22 October 2013

TAMWA IUNGWE MKONO KUPIGANIA USAWA WA KIJINSIA



Alexander Joseph
"Tofauti hii inatokana na ukweli kuwa, hicho ni kipindi cha ongezeko la talaka na kasi ya watoto kubaki wakilelewa na mama wa kambo.
  Tofauti na ilivyo ada kwa jamii nyingi za Kitanzania kwamba wakati wa mavuno jamii nzima katika familia tangu watoto, wanawake na wanaume huwa na kipindi cha furaha, hali ni tofauti katika wilaya ya Newala kwani hicho ni kipindi cha majuto na maumivu kwa wanawake na watoto.
Tofauti hii inatokana na ukweli kuwa, hicho ni kipindi cha ongezeko la talaka na kasi ya watoto kubaki wakilelewa na mama wa kambo.
Mwandishi Flora Nzema ameandika katika Sauti ya Siti, la Juni 2013, akisema, "Ni wakati ambao kaya nyingi husafisha maghala kwa ajili ya mazao mapya, pia ni wakati ambao kaya nazo 'husafishwa' upya na katika zoezi hilo, wake wengi wa zamani nao hutalikiwa na kutoa nafasi kwa 'wake wapya' kuolewa."
Anazidi kufahamisha akisema, "Desturi hii hufahamika kama 'kusafisha ghala' kunakotafsiriwa kwa maana ya kutoa mke wa zamani kuingiza mke mpya ndani ya nyumba."
Sauti ya Siti inamnukuu mkazi mmoja wa Newala alipoulizwa kuwa desturi hii imetoka wapi na kwa nini inaendelea ambaye anasema, "Hii sasa hivi imekuwa desturi yetu, wakati tunasafisha ghala kwa ajili ya mazao mapya, pia tunasafisha nyumba kwa ajili ya mke mpya."
'Nimelikuta hili wakati ninakua na watu bado wanaendelea kufanya hivyo."
Ugonjwa au kasumba hii chafu ni kichocheo cha umaskini miongoni nwa familia katika Wilaya ya Newala na huwapa mateso na manyanyaso ya kiuchumi, kiakili na kijamii wanawake na watoto na hivyo, kukwamisha juhudi za nchi katika kukuza maendeleo na ustawi wa nchi.
Ukiachia mbali ukatili huo wanaofanyiwa wanawake wilayani Newala na maeneo mengine nchini dhidi ya umiliki wa rasilimali nchini kwa wanawake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Valerie Msoka anasema haki ya wanawake kumiliki mali haijatajwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata katika Rasimu ya Katiba mpya.
"Haki ya wanawake kumiliki mali haikutajwa kabisa katika Ibara ya 36 ya Rasimu na haikutajwa kwenye Ibara ya 46 hususan suala la ardhi, madini na maliasili,' anasema Msoka.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali TAMWA na kituo chake cha usuluhishi (CRC) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania Bara (TAWLA), Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) inatekeleza mpango wa kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto (GEWEII) katika wilaya 10 za Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkurugenzi huyo anasema kuwa Katiba Mpya ifute sheria kandamizi kwa wanawake, hivyo mashirika haya yanapendekeza kuwa mchakato wa Katiba mpya utokane na ushiriki wa wanaume na wanawake na iweke bayana makubaliano ya misingi mikuu itakayoongoza nchi.
Kwa mujibu wa mazungumzo baina ya Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TAMWA, kinachohitajika pamoja na mambo mengine muhimu, ni kuwapo kwa Katiba mpya iliyojengwa kwa misingi ya usawa, utu na kwamba katiba hiyo iwe imara kutoruhusu kuwapo au kupenyezwa kwa aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia.
TAMWA kupitia kwa Mkurugenzi huyo inasema, "Katiba hiyo itambue kuwa mwanamke na mwanamume wote ni binadamu walio na haki sawa hivyo, ihamasishe ukuaji wa mwanamke na mwanamume katika uchumi, siasa, utamaduni na jamii itambue kwamba imetokana na mwafaka wa kitaifa uliopata ridhaa ya wanawake na wanaume wenye haki sawa."
Katiba mpya iwajibishe Serikali kuhakikisha raia wote, wanapata haki sawa zinazolindwa.
Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania katika chapisho lake liitwalo, Masuala muhimu ya wanawake ya kuzingatia Katiba mpya unasema, "Sheria za nchi zitambue mikataba hii ili kuepusha ucheleweshaji wa kutafsiri au kuruhusu tafsiri zenye kukinzana na misingi ya mikataba husika.
'Kwa kuzingatia kwamba rasilimali za nchi ni mali ya kila Mtanzania (mume au mke), na ili kuleta ukombozi kwa wanawake na jamii nzima, Katiba Mpya iweke bayana kwamba wanawake wa Kitanzania wana haki sawa za kufikia, kutumia, kumiliki na kufaidika na rasilimali za nchi yetu ikiwa ni pamoja na ardhi, madini na vitu vyote vilivyoko nchi kavu na majini."
Mratibu wa Mradi wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji kwa Wanawake (GEWE), Bi. Salome Assey aliwahi kuhojiwa katika jarida moja na kusema kuwa, baadhi ya sheria zinazodhoofisha kampeni dhidi ya ukatili wa kijinsia akiitaja mojawapo kuwa ni Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 anayosisitiza kuwa ni kandamizi.
TAMWA iungwe mkono ili inapolilia usawa wa kijinsia, basi kilio hicho kisikike ili Katiba Mpya ijayo iweke misingi itakayozuia kuhodhiwa kwa madaraka katika mihimili mikuu ya utawala kwa jinsi moja.
TAMWA na wanaharakati wengine wa haki na usawa wa kijinsia wasikike sauti zao ili taasisi za kiuongozi zikiwamo za urais, makamu wa rais, waziri mkuu, mwanasheria mkuu, halmashauri na wilaya, vyama vya kisiasa, bodi za mashirika ya umma na uongozi mpaka ngazi za chini kabisa, zitazamwe upya na kuweka wazi kwa usawa kwa wanawake na wanaume katika katiba ijayo.
Ili kulinda haki na usawa wa kijinsia, iundwe Tume ya Haki za Wanawake itakayokuwa chombo maalumu kitakachoiwajibisha serikali na taasisi mbalimbali nchini kutekeleza haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.
"Katiba mpya iwajibishe serikali kuchukua hatua za kisera na kisheria ili kulinda wanawake wenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili, na kufikia huduma za msingi za kukimu maisha kama vile huduma za afya, elimu, hifadhi ya jamii na fursa sawa katika ajira huku ikitambua kwamba kundi hili huathirika maradufu na mfumo dume," inasema TAMWA katika moja ya machapisho yake.
Katiba Mpya iweke msingi wa kubatilisha sheria, mila na taratibu zinazokinzana na misingi ya haki za wanawake kama itakavyoainishwa katika Katiba Mpya zikiongozwa na haki zilizoainishwa katika mikataba ya kimataifa ya kikanda ambayo Tanzania imeridhia.
Kwa mantiki hiyo Msoka anasema, "Ni muhimu wajibu wa Serikali katika kulinda haki za wanawake na watoto wa kike zibainishwe kikatiba, ikiwa ni pamoja na kuunda chombo mahususi cha kusimamia utekelezaji wa haki hizi."
Sauti ya TAMWA kulilia Katiba Mpya iwajibishe Serikali kutekeleza mikataba yote ya kimataifa iliyoiridhia kuhusu haki za wanawake, iungwe mkono.
"Rasimu ya Katiba Mpya nayo haijakataza ndoa za utotoni, ama kukataza ubaguzi wa umri wa ndoa kwa watoto wa kike; jamii inataka Katiba Mpya ijayo ilete misingi ya usawa ukiwamo usawa wa kijinsia na kuwapo kwa utawala bora."
Anasema, "Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inahalalisha ndoa kwa msichana wa miaka 14 kwa idhini ya wazazi au walezi na miaka 15 kwa idhini ya mahakama. Sheria hii inakinzana na Sheria nyingine ikiwamo Sheria ya Makosa ya Kujamiiana na Sheria ya Mtoto."
"Sheria zote zenye ubaguzi wa kijinsia lazima zibatilishwe katika katiba mpya ijayo na pia, utu wa mwanamke ulindwe.'
Msoka anasema hilo litawezekana endapo watoto wa kike watawekewa mazingira rafiki katika shule na uhakika wa kuwa salama sambamba na haki za wazee kulindwa dhidi ya ukatili.
Anasema "Utu wa mwanamke lazima ulindwe na Katiba Mpya iendeleze misingi ya kumlinda mwanamke dhidi ya ukatili ukiwamo ubakaji ndani na nje ya ndoa, unyanyasaji wa kisaikolojia, ukeketaji wa watoto wa kike na ndoa za utotoni pamoja na vitendo vingine vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike," anasema Msoka.
Akizungumzia Sura ya Nne ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2013 kuhusu Haki za Binadamu, Wajibu wa Raia na Mamlaka ya Nchi, Ibara za 22 hadi 47, Msoka anasema, "Hii ni sehemu ya msingi katika kuweka misingi ya Uongozi uliojikita katika misingi ya utawala bora, utawala wa sheria, uwajibikaji kwa kuzingatia mlengo wa jinsia."
Msoka anaongeza, "Ibara 22 hadi 37 zimebainisha haki zote za msingi za binadamu na Ibara ya 38 hadi 47 haki za makundi zikiwamo haki za mtuhumiwa na mfungwa, haki za watu walioko chini ya ulinzi, haki za mtoto, haki na wajibu wa vijana, haki za wenye ulemavu, haki za makundi madogo madogo katika jamii, haki za wanawake na haki za wazee."
Mkurugenzi huyo kwa niaba ya TAMWA anasema, "Ulinzi dhidi ya ukeketaji watoto wa kike na ukatili dhidi ya vikongwe kwa imani za ushirikina, pia haukutajwa."
Akizungumzia utata uliopo katika haki ya upatikanaji wa huduma bora za afya Msoka anasema, "Ni kama kebehi, kwani itatolewa tu, ikipatikana, nani atakayeamua huduma hizi ni za kipaumbele na zipatikane vipi; ni kitendawili?...
Uwajibikaji na usimamizi wa haki hizi hauko wazi."
Kuhusu haki ya uzazi salama, anasema, "Katiba mpya ihakikishe kuwa afya ya uzazi na uzazi salama kwa kila mwanamke inalindwa kikatiba. Serikali iwajibishwe kuwekeza katika afya ya uzazi ili kumpunguzia mwanamke mzigo mkubwa anaoubeba katika kuendeleza kizazi cha Tanzania."
"Ikumbukwe kwamba, katika kutimiza jukumu la uzazi katika jamii, wanawake hukumbana na changamoto nyingi zinazotishia haki yao ya msingi ya kuishi."

No comments:

Post a Comment