Na Mwandishi Wetu
Zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kufanyika kwa
Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), mgombea wa nafasi
ya urais, Jamal Malinzi leo anatarajiwa kukutana na waandishi wa habari
kuzindua rasmi kampeni zake, huku akitoa mpango endelevu wa kuendeleza soka
nchini ndani ya kipindi chake.
Akizungumza na mwandishi wa
habari hizi Dar es Salaam
jana, Malinzi alisema ameamua kuzindua rasmi kampeni zake ili Watanzania wajue
kile ambacho anakusudia kukifanya, iwapo atachaguliwa kuongoza chombo hicho.
"Kwangu ni muhimu
zaidi Watanzania wajue sera zangu na wafahamu nini nitafanya iwapo nitashika
madaraka ya kuiongoza TFF.
"Unaweza ukawa shahidi
jinsi ambavyo Watanzania wengi wanavyopenda soka, lakini imetokea bahati mbaya
soka haiwapendi wao. Kuna mahali tunatakiwa kurekebisha, hicho ndicho kitu
ninachotaka kuweka hadharani.
"Huu si wakati wa
kupiga kelele, lazima tuangalie tulipokosea na tuchukue hatua za haraka
kurekebisha, sitaki kuweka kila kitu hadharani, ni vyema kesho (leo) tuisubiri
na utajua kila kitu kuhusu mimi.
"Naamini
nitaeleweka kwa Watanzania na wapiga kura ndani ya TFF, kesho (leo) si mbali
ila ni kusubiri na kujua kile ambacho nitakitoa kwenu," alisema.
Malinzi, mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa
kiti hicho kutokana na uwezo wake mkubwa wa uongozi ndani ya vyama na klabu za
michezo hapa nchini, alisema pamoja na yote hayo anaamini hakutakuwa na mchezo
mchafu katika uchaguzi huo.
"Tuache
mtu anayetakiwa ndiye aongoze chombo hicho, kwangu ninachotaka ni haki na
kutokuwepo kwa mchezo wowote mchafu," alisema.
Uchaguzi
Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika Jumapili ijayo, ambapo unasubiriwa kwa hamu
kubwa na mashabiki wa soka hapa nchini kujua nani atatwaa kiti hicho kutoka kwa
Leodegar Tenga.
Malinzi
alifanikiwa kupita katika kuwania nafasi hiyo, baada ya zengwe kubwa kuibuka
kwake huku awali jina lake liking'olewa kabla ya Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA), kutaka uchaguzi uahirishwe ili kusikiliza malalamiko ya
wagombea mbalimbali.
Mwongozo wa
FIFA ndiyo uliosaidia kwa kiasi kikubwa kwa Malinzi kurejea kugombea nafasi ya
urais ndani ya TFF.
No comments:
Post a Comment