“Ukistaajabu ya
Musa utayaona na Firauni” ni maneno ambayo yamekuwa yakitumiwa na watu
mbalimbali hapa nchini, yenye lengo la kuikumbusha jamii fulani juu ya yale
yanayotokea kwa wakati huo.
Maneno haya,
nimelazimika kuyakumbuka katika makala haya kutokana na tukio lililotokea
wilayani Geita wiki iliyopita, ambapo gari la kubeba wagonjwa lilikamatwa
likiwa linatumika kubeba mafuta ya wizi katika mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM).
Kamanda wa
Polisi Mkoani Geita, Leonard Paulo, anazungumzia tukio hilo kuwa lilitokea
Septemba 5, mwaka huu saa saba usiku likiwa na lita 630 za mafuta zenye thamani
ya sh.mil 1.3.
Analitaja kuwa
ni lenye namba za usajili T.671 AKW aina ya Land Cruiser ambalo ni la kituo cha
afya cha Nzera katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Anasema
lilikuwa likiendeshwa na Bw.Amud Bihemo (28) ambapo lilikuwa limefunikwa
maandishi yanayotoa utambulisho wake kuwa ni gari la wagonjwa kituo cha afya
Nzera na mengineyo kama vile alama ya msalaba
mwekundu ili lisitambulike kwa urahisi.
“Limekamatwa na
polisi kwa kushirikiana na walinzi wa mgodi huo, likiwa mgodini katika eneo la
kufua umeme wa mgodi lijulikanalo kama Geita power, huku maandishi
yanayolitambulisha kama gari la wagonjwa Nzera yakiwa yamefunikwa kwa karatasi
za mng’ao na ile sehemu ya kubebea mizigo nayo ikiwa imeng’olewa pamoja na kimulimuli
chake ambapo pia waliweka kitambaa cha kuakisi mwanga ili lifanane na yale ya
mgodi huo,” anasema Kamanda Paulo.
Anawataja
watuhumiwa wengine ambao walikamatwa eneo la tukio kuwa ni Bw.Malemo Paul (38),
Bw.Seleman Magoso (31), Bw.Julias Boas (28), Bw.Rashid Hussein (27) na Ismail
Zuberi(26) wote walinzi wa kampuni ya ulinzi ya G4S.
Wengine ni
Bw.Christopher Kombo(26), mfanyakazi wa mgodi huo na Joseph Christopher na
kwamba watuhumiwa wengine walifanikiwa kutoroka.
Kwa hakika
tukio hili, linawagusa watu wengi si wilayani humo pekee bali hata katika mikoa
mingine hasa kwa wananchi waishio maeneo ya vijijini, ambao wamekuwa
wakitaabika kutokana na huduma duni za usafiri pindi wanapokabiliwa na matatizo
ya kiafya.
Gari hili la
kubeba wagonjwa ni msaada uliotolewa na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) mwezi
Desemba mwaka jana, likiwa na thamani ya sh.mil. 40 ili kusaidia kuondoa kero
ya wananchi wanaopata huduma ya matibabu katika kituo cha afya cha Nzera.
Kituo hiki cha
afya ambacho kiko umbali wa zaidi ya kilomita 40 kufika ulipo mgodi huu,
kinategemewa na idadi kubwa ya wananchi wanaoishi katika tarafa ya Bugando
yenye kata sita ambazo ni Nzera, Senga, Nkome, Muharamba, Fulwe pamoja na
Ruenzela.
Kwa mjibu wa
sera ya afya, kituo hiki kimelenga kutoa huduma kwa wananchi wapatao 34,812
ambao ni kutoka kata ya Nzera pekee na ndio walistahili kuhudumiwa na gari hili
lakini kutokana na upungufu wa magari ya wagonjwa limekuwa likitoa huduma na
maeneo mengine ndani ya tarafa hii.
Baadhi ya
familia zinazoishi katika maisha duni, zimekuwa zikilazimika kutumia usafiri wa
baiskeli na nyingine kutumia mikokoteni inayokokotwa kwa punda ili kuwawezesha
wagonjwa wao kuzifikia huduma za afya kama
vile zahanati, vituo vya afya ama hospitali za wilaya na zile za rufaa.
Usafiri wa aina hii mara nyingi umekuwa ukisababisha vifo vya mara kwa
mara hasa kwa akina mama wajawazito wanapopatwa matatizo wakati wa kujifungua
pamoja na watoto ambao wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo kubwa la ugonjwa wa
malaria.
Tukio
hili la gari la wagonjwa kutumika katika shughuli za wizi kinyume na matarajio
ya serikali na wananchi kwa ujumla, maoni tofauti yametolewa huku mambo mapya
yakijitokeza.
Wananchi wa Nzera ndio hasa walioguswa na tukio hili kwa kile
wanachokiona kuwa hali ya afya zao iko shakani kutokana na hujuma kama hizi za matumizi yasiyo sahihi ya magari ya kubeba
wagonjwa.
“Taarifa hizi binafsi zilinihuzunisha
mno, tumekuwa katika mateso makubwa kabla ya kuletwa katika kituo hiki,
lilikuwa msaada kwetu kwani kuna familia nyingine hazina fedha kwa ajili ya
kukodi gari kutoka hapa Nzera hadi hospitali ya wilaya ya Geita, hivyo lilikuwa
linatusaidia kwa kweli hasa sisi kina mama,” anaeleza kwa masikitiko Bi.
Verediana Nestory mkazi wa Nzera katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya
aliyetembelea kijijini hapo.
“Tunapata shida lisipokuwepo hili gari la wagonjwa, watu wengi
watapoteza maisha kwa sababu tu ya kushindwa kupata huduma mapema kutokana na
kutokuwa na fedha, mfano huko nyuma kabla halijaletwa hapa kuna jirani yangu
niliwahi kumshuhudia akiweka dhamana ya mbuzi ili apate gari ya kukodi toka kwa
mtu binafsi ili mgonjwa wake apelekwe hospitali ya Wilaya ya Geita,” anaongeza.
Anasema, jirani yake huyo aliyeweka dhamana ya mbuzi hakuwa na fedha kwa
ajili ya kulipa usafiri wa gari ili kumuokoa binti yake aliyekuwa na tatizo la
kujifungua, ambapo mumewe alimtelekeza na kukimbilia kusikojulikana.
Mwanamke mwingine ambaye hakutaka kutaja jina lake
gazetini, mfanyabiashara ya duka
jirani na ulipo mgahawa aliokuwa akipendelea dereva wa gari hilo
la wagonjwa kijijini hapo, anasema wao wanachotaka gari hilo lirejeshwe katika kituo hicho cha afya.
“Kama ni wizi amefanya dereva kwa tamaa zake sawa lakini
tunachotaka sisi wananchi wa Nzera, gari letu la wagonjwa waturudishie tu,
kwani lilikuwa likisaidia watu wengi katika maeneo haya ya tarafa nzima ya
Bugando, haiwezekani kosa afanye dereva halafu wananchi tuadhibiwe kwa kukosa
huduma,” anasema.
Baadhi ya wananchi walisema kuwa licha ya kuwa gari hilo
lilitakiwa kutoa huduma hiyo bure, lakini baadhi yao
walikuwa wakitozwa fedha kati ya sh.10,000 hadi 30,000 kama gharama ya
kuchangia mafuta, fedha ambazo zinasadikika zilikuwa zikichukuliwa na dereva wa
gari hilo.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya Nzera, Dkt. Bahati
Nyamachaguri ni kuwa kabla ya tukio hilo la kukamatwa kwa gari hilo la
wagonjwa, kuna mgonjwa aliyemtaja kwa jina la Domicia Kabale (56) alikuwa
amelazwa kituoni hapo na alipatwa na tatizo la kupooza mdomo ambapo alilazimika
kupelekwa hospitali ya wilaya ya Geita kwa matibabu na uchunguzi zaidi.
“Tulilazimika kulitumia gari hili la wagonjwa mimi ndiye niliongoza
msafara na ndani ya gari tulikuwemo watu wanne akiwemo mgonjwa na ndugu yake,
kwa kuwa kesho yake nilitakiwa kuchukua dawa za kupunguza ugonjwa wa virusi vya
Ukimwi(VVU).”
“Tulifika salama saa 11 hivi jioni ya siku hiyo, mgonjwa akapokelewa na
wenzetu wa hospitali ya wilaya na kwa mujibu wa sheria niliamini gari hilo litabaki hapo
hospitali hadi kesho yake,” anaongeza.
Anasema, kesho yake asubuhi wakati anafika hospitalini hapo akijiandaa
kwenda kuchukua dawa hizo lili arudi kituoni kwake kwa kulitumia gari hilo, alishangaa baadhi ya madereva waliokuwa
wamekusanyika wote wakiwa wameelekeza macho yao kwake na baadaye aliambiwa kuwa gari la
kituo chake cha Nzera liko kituo cha polisi baada ya kukamatwa likifanya
uhalifu mgodini.
“Nilienda kituoni pamoja na mkurugenzi, tulikuta kweli gari liko hapo
polisi, likiwa limezibwa maandishi kwa stika, sehemu ya juu ya kubebea mizigo
imeng’olewa na imewekwa kitambaa cha mng’ao kama
yale ya mgodini, nilibaki kushangaa.” anasema.
Mganga huyo Mfawidhi, anasema gari hilo
huwa linawekewa mafuta kila siku ya Jumatatu kutoka ofisi ya Halmashauri ya
wilaya na kuwa tukio hilo
alilosema kuwa siyo zuri limemuumiza yeye binafsi.
“Kwa
kweli limenipatia fundisho kubwa wananchi walikuwa wamelizoea kutokana na kuwa
msaada wao mkubwa ingawa wapo baadhi ya viongozi wa kisiasa walikuwa wakitoa
vitisho kwa dereva pindi anapogoma kufanya yale wanayotaka ikiwemo kubeba
wagonjwa wao pasipo kupitia ngazi zinazohusika za uongozi. Hii inatokana na
baadhi ya watu kutojua utaratibu.
Mwandishi wa makala haya akiwa kituoni hapo, alishuhudia mume na mke
waliokuwa na mtoto wao aliyekuwa na tatizo la kuishiwa damu kwa mjibu wa
daktari, wakibaki kuangua kilio kutokana na kushindwa gharama ya nauli ya
sh.4,000 ili kumfikisha mtoto huyo hospitali ya wilaya ya Geita kwa matibabu.
Majira iliweza kubaini kuwa katika kituo hicho, hapakuwepo na kitabu cha
makabidhiano kwa ajili ya kusaini pindi gari hilo
linapoingia ama kutoka ambapo dereva wake pia hakuwa mtumishi wa kudumu wa
Halmashauri hiyo bali alikuwa akifanya kazi kama
kibarua (cassual) aliyekuwa akisaini mkataba kila baada ya miezi mitatu.
Mmoja wa dereva basi dogo la abiria maarufu kama Hiace linalofanya
safari zake kutoka mjini Geita kwenda Nkome kupitia kijijini hapo, ambaye
hakutaka kutaja jina lake kwa usalama wake, anasema mara nyingi gari hilo la
wagonjwa amekuwa akilikuta limeegeshwa porini jirani na eneo la mgodi wakati wa
usiku.
“Hawa bwana watakuwa wamedhulumiana wao kwa wao tu ni mara nyingi
pengine limekuwa likitumika kwa shughuli kama
hizi hasa usiku, nimekuwa nikikutana nalo limeegeshwa hapa porini usiku, siku
zimefika mwisho, dogo amechezea kazi ningelikuwa na ndugu yangu huko wizarani
ningelimpigia nipate hiyo nafasi,” anasema.
Naye mlinzi mmoja wa kampuni ya Intensive Security inayotoa huduma ya
ulinzi katika hospitali ya wilaya ya Geita(jina limehifadhiwa), anasema siku ya
tukio dereva huyo aliwaeleza kuwa yuko zamu ya usiku, hivyo gari lake litakuwa
na mizunguko ya mara kwa mara kutoka nje na kuingia lango kuu la hospitali hiyo
ya wilaya.
“Unajua bwana yaani unaweza kudanganya sana lakini kama siku imefika
imefika tu, siku hiyo alikuja hapa getini na kutueleza yuko zamu na kama
kawaida tuna vitabu huwa tunaweka kumbukumbu yaani siku hiyo alianza kutoka saa
2 usiku na kuingia mara nyingi kweli hadi tukachoka kufungua geti tukalazimika
kuliacha wazi na mara ya mwisho alitoka saa 7 usiku,”anasema mlinzi huyo wa
Kampuni ya Intensive Security na kuwa kuruhusiwa kwa gari hilo kunatokana na
magari ya wagonjwa wakati mwingine kutumika kuwapeleka madaktari nyumbani kwao
pindi wanapomaliza kazi za kuhudumia wagonjwa.
Mkuu wa Mkoa na wilaya nao wanena
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Magalula Said Magalula, katika mazungumzo na
waandishi habari ofisini kwake, amewataka madereva na viongozi wa serikali
kuacha kutumia vibaya mali
ya umma kwa kuwa ni aibu.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bw. Manzie Omary Mangochie, anasema tukio hilo limemshtua mno na
kwamba hakuwa na mawazo kuwa kuna siku ataliona gari la wagonjwa likiwa
linatumiwa katika vitendo vya wizi badala ya kufanya kazi yake ya kubeba
wagonjwa.
“Nimesikitika sana,
binafsi nimelazimika kufika kituoni mwenyewe kuona kitendo hiki cha fedheha!
Lazima hatua zichukuliwe kamwe hatutokubali vitendo vya namna hii viendelee
katika wilaya yetu, nimeagiza hatua kali zichukuliwe mara moja,”anasema mkuu
huyo wa wilaya kwa masikitiko makubwa.
Kauli ya uongozi wa Halmashauri
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bw. Ali
Kidwaka, anakiri kuwa ni kweli dereva huyo alikuwa kibarua kwa muda wa mwaka
mmoja sasa.
“Niliunda timu maalumu kufuatilia mara
baada ya tukio hili na ilifahamika dereva hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa
Halmashauri, lakini pia limetupatia fundisho na angalizo kubwa,” anasema.
“Gari
la wagonjwa kutumika katika wizi kama huu bila shaka hata wewe mwandishi hili
wazo sidhani kama ulikuwa nalo kuwa inaweza kuwa, ndivyo hivyo hata mimi lakini
kuanzia sasa tunaanza kufanya ufuatiliaji magari yote ya serikali katika
Halmashauri, tutatoa waraka kama njia ya
kudhibiti na kweli tutafanya hata ziara za kushtukiza,” anaongeza.
Anasema, kwa sasa Halmashauri hiyo yenye vituo vya afya vitano ambavyo
ni Katoro, Chikobe, Kashishi, Bukoli na Nzera inakabiliwa na upungufu mkubwa wa
magari ya kubeba wagonjwa ambayo yaliyopo sasa ni mawili pekee.
Kwa mjibu wa taarifa ya maombi maalumu yaliyopelekwa Wizara ya Fedha kwa
Halmashauri hiyo mwaka 2011, jumla ya sh.mil. 420 zilikuwa zimeombwa kwa lengo
la kununua magari matatu ya kubeba wagonjwa, maombi ambayo hayakukubaliwa.
Maombi hayo yalikuwa yamelenga kurahisisha utoaji wa huduma kwa haraka
ikiwa ni pamoja na kuokoa maisha ya wananchi wilayani humo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw.Elisha
Lupuga anasema “dereva huyu lazima afukuzwe kazi mara moja na kutokana na tukio
hili jana tumefanya kikao na madereva wote wa Halmashauri, tumeonya kuwa endapo
litajirudia hatutawafumbia macho wale wote watakaopatikana wakijihusisha na
vitendo hivi,” anasema.
“Suala la kwamba dereva alikuwa mwajiriwa wa muda si hoja bali hata kama
angelikuwa ameajiriwa angefanya hivyo kama ni
tabia yake, hivyo lazima hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria,” anaongeza
mwenyekiti huyo.
Viongozi wa vyama vya siasa wanazungumziaje tukio hili?
Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani
Geita, Bw.Said Kalidushi anasema kuwa tukio hilo ni sawa na hujuma kwa wagonjwa ambao
ndio wanaolitegemea zaidi.
“Ni hujuma kwa wagonjwa, mfano endapo pangelikuwepo na mgonjwa ambaye
alitakiwa kutolewa kituoni hapo kwenda hospitali ya wilaya ya Geita kwa
matibabu zaidi ina maana angelipoteza maisha kutokana na hujuma kama hizi.”
“Siamini inakuwaje gari la wagonjwa liende mgodini kuiba mafuta badala
ya kuhudumia wagonjwa? CCM imekuwa ikilalamikiwa kwa matukio kama haya, hizi ni
tamaa zake na gari hili lilitolewa na mgodi na hilo hilo ndilo limeenda kuiba
humo ndani yaani hii ni sawa na mbwa anayemng’ata mfugaji wake...” anasema na
kuongeza kitendo hicho kisiwavunje wafadhili bali waendelee kutoa misaada kwa
jamii pale wanapoona inafaa kuwa hivyo.
Msemaji wa Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) mkoani Geita, Ignas Karashani, anasema kuwa serikali
inatakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini endapo kitendo cha gari hilo kwenda kufanya wizi
mgodini kilikuwa na shinikizo toka kwa kiongozi yoyote ili hatua zichukuliwe
mara moja.
“Kazi ya gari hili ni kubeba wagonjwa kwa dharura, huko nani aliamuru
liende? Pale Nzera kuna diwani ambaye ni Musukuma kama diwani naye alipaswa
kufuatilia kwa karibu kwa sababu linahudumia watu wake, lazima naye ahojiwe
huenda alishinikiza kwa maslahi yake,” anasema Diwani wa kata ya Nzera ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Bw.Joseph Musukuma yeye alitupia lawama Mganga
Mfawidhi wa kituo hicho pamoja na dereva kuwa wanastahili kuwajibika.
“Mganga Mkuu na dereva wote wanatakiwa kwenda jela tu hao,” alimaliza
kisha kukata siku kwa kile alichoeleza alikuwa akiendelea na mkutano.
Uongozi wa mgodi
Kaimu Mkurugenzi Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Bw. Jasper
Musadaidzwa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema kuwa mgodi huo
umeshtushwa na tukio hilo
la wizi uliofanywa kwa kutumia gari la kubeba wagonjwa.
Anasema, mgodi huo ulitoa msaada wa gari hilo, kwa lengo la kusaidia kusafirisha
wagonjwa, watoto na akina mama wajawazito kwa kuzingatia moja ya sera ya afya
ya mgodi huo isemayo wananchi lazima wanufaike na uwepo wao.
“Tumeshtushwa na wizi huu ambao umefanywa na watu wachache ambao
wanatumia rasilimali za umma kwa matumizi yao
binafsi badala ya kuokoa maisha ya watu,” anasema mkurugenzi huyo wa GGM.
Kukamatwa kwa gari hilo
la wagonjwa likiiba mafuta mgodini humo, kumeleta hofu kubwa kuwa huenda
pengine yapo baadhi yanatumika katika usafirishaji dawa za kulevya kwa kuwa si
rahisi kukaguliwa na polisi kwa kudhaniwa yamebeba wagonjwa.
Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania
inakabiliwa na uhaba mkubwa wa magari ya kubeba wagonjwa katika vituo na
hospitali mbalimbali, hali ambayo ilisababisha Rais Jakaya Kikwete wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu 2010, kuahidi kusambaza pikipiki za matairi matatu
(bajaji) zipatazo 400,000 nchini.
Katika ahadi hiyo, Rais Kikwete alisema lengo ni kusaidia wagonjwa
hususani wanawake wajawazito kuwahishwa hospitali wakati wa kujifungua.
Kwa mujibu wa sera ya afya ya mwaka 2007, Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali itahakikisha utoaji wa huduma bora za uzazi katika vituo vya
kutolea huduma za afya zinazowavutia wanawake, wanaume na vijana hapa nchini.
.
No comments:
Post a Comment