Na Fatuma Rashid
Klabu ya Yanga imepigwa faini ya sh. milioni 5, baada ya baadhi ya
viongozi wake kuzuia kituo cha Azam Televisheni kuonesha mechi ya Ligi Kuu ya
Vodacom dhidi ya Mtibwa Sugar..
Mechi hiyo ilichezwa Oktoba 10 Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam kati ya timu hiyo na Mtibwa Sugar na pia TFF
imetishia kuishusha daraja Yanga kama itarudia tena kosa hilo.
Hii ni mara ya pili katika msimu huu kupigwa
faini katika michezo ya Ligi Kuu baada ya awali kutozwa faini ya sh. milioni
moja kutokana na mashabiki wake kufanya vurugu katika mechi dhidi ya Coastal
Union, iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam na timu zote kutoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Angetile Osiah alisema kwa mujibu wa kanuni 32(9) inasema kuwa klabu yoyote
itakayozuia chombo chochote cha habari, ambacho kimepewa mamlaka na TFF
kuonesha mpira basi faini yake ni sh. milioni 5.
Angetile alisema kama
klabu hiyo itarudia tena kosa, basi adhabu itakayotolewa na TFF ni kushushwa
daraja kwa timu hiyo.
Alisema endapo kama
atatokea kiongozi yeyote, atakayezuia mdhamini ambaye pia amepata haki kutoka
TFF, kwa mujibu wa kanuni ya 36 kiongozi huyo atafungiwa kutojihusisha na mpira
kwa muda wa miaka saba.
Angetile
aliongeza kuwa klabu yoyote haina haki ya kuzuia chombo cha habari kurusha
matangazo ya mechi kwani Ligi Kuu ni mali ya TFF
No comments:
Post a Comment