Rais Jakaya Kikwete,
amemtumia salamu za rambirambi katika kuomboleza kifo cha mtangazaji mkongwe
nchini aliyekuwa Meneja wa Kituo cha Abood Media, Julius Nyaisanga kwa jina
maarufu Uncle J, anaripoti Mwandishi Wetu.
Nyaisanga ambaye aliwahi
kufanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kwa sasa TBC Taifa na Kampuni
ya IPP Media ambako alikuwa Mkurugenzi wa Radio One, alifariki dunia Oktoba 20
mwaka huu, mkoani Morogoro. kwa ugonjwa wa kisukari.
“Nimeshtushwa,
nimesikitishwa na kuhuzunishwa kwa kifo cha mtangazaji maarufu na mkongwe
nchini katika tasnia ya habari hususan upande wa utangazaji.
“Julius Nyaisanga ameacha pengo kubwa katika
tasnia hii, enzi ya uhai wake alikuwa na bidii kubwa ya kazi na mwenye sauti
iliyokuwa na mvuto mkubwa kwa wasikilizaji,” alisema.
Rais Kikwete alitoa pole kwa familia ya
marehemu kwa kuondokewa na kiongozi wa familia na kuwahakikishia wanafamilia,
ndugu na jamaa zake kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo.
Alitoa pole kwa waandishi wa habari na
watangazaji kote nchini kwa kumpoteza mwanataaluma mwenzao ambaye kuondoka
kwake kumesababisha pengo kubwa katika taaluma ya habari na utangazaji nchini.
Wakti huo huo, mwili wa marehemu Nyaisanga leo utaagwa katika Viwanja vya
Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam kuazia saa nne asubuhi na baadaye
kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Tarime, mkoani Mara kwa mazishi.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri
nchini (TEF), ilisema Nyaisanga ni miongoni mwa wanahabari ambao wajumbe wa
jukwaa kila walipofika Morogoro kwa shughuli mbalimbali, walishirikiana naye
ndani na nje ya mikutano.
TEF itamkumbuka daima
jinsi alivyoweka alama yake katika tasnia ya habari ambapo alama hizo
zitaendelea kuwa hai kuenziwa kwa kutekeleza wajibu na maadili ya taaluma.
.
No comments:
Post a Comment