Na
Mwandishi Wetu
Mgombea Urais katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Jamal Malinzi amesema endapo atachaguliwa katika nafasi hiyo, anaahidi
kuenzi mafanikio ya awamu inayomaliza muda wake.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Malinzi
alisema moja ya mafanikio hayo ni kustawisha utulivu katika uendeshaji wa mpira
na kufanya jitihada za kubuni, kuboresha na kustawisha maendeleo ya mpira wa
miguu nchini.
“Jitihada kubwa zitawekwa kwenye muundo wa
idara ya ufundi, katiba ya TFF imeainisha kuwa shirikisho hilo
ndiyo msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, hivyo jukumu la kuleta
maendeleo ya mchezo huu kwa kiasi kikubwa linaiangukia TFF.
“Kwa msingi huu, basi asilimia kubwa ya
rasilimali za TFF lazima ziwekewe katika kuleta maendeleo ya mpira. Kwa mfumo
wetu wa uendeshaji, kichocheo kikuu cha maendeleo ya mpira ni idara ya ufundi
TFF,” alisema Malinzi.
Alisema pia msisitizo uwepo kwenye ujenzi wa
kituo cha mpira (Football Centre of Excellency), ni kituo maalumu cha mafunzo
ya mpira wa miguu, ambapo katika kituo hicho kuna kila aina ya miundombinu,
viwanja vya kufundishia mpira, vituo vya tiba, madarasa, maabara za utafiti,
hosteli na vinginevyo.
Malinzi alisema kuhusiana na suala la timu
kupanda daraja, ili kuongeza ushindani na kupanua mpira uchezwe kona zote
nchini, mtindo wa kucheza kikanda ili kupata timu za kupanda daraja kuu utakuwa
ni wa kudumu na utaimarishwa kwa kutafutiwa udhamini na kuboreshwa viwanja kwa
kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo.
“Kuanzisha mashindano mapya na kufufua ya
zamani, wataalamu wa kandanda wanasema kuwa ili mchezaji awe katika kiwango
bora inabidi acheze kwa mwaka kimashindano wastani wa mechi 40. Ligi yetu kuu
inatoa fursa kwa mchezaji kucheza michezo 26 kwa mwaka iwapo atapangwa kila
mechi hiyo haitoshi,” alisema.
Kwa upande wa mpira wa wanawake, Malinzi
alisema hadi sasa hakuna mfumo imara na unaoeleweka wa kuendeleza soka la
akinamama, ambapo alisema soka hilo la wanawake
lilianzia Wilaya ya Kinondoni na kukulia huko ambapo kuna timu zenye majina kama Mburahati Queens na Sayari Queens.
Pia alisema maandalizi ya vijana ni lazima
mpango endelevu wa maendeleo ya soka la vijana uandaliwe mapema, uratibiwe na
kusimamiwa kwa makini.“Ndugu zangu nasisitiza kuwa maendeleo ya mpira Tanzania kwa
hapa yalipofikia yanahitaji ubunifu, ujasiri na msukumo mpya ili tuweze
kuunyanyua mpira wetu na kuupa mwelekeo mpya, mwelekeo wa matumaini, mwelekeo
wa kulipeleka soka letu katika kushinda vikombe vikubwa barani mwetu Afrika na
duniani,” alisema.
No comments:
Post a Comment