Na Elizabeth Mayemba
MSHAMBULIAJI mpya wa Simba raia wa
Burundi, Hamis Tambwe ameanza kuonesha cheche zake katika klabu hiyo, baada ya
juzi kuifungia bao pekee walipocheza na Stand United ya Shinyanga katika mechi
ya kirafiki.
Simba walikuwa
Kahama na Shinyanga kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao dhidi ya Rhino Rangers
ya Tabora ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayochezwa mjini Tabora
kesho.Akizungumza kwa
simu wakiwa njiani kwenda Tabora, Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are
'Mzee Kines', alisema waliondoka jana mkoani Shinyanga na walitarajia kufika
jioni ya siku hiyo Tabora kwa ajili ya mechi yao ya kesho.
Alisema wakiwa Shinyanga walicheza
mechi ya kirafiki na Stand United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na
kushinda bao 1-0, lililofungwa na Tambwe.Mzee Kines alisema wachezaji wote wapo
katika hali nzuri hakuna majeruhi hata mmoja, hivyo inampa wakati mzuri Kocha
Mkuu wa timu hiyo, Abdallah 'King' Kibadeni kupanga vizuri kikosi chake.
Akizungumzia uhamisho wa wachezaji wao wa
kimataifa, Tambwe na beki Gilbert Kaze Mzee Kines alisema uongozi
ulishamalizana na klabu ya Vital'0 na wakati wowote kuanzia sasa vibali hivyo
vitatua nchini."Uongozi umeshamalizana na Vital'0
na wakati wowote kuanzia sasa vibali hivyo vitatua nchini na wachezaji hao
wataichezea timu yetu, mashabiki wetu na wanachama wasiwe na wasiwasi na
hilo," alisema Mzee Kines.
Alisema kuna watu wasioitakia mema timu yao na
kuzusha maneno mengi kuhusu wachezaji hao wapya, lakini wao hawatishwi na
wanapambana na kila changamoto iliyo mbele yao.
No comments:
Post a Comment