Adolf Mkono
‘‘ CCM wanaona jinsi wapinzani wao wanavyozidi kuimarika siku hadi
siku na kujua matokeo halisi ya idadi za kura walizopata wao dhidi ya mpinzani
wao na kuzifanyia kazi
Harakati za kinyang'anyiro cha kiti cha
urais mwaka 2015 kimekuwa kikivitesa vyama vya siasa na baadhi ya wanasiasa
huku wananchi wakiendelea kutaabika kwa ukali wa maisha.Baadhi ya
wanasiasa wamediriki kutamka wazi kuwa watagombea katika kiti hicho na kuzua
malumbano kwa wananchi wao badala ya kusimamia shughuli za maendeleo kuwakomboa
wananchi wao.
Ni rahisi
kutambua kuwa harakati za chini na zingine za wazi kwa vyama hivyo kikiwemo CCM
kama chama tawala tangu kumalizika kwa
uchaguzi mkuu 2010, inatoa maana moja tu kubwa kuweka mazingira sawa katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hatua hii ya
kila chama kuhangaika mapema kiasi hiki huku ikiwa ni nusu ya kipindi kingine
cha uchaguzi ni ishara nzuri kwa ukuaji na kukubalika kwa mfumo wa vyama vingi
kwa sehemu kubwa ya Watanzania tofauti na miaka ya nyuma.
Hali hii inaashiria
kuwa uchaguzi ujao utakuwa mgumu kwa pande zote kutokana na maandalizi
yanayoendelea sasa.Wananchi
wamefunguka na kufuatilia yanayoendelea, hivyo ni wakati mwafaka kwa serikali
pia kulinda amani iliyopo kwa gharama yoyote ili kuepusha migogoro baada ya
uchaguzi ambayo mwisho wa siku hurudisha nyuma maendeleo.
Wakati huu
tunapoendelea na mchakato wa katiba mpya ni vizuri sasa wananchi wakasikilizwa
kile wanachokitaka kwani wengi wao wamekuwa wakitoa maoni kuhusiana na suala
hilo.Harakati
zinazoendelea kwa vyama vya siasa na hapa hebu tuanze na CHADEMA chama ambacho
katika uchaguzi wa rais 2010 kilimsimamisha Dkt.Wilbroad Slaa kama mgombea
hatua iliyomtoa katika nafasi yake ya ubunge.
Matokeo yake
ikawa ni kuwa nje ya uwakililishi wa wananchi atakisaidia vipi chama chake hasa
ikizingatia njia aliyoitumia kukijenga ilikuwa ni kupitia bunge alikoibua
madudu ya EPA na RICHMOND na kusababisha matokeo mabaya ya CCM kwa uchaguzi wa
mwaka 2010.
Waswahili husema,
adui yako muombee njaa! Na kama CCM walifuata kanuni hiyo ukweli ni kwamba
watakuwa wanakosea na kama hawaamini watakuja kugundua hilo wakiwa tayari
wamechelewa.Sidhani kama wanaweza
kujisahau kiasi hicho, imani yangu ni kuwa wanafuatilia kila hatua inayoendelea
ndani ya chama hicho ndio maana hawataki kubweteka hata kidogo.
Moja ya kitu
walichokigundua CHADEMA ni udhaifu wa uongozi ndani ya chama hicho hasa ngazi
za matawi, kata, wilaya na majimbo, kazi ambayo Dkt.Slaa kama katibu mkuu wa
chama amekuwa akiifanya ukaguzi na kuhakikisha anaweka uongozi imara kwa ngazi
hizo ambayo tayari imekamilika zaidi ya wilaya 150.
Kwa yoyote
atakayeteuliwa na CHADEMA kupeperusha bendera yake katika nafasi ya urais
ataingia kwenye kinyang'anyiro huku akiwa na imani kubwa kuwa kweli nyuma yake
ana 'makamanda' wa uhakika kama wao wanavyopenda kujiita na ikumbukwe kuwa kwa
kazi inayoendelea ni vigumu CCM kupata viti vya bwerere kama ilivyopata awali.
Hali ikiwa hivi
upande wa chama kikuu cha upinzani kwa sasa CHADEMA, CCM nao hawajalala japo
mbinu zao ni tofauti kidogo na wenzao wa upinzani maana kama ni kuimarisha
ngazi za chini tayari mwasisi wa chama hicho upande wa bara Hayati Baba wa
Taifa Julius Nyerere aliifanya.
Kwa matukio ya hivi
karibuni yanayoendelea ndani ya chama tawala na serikali yake ni vigumu kuamini
kama yanatokea kwa bahati mbaya ama kusudi.Kuna watu wanabeza
uteuzi wa sekretarieti iliyopo ila ukweli ni kwamba inajua kucheza na rika la
vijana ambalo ndilo tishio kwa ustawi wa chama chochote.
Hivi karibuni
tulisikia CCM wakianzisha kanda maalum upande wa wanafunzi wa elimu ya juu eneo
lililotumiwa na CHADEMA miaka michache iliyopita na kuleta ufanisi mkubwa kwa
matunda ya akina Zitto, Mnyika na Mdee, ambao tayari kwa sasa ni nguzo za chama
hicho.
Kuna dhana kwamba
sekretarieti hiyo inaendeleza mpasuko wa makundi ya chama hicho moja likiwa
lile la watuhumiwa wa ufisadi na wapinga ufisadi ndani ya CCM.Katika hili, ukweli
ni kwamba kundi lisilopenda maendeleo ya chama ni vigumu kwao kukiacha chama
chao tofauti na vijana ambao kuhamia upinzani kwao ni kitendo cha kishujaa na
zaidi ya hapo tofauti zao zitafikia mwisho baada ya CCM kumpata mgombea wake wa
urais 2015.
Watuhumiwa wa ufisadi
wanaweza kuwa na tofauti na mapungufu mengi lakini tukumbuke CCM kuondoka
madarakani ni vigumu kwao kubaki salama japo kuna wanaoonekana kama vinara wa
ufisadi lakini ukweli ni kwamba hapo hakuna aliye msafi kiasi cha kuamini
kwamba nje ya serikali ataendelea kuwa salama si kwa sababu viongozi wa sasa ni
mafisadi la hasha!
Bila shaka CCM wanaona
jinsi wapinzani wao wanavyozidi kuimarika siku hadi siku na kujua matokeo
halisi ya idadi za kura walizopata wao dhidi ya mpinzani wao na kuzifanyia
kazi.Na kama hali
itaendelea kuwa hivyo ya kushindwa kuisambaratisha CHADEMA itabidi sasa CCM
wajisalimishe kwa mtu mmoja ndani ya chama hicho ili kuibuka kama mgombea
binafsi kwa ajili ya kupunguza kura za mpinzani wake.
Tukiendelea na
mchakato wa katiba mpya, ni wakati wa kuyarekebisha yote yanayokinzana na vyama
vingi kama, matokeo ya urais kupingwa mahakamani.Hii ni moja ya sababu
iliyokuwa ikichangia msukumo wa madai ya katiba mpya kwa wapinzani. Sasa hivi
CCM ndo wameanza kulipigia chapuo jambo hili katika mchakato wa katiba mpya.
Katiba iliyopo sasa
rais aliyepo madarakani alikuwa akiingia kwenye kinyang'anyiro cha nafasi hiyo
huku akiwa bado ndiye rais wa nchi ukiachilia yeye kuvunja Bunge na baraza lake
la mawaziri hili linatakiwa kutazamwa ili kuondoa utata.
Wapo waliokuwa
wanaona ni vyema serikali ikawa chini ya muhimili mmojawapo kati ya Bunge au
mahakama japo kila sehemu ina changamoto zake, ukisema dola kwa kipindi hicho
iwe upande wa mahakama kuna uwezakano wa kuibuka hoja mkuu wa muhimili huo kuwa
mteule wa rais na kama litakuwa Bunge.
Pia, kuna hoja ya
spika kuwa sehemu ya chama tawala, wakati hayo yote yakihitaji majadiliano
tayari CCM wameisha kubali matokeo kupingwa mahakamani, inawezekana baadhi ya
changamoto zikapatiwa ufumbuzi ila ni ngumu madai yote kupita kama
yanavyopendekezwa na wapinzani.
Kiongozi mwenye nia
thabiti ni yule anayeumia kwa ajili ya wananchi wake, ni wakati mwafaka sasa
kutafuta njia ya kuwatoa wananchi katika hali ya ugumu wa maisha na kupanda kwa
bidhaa ili kuongeza uzalishaji katika taifa.
.
No comments:
Post a Comment