabomu ili kuwatawanya wananchi.
mashine hizi ni mradi tu wa wakubwa mambo ya ten pacent inashangaza vipi nchi zilizoendelea km china india thailand nk hawatumii mashine hizi ila ktk super market na maduka makubwa leo hapa bongo eti ndo tumeendelea hata machinga watumie mashine Pole Rais Kikwete mafisadi wanakuandama katika kila sekta
ReplyDeleteHayo maisha bora kwa TRA tu? waache watanzania nao wajikwamue, tafuteni kodi kwenye vyanzo vingine kama madini
ReplyDeletemuuza duka ni wakala tu wa TRA ni vipi anunue hiyo mashine kwa sh.800,000 badala ya kugawiwa bure. Aafu RC na wewe acha kutoa amri haraka haraka bila hata ya kuwa na mazungumzo na wahusika. huoni kama unaanzisha vurugu ? MOLMOLI BEE.
ReplyDeleteHizo mashine mbona zinatofautiana bei na TRA inawalazimisha wafanyabiashara kununua mashine hizo sehemu moja tu wakati mashine hizo zinauzwa sehemu mbalimbali huo ni ufisadi wa viongozi wa TRA.
ReplyDelete