- YANGA HUKU SIMBA KULE
Na Neema Ndugulile
Ligi Kuu ya
Vodacom, inatarajia kutimua vumbi tena leo katika viwanja vitatu tofauti,
ambapo Yanga itaikaribisha Rhino Rangers katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itaingia
uwanjani hapo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bila kutarajiwa dhidi ya
watani wao wa jadi, Simba katika mechi iliyopigwa Jumapili kwenye uwanja huo na
kulazimishwa sare ya mabao 3-3.
Katika mechi
hiyo Yanga, ilijiamini kuifunga Simba baada ya kuwa inaongoza mabao 3-0 hadi
mapumziko, lakini kipindi cha pili kibao kiligeuka na mabao yote kurudishwa.
Hivyo katika mechi ya leo, Yanga ambayo ipo nafasi ya nne katika msimamo
wa ligi hiyo, itataka kutoka na ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya
kutetea ubingwa wake.
Wakati Yanga wakiwa Uwanja wa Taifa, watani wao Simba watakuwa wageni wa
Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani
jijini Tanga.
Mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi, Dominic Namisanya kutokana Dodoma, inatarajiwa kuwa
na ushindani mkali kutokana na historia ya timu hizo.
Simba itaingia uwanjani ikiwa ya tatu katika msimamo wa ligi kwa kuwa na
pointi 19, huku Coastal Union wapo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 11.
Nayo Tanzania
Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya Ashanti United
na Simba, itarejea kwenye uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa kuikaribisha
Kagera Sugar.
Katika hatua nyingine, mechi ya Ligi Daraja
la Kwanza (FDL) inaendelea leo kwa mechi moja ya kundi A, itakayozikutanisha
Tessema na Villa Squad katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment