Na Goodluck Hongo
Watu wawili wamenusurika kufa baada ya ndege
ndogo aina ya Cessna 204, 5H-IBB, kuanguka jana asubuhi katika eneo la Kambi ya
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) Gongolamboto, Dar es Salaam.
Ndege hiyo
ilipata hitilafu kwenye injini ikiwa angani na watu wawili ambao ni rubani wa
ndege hiyo, Aziz Salim (59), mkazi wa Upanga aliyekuwa akimfundisha rubani
mwanafunzi anayeitwa Ahmed Mahmud (24), raia wa Kenya, mkazi wa Kariakoo.
Akizungumza na
Majira Dar es Salaam
jana, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, ACP Hamisi Selemani, alisema watu
hao walijeruhiwa baada ya ndege hiyo kuanguka.
"Rubani
wa ndege hii (Salim), ambayo inamilikiwa na Kampuni ya As Salaam, alitoa
taarifa kuhusu hitilafu ya injini akiwa angani na kusema muda wowote ndege
inaweza kuanguka hivyo aliamua kuishusha eneo ambalo halina makazi ya watu na
kuharibika vibaya," alisema Kamanda Selemani.
Aliongeza
kuwa, ndege hiyo iling'oka tairi la mbele, kuharibika mabawa yake pamoja na
kubondeka ambapo majeruhi hao walipata majeraha maeneo ya usoni na maeneo
mengine ya miili yao.
Alisema majeruhi hao walikimbizwa Hospitali ya Jeshi Gongolamboto na baadaye
kuruhusiwa.
No comments:
Post a Comment