22 October 2013

UHARIBIFU WA MAZINGIRA UNAKWAMISHA MAENDELEO NCHINI



Na Ramadhan Libenanga
Kasi ya maendeleo katika nchi zinazoendelea inaweza kurudi nyuma miaka mitano ijayo, iwapo hatua thabiti hazitachukuliwa kupunguza kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti ya 2011 kuhusu Uendelevu na Usawa ilieleza kuwa, uendelevu wa mazingira unaweza kufikiwa kwa njia ya haki na yenye matokeo mema iwapo masuala ya afya, elimu, kipato na tofauti za jinsia kuchukuliwa hatua za kimataifa kuhusu uzalishaji.
Uharibifu wa mazingira unatishia uhai wa viumbe duniani kwa kiasi kikubwa hutokana na shughuli mbalimbali za wanadamu ikiwemo ukataji miti na kuchoma moto misitu ya asili.
Msisitizo mkubwa umekuwa ukifanywa na wadau wa mazingira kwa kuhakikisha mikataba na sheria zinawekwa ili kulinda, mazingira na viumbe adimu wasitoweke.
Wilaya ya Kilombero ni moja ya wilaya iliyobarikiwa kuwa na mito zaidi ya 20 kati yake mito mikubwa 9 isiyokauka maji kwa kipindi cha mwaka mzima Mbali na vivutio hivyo, kumekuwa na uelewa mdogo wa masuala ya uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji .
Ukosefu wa elimu katika vijiji mbalimbali ndani ya wilaya hiyo umesababisha wananchi kushindwa kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji vilivyowazunguka katika maeneo yao.
Tatizo la uharibifu wa mazingira na uchafuzi wa vyanzo vya maji ni baadhi ya sababu kubwa zinazochangia upungufu wa maji na mabadiliko ya tabia nchi .
Ongezeko la watu na kukua kwa shughuli za kiuchumi pia, ni chanzo cha ongezeko la matukio ya uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji katika maeneo hayo.
Hivi karibuni katika Kijiji cha Sanje Tarafa ya Kidatu, Wilaya ya Kilombero, kulikuwa na mgogoro wa wananchi na kufikia hatua ya kuziba barabara kuzuia magari yaendayo makao makuu ya wilaya hiyo kupitika kwa urahisi baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho na wajumbe wawili kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuharibu vyanzo vya maji .
Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakiathiri kwa kiasi shughuli za maendeleo hasa katika sekta ya kilimo , kutokana na mfumo wa wakulima nchini kutegemea mvua za masika.
Mwenyekiti huyo hakusita kueleza ukweli katika suala zima la tuhuma zinazowakabili mpaka kufikia kuingia hatiani kuwa ukosefu wa elimu juu ya masuala ya uhifadhi wa mazingira , ardhi na vyanzo vya maji kwa viongozi katika Serikali za mitaa .
Mwenyekiti huyo alikiri kutenda kosa hilo kwa kisingizio cha kukosa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji na ardhi.Ofisa wanyamapori Wilaya ya Kilombero, Bw. Madaraka Aman anasema kuwa, uongozi wa serikali ya kijiji hicho ulichepusha mto Sanje kwa lengo la kutaka kujinufaisha wenyewe badala ya manufaa kwa wananchi .
Anasema, azimio la mwaka 1970 la mkutano uliofanyika katika mji mdogo nchini Iran unaotambulika uliweka mikataba ya kuhifadhi ardhi oevu kwa lengo la kulinda, mito, mazingira na vyanzo vya maji.
  Mkataba huo unatahadharisha na kutaka udhibiti wa mambo yanayohatarisha uharibifu wa mazingira kama kuziba mito, kuchepusha mito, kukausha, kuchimba mawe katika vyanzo vya maji pia, shughuli zote zenye kuhatarisha mazingira .
  Anasema, sheria hiyo inapaswa kuzingatiwa na idara za Serikali ikiwa ni pamoja na mamlaka za maji , ambapo katika sheria hiyo kifungu cha 8 kinatamka kuwa ‚"maji yote yaliyopo Tanzania ni mali ya jamhuri ya muungano,".
  Kwa mujibu wa sheria hiyo maji ni rasilimali ya taifa ,hakuna umiliki binafsi wa rasilimali za maji hata kama yapo au yanapita katika eneo la makazi ya watu.
  Anasema, mtu ama taasisi anaweza kupewa haki ya kutumia na sio kumiliki ambapo, haki hiyo hutolewa na ofisi za mabande tu hivyo kwa misingi hiyo uongozi wa Serikali ya kijiji ulifanya kosa kwa kujua ama kutojua sheria .
  Anasema kuwa, sheria hiyo inasema baadhi ya miradi haitaruhusiwa kutekelezwa kabla ya kufanywa tathmini ya uharibifu wa mazingira.Anaeleza kuwa, adhabu ya kosa hilo ni kuwa mtuhumiwa yeyote atakayeingia hatiani kwa makosa ya sheria hiyo atapewa adhabu ya faini kiasi cha shilingi 50,000 mpaka milioni 50 ama kifungo cha kuanzia miaka mitatu mpaka saba .
  Kifungu hicho kitamhusu mtu ambaye atakiuka kifungu cha sheria namba 57 ya mazingira bila kujali nyadhifa yake ndani ya Serikali au chama Hata hivyo Bw.Madaraka anadai kuwa sekta ya maliasili imekuwa ikikwamishwa kutekeleza baadhi ya majukumu kutokana na kuingiliana na masuala ya kisiasa wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu za kazi.
  Anadai kuwa, baadhi ya wanasiasa wamekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira katika maeneo yao, kwa kuona nafasi zao za kisiasa katika uvunjwaji wa sheria katika idara ya maliasili .
  Anasema, kesi nyingi za maliasili itikadi za kisiasa zimekuwa zikiingia na hivyo kuwafanya wataalamu wa idara hiyo kushindwa kutekeleza wajibu wao .Amewataka viongozi wa kisiasa, kutoingilia shughuli na utekelezaji wa udhibiti wa matukio ya uharibifu wa mazingira na badala yake waendelee kufanya shughuli zao
  "Wanasiasa wamekuwa kikwazo katika kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria" anasema Bw. Madaraka.Anasema, majukwaa ya kisiasa yanatakiwa kutumika kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao, badala ya kuwapotosha pale wanapoingia hatiani na kuwashawishi kufanya maandamano yasiyo na msingi





No comments:

Post a Comment