21 October 2013

CHINA KULETA WATALII 10,000 KILA MWAKA



Na Mwandishi Maalumu, SHENZEN, China
    China imeahidi kuleta watalii 30,000 nchini Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwakani.
Ahadi hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Wakala wa kutoa Huduma za Usafiri wa China na Hong Kong (China Travel Services Hong Kong Limited-CTS), Bw. Zhang Xuewu baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, jijini Shenzen, nchini China.
Alisema kampuni yake itawaandaa mawakala wa usafirishaji watalii ili kuhakikisha watalii 10,000 wanapatikana kila mwaka ambao kiu yao ni kuangalia vivutio vya Tanzania."Wengi wanapenda kutembelea mbuga, hapa China wamezoea kuona wanyama walio sakafuni (sanamu katika makumbusho), wakija watawaona wanyama kwenye mbuga," alisema.
Bw. Pinda ambaye yupo nchini humo katika ziara ya kikazi kwa mwaliko wa Serikali ya China, alisema haelewi kwanini kampuni hiyo imeweza kupeleka watalii Afrika Kusini na nchi jirani za Afrika Mashariki wakati haina urafiki nazona kushindwa kuwapeleka Tanzania yenye uhusiano nao mzuri.
Akizungumza mbele ya Bw. Xuewu na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania ambao ameambatana nao, Bw. Pinda alisema amepewa maelekezo na Rais Jakaya Kikwete kufuatilia suala la watalii kutoka China kwani mazungumzo ya jambo hilo yalianza wakati wa Rais Bw. Benjamin Mkapa.
"Katika bara la Afrika, hakuna nchi yenye vivutio lukuki kama Tanzania inayofaa kwa safari za mbugani kama mtu anataka kuona vivutio vizuri na vya asili, kwanini hatupati watalii wa kutosha, tunafanyaje," alihoji Bw. Pinda.
  Alisema njia mojawapo ni kuhakikisha kunakuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka miji ya China hadi Dar es Salaam jambo ambalo litasaidia kupunguza kero kwa wasafiri ambao hivi sasa inabidi waunge safari mara mbili hadi tatu kufika Tanzania.
  "Tuangalie uwezekano wa kuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka China hadi Dar es Salaam au Arusha...wenzetu Kenya na Afrika Kusini wameweza kupata watalii wengi sababu wana ndege za moja kwa moja," alisema.
  Alimshawishi Bw. Xuewu aangalie uwezekano wa kujenga hoteli katika mikoa ya Tanzania ili kupunguza uhaba wa vyumba pale watalii watakapoanza kufurika.Alimhakikishia fursa ya kujenga uwanja wa gofu chini ya Mlima Kilimanjaro kwani yote mawili ni maeneo ambayo kampuni yake ina uwezo wa kuyafanya kama sehemu ya majukumu yake.
  Bw. Pinda alimpa Bw. Xuewu wazo na kusema kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya urafiki wa Tanzania na China, CTS inaweza kuandaa kundi kubwa la wakala wakaenda Mjini Arusha na kufanya mkutano wa siku mbili au tatu.
  Alisema wakiwa Mjini Arusha, watapata fursa ya kujadili namna ambavyo Tanzania na China zinaweza kushirikiana ili kukuza suala zima la utalii na wakimaliza mkutano, wanasaini makubaliano kati yao na Bodi ya Utalii nchini (TTB) ili mambo yasonge," alisema.
  Kwa upande wake, Bw. Xuewu alikiri kuwepo mazungumzo ya wakuu wa nchi akisema; "Mwaka 2004, Rais Hu Jintao alifikia makubaliano na Rais (Mkapa) kwamba watafungua milango ya utalii kwa Tanzania.
"Machi, 2013, Rais Kikwete na Rais wa China, Bw. Xi Jinping, walirudia tena mazungumzo hayo na kukubaliana kuwa Tanzania itapewa kipaumbele cha pekee kwa watalii wa kutoka China.
  "Hata wewe na Waziri Mkuu wetu, Bw. Li Keqiang, juzi mmeshuhudia Mawaziri wakisaini makubaliano juu ya suala hili, Serikali mmedhamiria kuinua viwango vya utalii ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania," alisema.
  Alimshukuru Bw. Pinda kwa wazo lake la kufanya mkutano Mjini Arusha na kumhakikishia kuwa, wako tayari kujenga hoteli, viwanja vya gofu, kuanzisha tawi la kampuni ya uwakala kama walivyoshauriwa

No comments:

Post a Comment