Na
Reuben Kagaruki, Arusha
Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi na
Ajira , Dkt .Makongoro Mahanga, amesema kazi ya kuoanisha kanuni za kukokotoa
mafao ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini imefikia pazuri na
uamuzi wa mwisho unasubiriwa kutoka ngazi ya juu serikalini.
Mahanga alitoa kauli hiyo
juzi mjini hapa wakati akitolea ufafanuzi hoja mbalimbali zilizotolewa na
baadhi ya washiriki wa mkutano wa 23 wa mwaka wa wanachama wa Mfuko wa Pensheni
wa PPF na Wadau Wengine wa Hifadhi ya Jamii mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka, kumaliza
kuwasilisha mada yake.
Mmoja wa washiriki wa
mkutano huo na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe, alitaka kujua kama SSRA
itaweza kuja na kikokotoo kipya cha mafao wakati wanaonufaika na kikokotoo cha
sasa ni watendaji wa Serikali ambao ndiyo watoa maamuzi.
“Kikokotoo kibovu
wanaonufaika nacho ni wale wale watoa maamuzi waliopo Serikali, sasa hapa dada
yangu Irene (Isaka) unadhani utafanikiwa kwa hili? Alihoji Filikunjombe.
Akijibu swali hilo kabla ya Naibu
Waziri Mahanga, Isaka alisema hoja ya mbunge huyo ni moja ya changamoto, lakini
kazi ya kuoanisha kanuni za kikokotoo cha mafao yote ya mifuko yote ya hifadhi
ya jamii imekamilika na kuwasilishwa Wizara ya Kazi na Ajira.
“Tayari tumekutana na
wadau ATE (Chama cha Waajiri) TUCTA (Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania) na
Wizara ya Ajira, hatua tuliyofikia ipo ngazi ya juu serikalini,” alisema Isaka
na kukiri kuna watu wanaathirika na ukokotoaji wa zamani.
Alisema, wanapoelekea
vikokotoo vya mafao wa wanachama wa mifuko ya hifadhi vitafanana ili viendane
na kiwango cha michango yao.
“Kwa hiyo ninachoweza kusema hapa ni kwamba suala la vikokoto limefika ngazi ya
Serikali na Wizara ya imesema suala hilo
limefika ngazi ya juu,” alisema Isaka.
Akikazia jibu la Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Waziri Mahanga alisema; “Suala
la vikokotoo SSRA wamemaliza kazi yao
na wametuletea sisi wizarani na tumemaliza kazi hiyo, sasa lipo kwenye vikao
vya juu vya Serikali, kwa hiyo uamuzi utatolewa wakati wowote ingawa mimi sio
ninayehitisha vikao vya Baraza la Mawaziri. Tuwe na matumaini hayo siwezi
kusema jambo hili litakwama,” Alisisitiza Mahanga.
Kuhusu tatizo la mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa chini ya wizara
tofauti, Dkt. Mahanga alisema katika nchi nyingi duniani mifuko ya hifadhi ya
jamii ipo chini ya wizara moja tena ya ajira.
“Hata sisi hapa kwetu tunaona
hili ni jambo zuri, lakini ukiangalia historia iliyoanzisha mifuko hii hauwezi
kusema mifuko iwe ndani ya wizara moja,” alisema.
Alisema, suala hilo
halina haraka litafanyiwa kazi kama ilivyo
maboresho mengine.
“Tunapoelekea
ni pazuri tutafikia wakati fulani mifuko yote itakuwa chini ya wizara moja,”
alisema Dkt. Mahanga.
No comments:
Post a Comment