Na Grace
Ndossa
Hali ya ulinzi na usalama nchini, imeendelea kudorora kutokana na
ongezeko la matukio ya uhalifu yanayoendelea kufanywa na baadhi ya watu. Mtafiti
Mwandamizi wa Taasisi ya Kupunguza Umaskini nchini (REPOA), Dkt. Abel Kinyondo,
aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akiwasilisha taarifa ya utafiti
uliofanywa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Afrobarometa, kuhusu matukio ya
uhalifu nchini.
Alisema
utafiti huo umefanyika kwa miaka tisa 2003-2012, ambapo matukio ya uhalifu
yamekuwa yakiongezeka kila siku kuanzia mwaka 2008-2012 pamoja na ukosefu wa
vituo vya polisi katika baadhi ya maeneo. Aliongeza kuwa, utafiti huo umebaini
kuwa wananchi wengi hawaripoti matukio ya uhalifu polisi kutokana urasimu
mkubwa uliopo, hivyo wananchi hawasilikizwi pamoja na polisi kudai rushwa.
"Utafiti huu
ulikuwa ukiangalia ongezeko la vitendo vya uhalifu nchini tangu mwaka
2008-2012, miaka ya nyuma matukio ya uhalifu yalikuwa machache sana,"
alisema Dkt. Kinyondo.Alisema utafiti huo kwa Tanzania umefanyika Mei na Juni
2012 na ulikusanya maoni ya watu 2,400 kila Mkoa.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA, Profesa Samwel Wangwe, alisema utafiti huu
umefanywa na nchi 34 ambapo kwa Tanzania
inaongoza kuwa na hofu ya uhalifu asilimia 40."Nchi inayofuata kwa kuwa na
hofu ya vitendo vya uhalifu ni Afrika Kusini (asilimia 38), Cameroon (37), Liberia
(35), na Swaziland
asilimia 34," alisema.
Aliongeza kuwa, utafiti uliofanyika mwaka
2011-2012 ni asilimia 42 tu ya watu walioripoti matukio ya uhalifu polisi
nchini Tanzania ambapo idadi
hiyo ni ndogo ukilinganisha na nchi ya Nigeria ambayo nusu ya wananchi
wake wanaripoti taarifa mbalimbali polisi.Prof. Wangwe alisema Jeshi la Polisi
nchini linapaswa kushirikiana na wananchi ili kuwafichua wahusika wa vitendo
hivyo ili waweze kukamatwa.
Aliitaka Serikali ishirikiane na sekta
binafsi ili kujenga vituo vya polisi na kununua vitendeakazi.
Ofisa Mnadhimu wa
Jeshi la Polisi, Beatus Silla, alikubaliana na utafiti huo juu ya upungufu wa
vituo vya polisi na kusisitiza kuwa, suala la ulinzi na usalama ni la watu
wote, si polisi pekee kwani jeshi hilo
halina polisi wa kutosha.
"Kutokana na
uhaba wa vituo vya polisi, tumelazimika kuweka Inspekta wa Polisi kila tarafa
na wamepewa pikipiki za kufanyia kazi ili kupunguza vitendo vya uhalifu,"
alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi na Utawala,
Profesa Amon Chaligha, alisema wananchi wanapaswa kushirikiana na vyombo vya
ulinzi ili kuimarisha utawala bora.
Alisema utafiti huo
pia unaonesha wanawake wanaogopa zaidi kuliko wanaume kutokana na jeshi hilo kutumia mabomu
katika mikutano mbalimbali hivyo kuwafanya waogope.
No comments:
Post a Comment