Na Anne Kiruku, EANA
Mkutano wa siku tatu unaojumuisha wataalamu wa vyuo vikuu vya umma
vya Afrika Mashariki na watendaji wakuu wa sekta binafsi, unatarajiwa kujikita
zaidi kuhusu uhaba wa wataalamu na mahitaji ya soko la ajira.
Mkutano huo wa Jukwaa la Wasomi na Sekta
Binafsi na Maonesho ya mwaka 2013 utakaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Jomo Kenyatta Kenya, utawajumuisha wadau kutoka nchi tano
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi hizo ni pamoja na Kenya, Uganda,
Tanzania, Rwanda na Burundi.
Mkutano huo
uliochini ya kauli mbiu, "Kuunganisha wasomi na sekta binafsi kupitia
sekta ya umma,'' unawaleta pamoja wataalamu wasomi waliobobea katika nyanja
mbalimbali na wafanyabiashara waandamizi, watajadili masuala yanayogusa pande
zote za washiriki wa mkutano huo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), Andrew Luzze
aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kwamba sekta binafsi
vyuo vikuu watajadiliana kwa pamoja mkakati wa kushughulikia suala la ukosefu
wa ajira na kukosekana kwa ujuzi unaotakiwa kwa wahitimu wa vyuo vikuu katika
Kanda hiyo ya Afrika Mashariki.
"Wanafunzi wanasema hakuna kazi.Sekta
binafsi inasema wana kazi, lakini ujuzi unaohitajika na sekta binafsi si ule
ambao wahitimu husika wanao,'' alisema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,
Katibu Mtendaji wa Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki, Prof. Mayunga
Mkunya amekubaliana na maoni hayo.
Tatizo hilo
alisema, lipo katika nchi zote tano wanachama wa EAC.''Tunataka kujadili namna
ya kufanya marekebisho ya mitaala ya kufundishia ambao utawezesha kuzalisha
wahitimu wenye ujuzi na mwelekeo.''
Luzze alisema washiriki wapatao
250 wameshathibitisha kuhudhuria. Kutakuwepo na watakaofanya maonyesho 77
kutoka vyuo vikuu na sekta binafsi.
No comments:
Post a Comment