23 August 2013

MUHIDINI GURUMO ASTAAFU MUZIKI



 Na Amina Athumani
MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini wa bendi ya Msondo Ngoma, Muhidini Gurumo ametangaza kustaafu muziki rasmi kutokana na umri wake kuwa mkubwa.Akizungumza Dar es Salaam jana, Gurumo alisema anastaafu shughuli za muziki huku maisha yake yakiwa duni kwani hana hata baiskeli.

"Muziki ni kama asili yangu, imefikia wakati sasa nasema basi nawaachia vijana waweze kuendeleza muziki wetu," alisema Gurumo.Alisema umri wake kwa sasa umekuwa mkubwa ambapo alisema ameimba kwa kipindi cha miaka 53, akiwa jukwaani.
"Sasa hivi nina umri wa miaka 73, nilizaliwa mwaka 1940 na nilianza kuimba muziki nikiwa na miaka 20 na sasa nastaafu muziki nikiwa na umri huu, lakini bado hali yangu kimaisha ni duni sina hata baiskeli," alisema Gurumo.Alisema tangu aanze kuimba muziki hadi sasa ametoa kopi 60,000, ambazo hazijamfaidisha kimaisha hivyo ameamua kuunda kamati, itakayokuwa inamsaidia katika kipindi hiki alichostaafu muziki.
"Muziki ulikuwa ni maisha yangu sasa nitaishije baada ya hapa, nimeona ni bora kuunda kamati itakayokuwa inanisaidia kwa njia moja ama nyingine," alisema.Kamati hiyo iliyoundwa na Gurumo ina wanamuziki na wakurugenzi wa bendi mbalimbali akiwemo Asha Baraka, Juma Mbizo, Saidi Mdoe, Waziri Ali na Saidi Kibiriki.
Akizungumzia kamati hiyo, Mbizo alisema yeye pamoja na wenzake watabuni njia ya kumsaidia mzee Gurumo kwa kuandaa tamasha moja ambalo mkongwe huyo, atapanda jukwaani kuwaaga Watanzania na fedha zitakazopatikana zitamsaidia mwanamuziki huyo.Mbizo pia amewataka wadau wa muziki kuangalia wazee kama hao, ambao walikuwa katika tasnia ya muziki kwa muda mrefu, lakini wakistaafu wanakuwa hawana maisha ya kuridhisha.

No comments:

Post a Comment