Na Darlin Said
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ,
kimesema badala ya Serikali kuifuta Sheria ya magazeti ya 1976, wameifanyia
marekebisho baadhi ya vifungu vyake kwa kuongeza adhabu kupitia Mswada wa
Marekebisho ya Sheria ya mwaka 2013, unaotarajiwa kujadiliwa katika kikao cha
Bunge kijacho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Bw. John Mnyika,
alisema kuongeza vifungu hivyo ni sawa na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari kutoa
maoni, haki ya kupata habari.
Alisema kupitia sheria hiyo kifungu cha 36
kinachohusu adhabu kwa magazeti yanayodaiwa kuandika habari za uchochezi,
Serikali imeongeza adhabu hadi kufikia sh. milioni 5 tofauti na faini ya sasa
ya sh. 150,000."Kifungu cha 37 kinasema adhabu kwa
magazeti yanayodaiwa kuandika habari za uongo, adhabu yake imekuwa sh. milioni
5, badala ya sh. 50,000," alisema Bw. Mnyika.
Aliongeza kuwa, pamoja na Serikali kuongeza
adhabu hizo pia imeshindwa kusikiliza vilio vya wadau wa habari kwa kuitaka
kukiondoa kifungu cha 25 kinachohusu adhabu ya kuvifungia vyombo vya habari.
Kutokana na marekebisho hayo, amewataka wadau
wa habari kuupitia mswada huo na kuutafakari kwa makini. Wakati huo huo, Bw. Mnyika alisema katika Kanuni
za Adhabu (Panel Code), Serikali imeongeza kifungu kinachohusu masuala ya
uchochezi na hotuba za chuki na kudai kifungo hicho kinalenga mambo ya dini,
siasa na mengineyo.
"Ndani ya kifungu hiki, neno chuki
limetafsiriwa kwa maana mbalimbali ikiwemo dhamira, kama mtu atatofautiana na
dhamira husika itachukuliwa kama chuki,"
alisema Bw. Mnyika. Alisema kutokana na tafsiri hiyo, itabana mihadhara ya
siasa, dini na vyombo vya habari ambavyo wataenda tofauti na dhamira iliyopo.
No comments:
Post a Comment