21 October 2013

RUSHWA IMETUPOFUSHA MACHO, TUNASUBIRI KUTUMBUKIA SHIMONI



Daniel Samson
"Dawa ya rushwa sio kulaumiana au kunyoosheana vidole na wengine kujiona watakatifu na rushwa haiwaathiri, lakini mapambano ha yanahitaji utashi na dhamira ya dhati kwa kila raia
"RUSHWA adui wa haki" ni msemo uliotumika sana na mwasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Nyerere katika harakati zake za kupinga utoaji na upokeaji rushwa ambayo ililenga kupotosha haki na usawa miongoni mwa wananchi.

Msemo huu haukutumika katika maneno bali alipinga rushwa kivitendo na kuhakikisha viongozi na wananchi wanaepukana na mdudu rushwa na kujenga jamii inayoheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu.
Kutokana na mfano mzuri wa Mwalimu Nyerere aliouonyesha kupambana na vitendo vyote vya kidharimu, viongozi na raia wote waliiga mwenendo wake na taifa lilithamini usawa na haki kwa watu wote bila kujali matabaka.
Hata chama ambacho alikuwa anakiongoza ambacho kinashika dola mpaka leo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika katiba yake kina kipengele cha ahadi za mwanachama ambazo kila mtu aliyetaka kujiunga na chama hicho alitakiwa kuapa au kutamka kwa dhati kabla ya kukubaliwa kuwa mwanachama wa chama hicho.
Ahadi namba nne inasema "Rushwa ni adui wa Haki, Sitapokea wala kutoa rushwa" maneno haya yalichukuliwa kwa uzito mkubwa kwa sababu Mwalimu Nyerere aliamini nguvu iliyopo katika kukiri jambo ili kila mwananchama wakati huo awe hodari wa kupinga rushwa.Na mara kwa mara wanachama walikumbushwa ahadi hiyo kwa lengo la kukiimarisha chama, lakini sidhani kwa wakati huu kama ahadi hiyo inatendewa kazi kama zamani.
Ahadi hiyo ilikuwa ni nuru sio tu kwa wanachama wa CCM bali kwa taifa lote. Faida ilionekana katika upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile maji, umeme, hospitali, elimu, makazi na chakula ambapo kwa kiasi kikubwa zilikuwa za kuridhisha kulingana na uchumi wa wakati huo ambao ulikuwa unategemea zaidi kilimo cha mazao ya biashara. Haki haikupatikana kwa fedha wala vitu bali kwa utu na upendo.
Hali ya mambo ni tofauti na wakati huu, hata wanachama wa chama hicho wengi wao wametuhumiwa kwa nyakati tofauti kuhusika na ufisadi mkubwa kama wa RICHMOND, EPA, KAGODA n.k.
Hii ni udhihirisho kuwa ahadi hiyo haina nguvu tena kama ilivyokuwa wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, ambapo kila mtu aliogopa kujiingiza katika vitendo vya kupokea na kutoa rushwa ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi wote bila kujali matabaka.
Rushwa imekuwa rafiki wa haki na wapo baadhi ya watu hasa vijana kukiri waziwazi kupokea na kutoa rushwa ili wapate haki kwa kisingizio kuwa bila 'mlungula' hakuna jambo linalowezeka.
Dhana hii potofu haipaswi kuachwa iote mizizi kwa sababu inalenga kuwanufaisha watu wachache na familia zao kwa njia zisizo halali.
Lakini umaskini walionao Watanzania wengi unawalazimisha kujiingiza katika vitendo hivyo vya kidharimu kwa sababu baadhi ya mifumo ya uongozi inatoa mianya ya kupindisha haki.
 Katika hali ya kawaida inaonekana rushwa inarahisisha upatikanaji wa stahili za maisha, lakini upande wa pili rushwa inaliangamiza taifa letu kwa kiasi kikubwa na kutishia kutoweka kwa amani na utulivu wetu ambao tumeujenga kwa muda mrefu sasa.
 Sio ajabu ukamuona mtumishi wa umma aliyeajiriwa takribani mwaka mmoja akimiliki magari, nyumba za kifahari ambazo kwa akili ya kawaida haiwezekani mtu kuzipata ndani ya mwaka mmoja kulingana na mshahara wake. Matokeo yake ni rushwa kutaka utajiri wa haraka haraka.
  Watawala na raia wamepigwa upofu, hakuna aonaye tumebaki kulaumiana sisi kwa sisi, tukijiuliza kwa nini taifa letu haliendelei kiviwanda, kilimo chetu ni cha kusuasua, tatizo la ajira linaongezeka maradufu, tindikali na visasi baina ya wanasiasa. Wananchi wamelala usingizi wa pono hawaoni tena, hata viongozi ambao ni dira ya taifa nao wameshindwa kupata dawa ya rushwa.
  Wengine wanajitenga kwa kisingizio kwamba wao hawatoi na kupokea rushwa na kujiona wako salama, lakini ukimya wao wa kutokukemea vitendo vya rushwa unazidi kuliangamiza taifa.
  Nchi ya Mexico imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa dawa za kulevya kwa sababu walichelea kudhibiti biashara hiyo mapema badala yake waliendekeza rushwa ili kuruhusu matumizi ya dawa hizo kwa njia zisizo halali.
  Leo utu wa mtu unapimwa kwa fedha na sio thamani aliyonayo, mfano askari wa barabarani akipokea rushwa ya shilingi 10,000 basi utu wake unalinganishwa na fedha hiyo. Kama tumefikia hatua hii tuko pahali pabaya kwa sababu hakuna kitu ambacho kinaweza kulinganishwa na uhai wa mtu.
  Watu wanathamini vitu kuliko utu, chuki na uhasama umeongezeka katika jamii yetu kwa sababu ya rushwa ambayo inazidi kuhalalishwa na hata wale watu wanaoaminika katika jamii kusimama kupinga upotoshaji wa haki, nao kwa wakati tofauti wamejiingiza katika kadhia hiyo.
  Kuaminiana hakupo tena, Watanzania ambao miaka ya nyuma tuliheshimiana na kuaminiana katika mambo mengi, leo tumegeuka kuwa wanyama kiasi kwamba watu wanaogopa kula na kunywa pamoja kwa kuhofia kuwekewa sumu.
  Tafiti kadhaa zinaonyesha kuwa Watanzania sita kati ya 10 hawaaminiani katika kutekeleza mipango waliyojiwekea, tafsiri yake ni ubinafsi umetawala.
  Kukithiri kwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya, vitendo vya kutekwa na kuteswa kwa baadhi ya watu, kumwagiwa tindikali. Kutakatisha fedha kwa kujenga majumba ya kifahari maeneo ya mijini ni matokeo ya watu fulani wenye maslahi yao binafsi kutumia pesa walizonazo kufanya vitendo vya kihalifu ili kupindisha haki na ukweli.
  Tunalipeleka wapi taifa hili ikiwa watu wanaopokea na kutoa rushwa ili kupotosha haki na kupora ardhi, mali za wananchi maskini, wanaonekana kama mashujaa na mfano wa kuigwa katika jamii. Wengi wanahoji kwanini hatuendelei ikilinganishwa na rasilimali nyingi tulizonazo, jibu ni rahisi tumekithiri katika rushwa.
  Nchi ya China ambayo ni taifa kubwa duniani lenye uchumi imara, limefika hapo lilipo kwa sababu viongozi na raia wake wanatambua wazi madhara ya kuendekeza vitendo vya kupokea hongo.
  Sio ajabu kuona taifa hilo limejiwekea sera na sheria nzito za kupambana na rushwa ambazo hazichagui viongozi wala raia, wote huwajibika kwa majukumu na wadhifa walionao katika taifa.
  Sheria ya kunyonga ambayo inatumika China imesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo hilo, ingawa ni kinyume cha haki za binadamu.
  Dawa ya rushwa sio kulaumiana au kunyoosheana vidole na wengine kujiona watakatifu na rushwa haiwaathiri, lakini mapambano haya yanahitaji utashi na dhamira ya dhati kwa kila raia.
  Tufahamu kuwa kupokea na kutoa rushwa ni tabia ambayo hujidhihirisha pale mtu anapotaka apewe fedha au vitu ili atimize au atimiziwe wajibu isivyo halali.
  Katika mapambano haya tunatakiwa kushughulika na saikolojia za watu na sio matokeo ya kile kinachotendwa, ingawa adhabu ni sehemu ya kubadilisha tabia ya mtu lakini ni zaidi ya hapo kama wananchi watakuwa na hofu itakayowafanya kuogopa rushwa kama wanavyoogopa moto.
  Hofu ambayo mtu anaumbiwa katika akili yake inamfanya mtu kuchukia matendo yote ambayo yatawadhuru wengine na hata yeye akitendewa hatafurahia kutendwa. Na hivi ndivyo Mwalimu Nyerere alivyotumia weledi wake kuwaaminisha watu ubaya wa rushwa katika maendeleo ya taifa.
  Tufike mahali Watanzania, kukataa rushwa kwa vitendo na kuungana pamoja kubadilishana tabia zetu ili wote tunufaike na rasilimali zetu kwa haki na usawa. Tukiliacha tatizo hili liendelee kukita mizizi hakuna atakayesalimika na matokeo ya rushwa.
  Mabadiliko yanaanza na wewe, kuwa sehemu ya mabadiliko katika nafasi uliyonayo ili taifa liepuke kuingia katika migogoro ambayo itakuwa vigumu kutoka. Rushwa hupofusha macho tusipoangalia tutatumbukia shimoni wote.






No comments:

Post a Comment