Na Goodluck Hongo
Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, jana imekabidhi vifaa
mbalimbali vya michezo kwa timu ya wahariri wa vyombo vya habari na timu ya
waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni
3.5.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja
Uhusiano wa Mambo ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalimu alisema wameamua kutoa vifaa
hivyo kutokana na umuhimu wa vyombo vya habari kwa umma.
Alisema licha ya Vodacom kudhamini Ligi Kuu
Tanzania Bara, lakini pia wanaendelea kudhamini mashindano mengine hivyo kwa
mechi ya wahariri na waandishi wa habari ni muhimu kutokana na wahariri wengi
kukosa nafasi hata ya kucheza mpira.
“Tumekutana na wahariri mara tatu na walipoomba
udhamini kwetu sisi tulikubali na kuamua kutoa vifaa hivi kama
jezi, viatu, mipira na suti za michezo ambapo licha ya vifaa hivyo lakini
mshindi katika mechi hiyo atapata jezi,” alisema Mwalimu.
Naye nahodha wa timu ya jukwaa la wahariri,
Kulwa Karedia ambaye ni Mhariri wa gazeti la Mtanzania alisema
wanaishukuru kampuni hiyo kwa mchango wao wa kutoa vifaa hivyo, ili kufanikisha
mechi hiyo ya aina yake ambayo itachezwa Jumamosi mkoani Iringa.
Alisema wao wamejiandaa vizuri kwa kuishinda
timu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa (Iringa Press Club) kwa kuwa
wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo, baada ya kufanya mkutano wao na
Kampuni ya Vodacom uliofanyika mkoani humo.
“Tunaishukuru mno Vodacom kwa
msaada huu walioutoa, ili kufanikisha mechi yetu hasa sisi watu wa habari,
lakini kama wahariri tumejiandaa vizuri katika
mechi hiyo na tutashinda,” alisema Karedia.
No comments:
Post a Comment