Dkt. Makongoro Mahanga
Na Heri Shaaban
Baraza la Madiwani Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, limelaani
vikali migogoro ya kisiasa isiyo na tija kwa wananchi hasa barua iliyoandikwa
na Mbunge wa Segerea, Dkt. Makongoro Mahanga ambayo ilishikiwa bango na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia.
Barua hiyo
inadaiwa kusababisha aliyekuwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Bw. Gabriel Fuime,
kusimamishwa kazi bila kufuatwa taratibu za utumishi hivyo kutia doa utumishi
wake wa muda mrefu.
Meya wa
manispaa hiyo, Bw. Jerry Silaa, aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika kikao
cha Baraza la Madiwani na kusisitiza kuwa, Dkt. Mahanga ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira, hakujali msaada wa Bw. Fuime ambaye aliutoa jimboni
kwake Katika Uchaguzi Mkuu 2010.
Inadaiwa kuwa,
kuna barua ya siri iliyoandikwa kwenda TAMISEMI ikimtuhumu Bw. Fuime na Bw.
Silaa wakidaiwa kuhusika na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.
Kutokana na
tuhuma hizo, Bw. Fuime alisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yake
ambapo miongoni mwa tuhuma hizo ni kushindwa kusimamia mapato ya halmashauri
hiyo na ukodishaji unaotia shaka katika Soko la Samaki Feri.
Hata hivyo, Bw. Fuime anadaiwa kukanusha
madai ya kusimamishwa kazi bali aliamriwa na TAMISEMI apumzike kwa madai ofisi
hiyo imepokea tuhuma dhidi yake.
Katika hatua nyingine, Bw. Silaa alisema
manispaa hiyo inatumia sh. milioni 10 ambazo ni gharama za simu kwa mwezi
ambazo kwa mwaka ni sh. milioni 12. Gharama nyingine ni safari za ndani na nje
sh. milioni 50 kwa mwezi (kwa mwaka milioni 600).
Wakati huo huo, madiwani wa manispaa hiyo
wamemchagua Bw. Kheri Kessy kuendelea na wadhifa wake wa Naibu Meya wa Manispaa
hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.
Bw. Silaa aliwapongeza
madiwani kwa uamuzi huo na kudai kuwa, Bw. Kessy ni kiongozi shupavu ambaye
amempa msaada mkubwa na kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati za Kudumu
waliochaguliwa na kuwataka waongoze kamati hizo kwa moyo na uadilifu.
No comments:
Post a Comment