24 October 2013

BAN KI-MOON AIMWAGIA SIFA APRM AFRIKA



 Na Hassan Abbas
  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Ban-Ki Moon amesema Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) ni nguzo muhimu ya kukuza utawala bora barani humo.

  Amewapongeza viongozi wa nchi za Afrika kwa kubuni na kutekeleza mpango huo ambao ulianzishwa kutokana na mawazo ya Mpango Mpya wa Ushirikiano Kuleta Maendeleo Afrika (NEPAD), kuhakikisha Bara la Afrika linakuwa na utawala bora ili kuharakisha maendeleo.
  Bw. Ki-Moon alitoa pongezi hizi wiki hii jijini New York, nchini Marekani baada ya kukutana na viongozi waandamizi wa APRM na NEPAD ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 68 ya UN, Wiki ya Afrika na NEPAD.
  Akizungumzia kuhusu APRM, Bw. Ki-Moon alisema kwa miaka 10 ya mwanzo tangu mpango huo uanzishwe, Bara la Afrika limeweza kupiga hatua kwani mchakato huo unahimiza utawala bora, kuheshimu katiba na kupanua demokrasia.
  "APRM imeweza kuweka utamaduni wa kisiasa wa kuheshimu utawala bora miongoni mwa Serikali za Afrika. Mchakato huu umeweza kuweka hadharani kanuni za kidemokrasia za kufuatwa na kuhimiza mijadala ili kukabiliana na migogoro," alisema.
  Tanzania ni miongoni mwa nchi 33 kati ya 54 za Umoja wa Afrika (AU) zilizojiunga na APRM na tayari imekamilisha ripoti yake ya kujitathmini inayoonesha hali ya utawala bora nchini.
  Alitumia fursa hiyo kuzipongeza nchi 17 zilizokamilisha ripoti zao za kujitathmini ambapo Tanzania na Zambia zilitathminiwa Januari mwaka huu hivyo kufikisha idadi ya nchi 17 kati ya 33.
 "Nazipongeza nchi 17 zilizohitimisha tathmini ya mwanzo. Mchakato huu umeweza kuimarisha uwajibikaji ndani ya nchi husika, katika baadhi ya maeneo APRM imeweza kuainisha viashiria vya migogoro na kutoa mapendekezo juu ya namna ya kuitatua," aliongeza.
  Kutokana na thamani ya mchakato wa APRM, Bw. Ki- Moon licha ya kutaka mpango huo uimarishwe zaidi, alizitaka nchi wahisani na jumuiya ya kimataifa kuendelea kuupa msaada ili uweze kufanikiwa katika malengo yake.
 "Miaka 10 iliyopita, APRM ilianzishwa ikiwa ni mchakato wa kijasiri ulioionesha dunia kuwa Afrika iko tayari kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto mbalimbali inazokutana nazo katika ujenzi wa demokrasia.
 "Miaka kumi sasa, mpango huu umethibitisha thamani yake, katika kuadhimisha hili naziomba jumuiya za kimataifa kuzisaidia NEPAD na APRM ziweze kufikia hatua ambapo viongozi wa Afrika watakuwa wakizidi kuwajibika kwa watu wao," alisema.
  APRM ilianzishwa Machi 9, 2003 ikiwa na lengo la kufanya tathmini za mara kwa mara za utawala bora miongoni mwa nchi wanachama kwa lengo la kubaini changamoto za kufanyiwa kazi na mambo mazuri ya kuimarishwa au kuigwa na nchi nyingine.
  Tanzania ilijiunga na mpango huu mwaka 2004, Bunge likaridhia APRM kuanza kazi nchini mwaka 2005. Januari mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete aliiwasilisha na kuitetea Ripoti ya Tanzania mbele ya Wakuu wenzake wa nchi na Serikali za APRM, Mjini Addis Ababa, Ethiopia.

No comments:

Post a Comment