26 August 2013

WAVUVI ,WAFUGAJI ZIWA RUKWA WAPIGANA



Rashid Mkwinda na Esther Macha, Momba
VU R U G U k u b w a iliyosababishwa na kile kinachoelezwa kugombea mpaka kati ya vijiji vya Senga wilayani Momba mkoani Mbeya na Kijiji cha Ilambo kilichopo Kata ya Kapeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa imeibuka na kusababisha nyumba 24 kuchomwa moto.Pia katika vurugu hizo watu sita walijeruhiwa kwa kupigwa fimbo na mapanga.

Taarifa za awali zilidai kuwa, vurugu hizo zilitokea Agosti 21, mwaka huu, majira ya saa 12 jioni katika kambi ya wavuvi iliyopo Kitongoji cha Mchangani ambapo kundi la wafugaji wenye ng'ombe wengi kutoka katika Kijiji cha Ilambo kilichopo wilayani Sumbawanga, kilivamia katika Kijiji cha Wavuvi na kuchungia mifugo yao katika ardhi tengefu la mwambao mwa Ziwa Rukwa.
Kutokana na hali hiyo Kamati ya Ulinzi Ziwa Rukwa (BMU) iliwataka wafugaji hao kuondoa mifugo yao katika eneo hilo, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa eneo hilo halifai kwa uchungaji wa mifugo ya aina yoyote kutokana na kuwa ni eneo tengefu ambalo halipaswi kuingizwa mifugo ndani yake.
Mwenyekiti wa kamati hiyo katika kitongoji cha Mchangani, Aziz Mlapakoro alisema kuwa mara baada ya kundi hilo la wafugaji kuingia katika mwambao wa Ziwa Rukwa, waliwafuata na kuwaomba waondoe mifugo yao na kwamba baada ya kuondoka kesho yake mifugo ikaingia tena ziwani bila wachungaji.
Mlapakoro alisema kuwa, mara baada ya kuona hali hiyo Kamati ya Ulinzi Ziwa Rukwa iliketi ili kujadili uvamizi huo ambapo baadaye walifikia uamuzi wa kuikamata mifugo hiyo na kuwataka wenye mifugo waje kuikomboa kulingana na sheria za usimamizi na uhifadhi wa Ziwa Rukwa.
Alisema kuwa, badala ya kuja kuchukua mifugo yao, kundi la vijana wenye silaha kutoka katika Kijiji cha Ilambo Kata ya Kapeta wilayani Sumbawanga kilivamia katika kijiji cha Senga na kuanza kuwapiga wananchi na kuwajeruhi na kuwachomea makazi yao huku wakiiba mali zilizomo.
Mkuu wa wilaya ya Momba, Abihudi Saideya ambaye alifika kwenye eneo la tukio alishuhudia makazi ya kijiji cha wavuvi yalivyoteketezwa kwa moto na baadhi ya mali kuibiwa na wavamizi kutoka katika kijiji cha Ilambo cha wilaya jirani ya Sumbawanga.
Akizungumza katika eneo la tukio mara baada ya kupewa taarifa na uongozi wa Kijiji cha Wavuvi, Saideya alisema kuwa, jumla ya watu sita wamejeruhiwa kwa kupigwa na vitu vinavyosadikiwa kuwa ni vyenye ncha kali baada ya kuvamiwa na kuchomewa makazi yao.
Alisema kuwa, mara baada ya taarifa hizo serikali ilitoa tahadhari ya kuzuia mapigano ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi kufika eneo la tukio na kuweka ulinzi na kuwazuia wananchi kutolipiza kisasi juu ya uvamizi uliofanywa na wananchi wa kijiji jirani cha Wilaya ya Sumbawanga.
"Tulifanya haraka kuzuia taharuki ya wananchi wa kijiji kilichovamiwa, askari walifika mapema katika eneo la tukio, tulifanikiwa kuwakamata watu saba na wengine tunaendelea kuwasaka," alisema Saideya.Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani aliwataja watu saba waliokamatwa katika tukio hilo kuwa ni Samwel Daud (42), Gervas Lucas (52), Nyerere Mwita(52), Richard Wilson (43), Gebrus Ramadhan (28), Lulinde Dase (43) na Funguza Masanja (43).
Alisema kuwa watuhumiwa hao kutokea katika Kijiji cha Kilambo Kata ya Kapeta wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa walivamia kambi za wavuvi na kuanza kuwapiga wakazi wa maeneo hayo, kwa kutumia fimbo kisha kuchoma makazi ya wavuvi yaliyojengwa kwa kutumia nyasi.
Alisema kuwa, watu sita walijeruhiwa katika tukio hilo ambao ni Msabaha Juma (40), Maximo Mwakanyemba(24), Michael Sanga (30), Chonde Kalisto (56), Zawadi John (39) na Gibson Edward Kachingwe (26).Aidha, Kamanda Diwani aliwataka wananchi kuwafichua wote waliojihusisha na tukio hilo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za matukio mbalimbali ya uhalifu.

No comments:

Post a Comment