- WAPORA MAMILIONI,WAJERUHI ABIRIA
Na Damiano
Mkumbo, Singida
Majambazi waliokuwa na silaha, wameliteka basi la Kampuni ya Taqwa
linalofanya safari zake kati ya Bunjumbura, Burundi na Dar
es Salaam. Katika tukio hilo,
abiria waliokuwa ndani ya basi hilo
waliporwa fedha za Kitanzania zaidi ya sh. milioni tano pamoja na dola za
Marekani 160,000.
Tukio hilo limetokea juzi saa 4
usiku katika Kijiji cha Milade, Kata ya Iguguno, Wilaya ya Mkalama, mkoani
Singida, Barabara Kuu ya Singida-Shinyanga. Basi hilo lilikuwa na abiria 51 ambapo majambazi
hao walitega mawe makubwa katika eneo lenye daraja.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani humo,
Geofrey Kamwela, alisema licha ya majambazi hao kupora fedha na mali za abiria,
pia waliwapiga, kuwajeruhi kwa marungu na mawe.
“Abiria 19 walijeruhiwa na kupelekwa Hospitali
ya Rufaa Mkoa wa Singida, basi lililotekwa lina namba T 298 BLD, aina ya Nissan
Disel BLD likitokea Bunjumbura kwenda Dar es Salaam, likiendeshwa na Bw. Ahmed
Seif (39), akiwa na abiria kutoka nchi
za Rwanda, Burundi na Congo (DRC).
“Baada ya kufika eneo lililowekwa kizuizi cha
mawe makubwa, dereva alijaribu kupita lakini tairi mbili za mbele zilipasuka
hivyo gari liliacha
barabara na kuserereka chini umbali wa meta 100 na kusimama,” alisema Kamanda
Kamwela.
Alisema baada ya basi hilo
kusimama, watu wapatao sita wakiwa na marungu, mawe walilivamia basi hilo, kuvunja madirisha,kuingia
ndani na kuwaamuru abiria wateremke chini.
Kamanda Kamwela alisema majambazi hao
walianza kumpora abiria mmoja mmoja vitu mbalimbali kama
fedha, simu, kamera za mnato na mabegi madogo huku wakiwapiga.
“Katika tukio hili,
abiria 28 waliporwa kati yao 19 wanaume na wanawake 12, pia kuna abiria ambao
walijeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao,”
alisema.
Aliongeza kuwa, mmoja kati ya majambazi hao
alikuwa ndani ya basi hilo akiwasiliana na
wenzake ambaye ndiye aliyekuwa akiwalazimisha abiria kuteremka chini wakiwemo
wanafunzi watano wa Vyuo Vikuu vya Harare na Maputo.
Alisema polisi walifika eneo la tukio dakika
20 baada ya watu hao kufanya uhalifu huo na kukimbia kusikojulikana. Daktari wa
zamu katika hospitali hiyo, Dkt. Banuba Deogratius, alisema wanaume 12 na
wanawake saba walipokelewa, kupatiwa matibabu na kuruhusiwa.
Kamanda Kamwela alisema
jeshi hilo
linaendelea na uchunguzi ili kuwanasa watu hao hivyo aliwaomba wananchi watoe
taarifa polisi zinazohusiana na viashiria vya kuonekana watu hao.
No comments:
Post a Comment