THE HAGUE, Uholanzi
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC),
imetoa kibali cha kukamatwa raia Mkenya, Bw. Walter Osapiri Barasa ambaye
anatuhumiwa kujaribu kuwahonga mashahidi ili wajiondoe katika kesi inayomkabili
Makamu wa Rais nchini Kenya,
Bw. William Ruto.
Viongozi
wa mashtaka katika mahakama hiyo, walisema mtuhumiwa huyo ameshtakiwa kwa
makosa matatu likiwemo la kutumia njia za ufisadi kumshawishi shahidi mmoja na
mkewe kwa kumlipa sh. milioni 1.4 za Kenya au dola za Marekani 16,200, ili
wajiondoe kama mashahidi.
Kiongozi wa mashtaka, Fatou Bensouda,
alisema ana ushahidi wa kutosha unaoonesha njama za Bw. Barasa kutaka kuwahonga
mashahidi ili wajiondoe katika kesi dhidi ya Bw. Ruto.
Bensouda alisema, kuna mtandao wa watu
wanaofanya kila wawezalo ili kuporomosha kesi hilo ambapo Bw. Barasa aliliambia Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC), kuwa yupo tayari kujitetea mbele ya mahakama
hiyo kwani hana hatia.
Bw. Ruto na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya,
wameshtakiwa kwa kupanga na kuongoza ghasia baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2007 ambapo watu 1,200 walifariki dunia.
Wakati huohuo , ICC imelazimika kuwa na vikao
virefu zaidi vya kusikiliza kesi dhidi ya Bw. Ruto kwa sababu ya muda uliopotea
kutokana na mshtakiwa huyo kurejea Kenya kwa dharura.
Jaji anayeongoza kesi hiyo, Chile Eboe-Osuji,
alisema mahakama itaangalia uwezekano wa kusikiliza kesi wiki ijayo siku ambayo
wangepumzika ili kuruhusu kesi nyingine kusikilizwa.
“Kama
tunavyojua, sote tumepoteza muda katika kesi hii kwa sababu ya matukio ambayo
hayakuweza kuepukika,” alisema. Kesi dhidi ya Bw. Ruto iliahirishwa Septemba
23, mwaka huu, kutokana na shambulizi la kigaidi katika jengo la kibiashara la
Westgate, Mjini Nairobi, nchini Kenya
Septemba 21, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60. Hata hivyo
Jaji Eboe-Osuji alisisitiza kuwa, kesi hiyo itaahirishwa kwa muda ili kutoa
nafasi ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya Rais Kenyatta, Novemba 12, mwaka huu
ambaye ni mshtakiwa mwenza na Bw. Ruto.
No comments:
Post a Comment