Na Martha Fataely,
Hai
BAADHI
ya wanafunzi wa udaktari na uuguzi katika Chuo cha Machame wilayani Hai,
wanashindwa kumaliza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya
Serikali kutotekeleza ahadi yake ya kukipatia ruzuku chuo hicho ili
kujiendesha.
Rais wa
wanafunzi wa chuo hicho, John Ware alisema kutotekelezwa kwa ahadi hiyo
kunawaathiri kwa kiasi kikubwa na kuwafanya baadhi ya wanafunzi kushindwa
kumaliza masomo yao kwa ukosefu wa gharama za kujitegemea.
Waganga 50 na wauguzi
36 waliomaliza mafunzo ya miaka mitatu ya fani hizo wamekumbusha ahadi hiyo
katika risala yao wakati wa mahafali ya 42 ya waganga hao, mahafali ya kwanza
ya wauguzi katika chuo hicho na uzinduzi wa ukumbi wa mikutano na bwalo la
chakula la chuo.
Naye Kaimu Mkurugenzi
wa chuo hicho, Dkt. Elifinya Massawe ameiomba Serikali iongeze idadi ya
watumishi wa hospitali na walimu wa chuo hicho ili ihudumie wananchi na kutoa
wataalamu wengi watakaokidhi mahitaji ya Serikali ya kuwahudumia wananchi
vijijini.
"Hii ada
inayolipwa na wanafunzi ndiyo tunaitumia kwa ajili ya kulipa mishahara na
shughuli nyingine muhimu, miaka mitatu sasa Serikali haijatupatia ruzuku,
kutokana na hilo ada ni kubwa, wanafunzi 2 wa Tanzania na Wakenya watatu
walikatisha masomo yao mwaka jana," alisema.
Akibariki wahitimu
ukumbi na bwalo hilo Askofu Dkt. Martin Shao wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini inayomiliki chuo hicho amewataka waganga
na wauguzi hao kwenda kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa bila kutanguliza
masilahi yao.
"Nyinyi
mnamaliza leo, mnakwenda kulitumikia taifa ni vyema mkatanguliza masilahi ya
taifa kuliko yenu binafsi, kumbukeni viapo vyenu," alisema.
Mapema Naibu Waziri
wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Agrey Mwanri aliwataka
wataalamu wa fani mbalimbali kuacha uchakachuaji wa taaluma zao ili kuepusha
taifa kupata madhara.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu
Waziri Mwanri, Mkuu wa Wilaya ya Moshi Dkt. Ibrahim Msengi alisema kitendo cha
kuchakachua taaluma kutasababisha taifa kupata hasara kwani wataalamu hao
bandia hawana uwezo wa kufanyakazi kwa ufanisi au kuleta mabadiliko.
No comments:
Post a Comment