Na
Theonestina Juma, Bukoba
Kampeni ya kitaifa ya
kuwaondoa wahamiaji haramu nchini iliyopewa jina la “Operesheni Kimbunga” awamu
ya pili ambayo inaendelea katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, imewanasa
majambazi watano wanaojishughulisha na biashara ya kuuza silaha zinazotoka nchi
jirani na kuziingiza nchini.
Naibu Kamishna
wa operesheni hiyo, Simon Sirro, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari Mjini Bukoba, mkoani Kagera, kuhusu maendeleo ya operesheni
hiyo.
Alisema hadi
sasa, majambazi 88 wamekamatwa miongoni mwao, watano wanaojihusisha na biashara
ya kwenda nchini Burundi
kununua silaha kwa sh. 300.000 na kuziingiza nchini na
kuziuza kuanzia sh. milioni moja.
“Majambazi
watatu wamebainika kusambaza silaha kwa wateja hapa nchini na majambazi wote ni
Watanzania, jambazi mmoja alikuwa akifanya biashara ya kuuza mbuzi nchini Burundi.
“Baadaye
alipoona biashara hiyo hailipi, aliwashawishi Watanzania wenzake kufanya
biashara ya kuuza silaha ambayo ndiyo inawalipa hivyo kuanza biashara hiyo,”
alisema kamanda Sirro bila kutaja majina ya majambazi hao.
Alisema
operesheni hiyo awamu ya pili, ilianza Septemba 21 hadi Oktoba Mosi mwaka huu
ikiwa na mafanikio makubwa ambapo wahalifu 529 walikamatwa na wahamiaji haramu 425 katika
Mikoa ya Geita, Kigoma na Kagera.
Aliongeza
kuwa, walioruhusiwa kwa uamuzi wa mahakama ni 159, waliorudishwa makwao kwa
hiari 122, walioachiwa huru 39 na wanaoendelea kuhojiwa hadi sasa 105.
Kamanda Sirro
alisema, watu watano wanashikiliwa kwa tuhuma ya kuwatorosha na kuwahifadhi
wahamiaji na majangili 11 ambapo silaha mbalimbali 23 zimekamatwa.Silaha hizo ni
pamoja na bunduki aina ya SMG, bastola, magobole 18, magazine mbili, bomu la
kutupwa kwa mkono pamoja na sare moja ya Jeshi la Burundi.
Katika hatua
nyingine, Kamanda Sirro alisema ng’ombe 2,220 wamekamatwa, 103 wanamilikiwa na
Bw. Kalemela George, wilayani Biharamulo ambaye mahakama imetoa amri ya
kutaifishwa baada ya kuwaingiza katika Hifadhi ya Taifa Biharamulo
kinyume cha sheria.
“Natoa wito
kwa wafanyabiashara wa nyama mjini Bukoba,kwenda kuwanunua kwa ajili ya
kuchinja na kuuza, hatua ya kutaifisha mifugo ni nzuri...kesi nyingine za
mifugo bado tunafanya utaratibu wa kuzifikisha mahakamani,” alisema.
Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali mstaafu Issa
Njiku, alisema operesheni hiyo bado inaendelea pia itakuwa endelevu.
No comments:
Post a Comment