Na Grace
Ndossa
SERIKALI imeshauriwa
kuanzisha juhudi za makusudi zitakazosaidia kukabiliana na uingizwaji wa bidhaa
zisizo na viwango zinazoingizwa nchini ikiwemo saruji.Ushauri huo umetolewa
na kampuni ya kuzalisha saruji ya Tanzania Portland Cement Company (TPCC).
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara
iliyotembelea kiwanda hicho mwishoni mwa wiki Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya
TPCC, Pascal Lesoinne, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Saruji
Afrika Mashariki (EACPA), alisema suala hilo kama halijapatiwa ufumbuzi
litaathiri uhai wa kampuni nyingi nchini na hatimaye kuathiri uchumi kwa
ujumla.
"Kampuni nyingi
za Tanzania za uzalishaji saruji zinakumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa
saruji itokayo nje hasa Pakistan," alisema na kuongeza;"Waingizaji wa
saruji toka nje wanatumia ipasavyo mianya iliyopo katika mfumo wa forodha na
uingiaji wa bidhaa kwa kulipa kati ya asilimia tano hadi 10 tu ya ushuru wa
forodha, hali ambayo inaigharimu nchi hasara ya zaidi ya sh. bilioni 25,"
alisema, Lesoinne.
Aliongeza kuwa
Tanzania haihitaji saruji ya kutoka nje kutokana na uwepo wa kampuni nyingi
zinazozalisha saruji hivyo zinaweza fikia mahitaji ya nchi kikamilifu.
Kwa upande mwingine
alisema kutopatikana kwa umeme wa uhakika kumeongeza gharama za uendeshaji wa
kampuni yake. Alitoa mfano kuwa kampuni yake inatumia zaidi ya dola milioni 2
kwa mwezi ili kuhakikisha umeme mbadala unapatikana pindi umeme wa TANESCO
unapokatika.
"Changamoto
kubwa inayoathiri uzalishaji wetu ni kutokuwepo kwa upatikanaji wa umeme wa
uhakika. Kampuni lazima ihakikishe kuwa wateja wanaendelea kupata bidha zetu
kwa wakati wote bila kikwazo," alisema.
Alisema kuwa kampuni
ambayo kwa sasa inazalisha zaidi ya tani milioni 1.3 za saruji kwa mwaka
itaweza kuzalisha hadi tani milioni 2 kwa mwaka baada ya uzinduzi wa kiwanda
chake kipya Oktoba, mwaka ujao.
Kwa upande wake,
Mbuge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alieleza wasiwasi kuhusiana na jitihada
zinazochukuliwa na mamlaka husika na kuziomba kufanya uchunguzi sahihi kujua
ukweli wa suala hilo.
"Hili ni suala
nyeti sana. Sisi kama kamati hatuwezi kulifumbia macho kwa kuwa lina athari
kwenye maendeleo ya uchumi wa nchi yetu," alisema Kafulila.
Mkurugenzi wa Viwanda
katika Wizara ya Viwanda na Biashara, Eliness Sikazwe, alisema Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, tayari ameteua kamati ya wanachama
saba kuchunguza suala hilo
na kuongeza kuwa kamati hiyo itatoa ripoti baada ya uchunguzi kukamilika.
No comments:
Post a Comment