- PADRI ATAKA WAANDISHI WA HABARI WAHESHIMIWE
Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitoa heshima za mwisho
mbele ya jeneza lenye mwili wa aliyekuwa mtangazaji mkongwe na Meneja wa Kituo
cha Abood Media, marehemu Julias Nyaisanga, aliyefariki dunia Oktoba 20 mwaka
huu, mkoani Morogoro, baada ya kusumbuliwa na kisukari. Marehemu Nyaisanga
aliagwa jana katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni Dar es Salaam
Na Rehema Maigala
Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, jana ameongoza mamia ya
wananchi kuaga mwili wa aliyekuwa mtangazaji mkongwe na Meneja wa Kituo cha
Abood Media, marehemu Julias Nyaisanga, aliyefariki dunia Oktoba 20 mwaka huu,
mkoani Morogoro.
Marehemu Nyaisanga aliagwa katika viwanja cha
Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam
na baadaye kusafirishwa kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika Tarime, mkoani
Mara.
Akizungumza katika viwanja hivyo, Dkt. Bilal
alisema marehemu Nyaisanga alikuwa kipenzi cha watu, mtangazaji ambaye ametumia
taaluma yake kuelimisha jamii hivyo ni vyema waandishi wa habari wakafuata
nyayo zake.
Aliongeza kuwa, marehemu alifanya kazi yake
katika mazingira magumu kwani kipindi alichoanza kazi, kulikuwa hakuna vyombo vingi
vya habari kama ilivyo sasa.
Naye Padri Stephano Kaombwe wa Kanisa
Katoliki ambaye ndiye aliyeongoza ibada, alisema tangu enzi za mababu hakuna
mwanahabari duniani anayekumbukwa kwa mazuri ambayo ameyafanya japo wao ndiyo
chumvi katika jamii.
“Bila ya kuwa na wanahabari ni sawa na chakula
kisicho na chumvi, wanahabari wanatusaidia kutuelimisha, kufundisha hata
kuburudisha hivyo tunapaswa kuwaheshimu,” alisema.
Aliongeza wanahabari wanapaswa kuiheshimu
chumvi ambayo wameipata kutoka kwa Mungu ili kuikomboa dunia hii.Marehemu
Nyaisanga aliwahi kufanya kazi Radio Tanzania,
Dar es Salaam
(RTD) kwa sasa TBC Taifa na Kampuni ya IPP Media, akiwa Mkurugenzi wa Radio
One.
Viongozi mbalimbali wa
vyama, Serikali, taasisi, wamiliki wa vyombo vya habari, Jukwaa la Wahariri
waliungana kumuaga marehemu Nyaisanga ambaye ameacha mke na watoto watatu.
Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment