03 October 2013

KIDATO CHA PILI KUANZA MTIHANI OKTOBA 7



Na Mariam Mziwanda
   Mtihani wa Taifa wa kidato cha pili mwaka 2013, utafanyika nchini kote Oktoba 7 hadi 21 mwaka huu, ambapo idadi ya shule na vituo vilivyosajiliwa ni 4,437 sawa na ongezeko la vituo 140 ukilinganisha na vituo 4,297 vilivyosajiliwa mwaka 2012

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
  Alisema watahiniwa 531,457 wameandikishwa kufanya mtihani huo kati yao wasichana 270,744, wavulana 260,723 ambao wote wanajumuisha makundi mawili yenye mahitaji maalumu.Makundi hayo ni watahiniwa wenye uoni hafifu ambao ni 89, wasioona 93 ambapo karatasi za watahiniwa wenye mahitaji maalumu zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji yao.
   “Mtihani huu una umuhimu mkubwa ili kupima kiwango cha maarifa na ujuzi wa mwanafunzi kutokana na mafunzo aliyoyapata kidato cha kwanza na cha pili, pia ni sehemu ya tathmini endelevu katika masomo ya elimu ya sekondari nchini,” alisema.
   Alisema mtihani huo pia utaiwezesha Wizara na wadau wa elimu kuona umahiri wa wanafunzi katika masomo na kutoa changamoto zinazosaidia wanafunzi, walimu, Wizara na wadau kutambua kasoro zilizopo kwenye mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji ili ziboreshwe.
  Aliwataka wanafunzi kuongeza juhudi za kusoma na kujifunza ambapo walimu, wazazi na walezi wakitakiwa kusimamia ipasavyo jukumu la mafanikio ya elimu bora kwa kila mwanafunzi.
  “Jukumu la kusimamia elimu bora ni la kila mtu, pia ni muhimu wanafunzi wote waliojiandikisha kuzingatia utulivu wafanyapo mtihani huu...wale ambao watafanya vibaya watapewa nafasi nyingine na wakishindwa tena, watapelekwa katika mfumo wa nje ya darasa ili kujiendeleza,” alisema.
   Akizungumzia changamoto za shule za kata, alisema idadi kubwa ya wanafunzi wenye matokeo mabaya ni tatizo hivyo Serikali inajipanga ili kuziba pengo la walimu ambalo ndiyo chanzo cha matokeo hayo na kuitaka jamii kuongeza ushirikiano kwa wenye uwezo wa kusomea fani hiyo na kukubali kuajiriwa katika shule hizo.

No comments:

Post a Comment