Na Rehema Mohamed
Washtakiwa
watatu wakiwemo mke na mume, waliohukumiwa vifungo vya kati ya mwaka mmoja na
nusu hadi miaka saba gerezani, baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya wizi
kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), wamewasilisha taarifa ya kusudio la
kukata rufaa kupinga adhabu hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao ni Bahati Mahenge, ambaye
alipewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka saba jela, Manase Mwakale,
aliyepewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano na mkewe Eddah Mwakale, aliyepewa
adhabu ya kutumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu baada ya Mahakama hiyo
kuwakuta na hatia katika makosa saba kati ya tisa yaliyokuwa yakiwakabili.
Washtakiwa hao wanaotetewa na wakili Deogratian Lyimo, walitiwa hatiani
Septemba 27, mwaka huu na Jopo la Mahakimu wakazi watatu ambao ni Sekela Moshi,
Lameck Mlacha na Sam Rumanyika waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana juzi mahakamani hapo, washtakiwa
hao waliwasilisha taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa kupinga adhabu hiyo
na kuomba wapewe mwenendo wa kesi na nakala ya hukumu.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa na Hakimu Mkazi Lameck Mlacha kwa niaba ya
jopo la mahakimu hao, washtakiwa Mahenge na Mwakale waliamriwa kurejesha sh.
bilioni 1.1.
Hakimu mwingine katika kesi hiyo ni Sam Rumanyika. Akisoma hukumu hiyo,
Hakimu Mlacha alisema washtakiwa wote watano kwa pamoja wanakabiliwa na makosa
tisa.
Makosa hayo ni ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa la wizi wa fedha
kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kughushi nyaraka za usajili wa Kampuni ya
Changanyikeni Residential Complex kuonyesha imetiwa saini na Mwenyekiti wake
Samson Mapunda ambaye ni jina la kufikirika, kutoa hati ya kiapo ya uongo,
kupata usajili wa kampuni kwa makosa ikiwemo kughushi nyaraka mbalimbali za
benki.
Pia, kughushi hati ya makubaliano ya
kuhamisha fedha kati ya Changanyikeni na kampuni ya Maruben Corporation ya
Japan, kutoa nyaraka isiyo sahihi BoT, wizi wa sh. bilioni 1.2 na kujipatia
ingizo la fedha.
No comments:
Post a Comment