- WATANZANIA WALISHWA VINYESI, MENGI YAIBUKA
Watoto wakicheza pembezoni mwa Ziwa Victoria.
Picha hii inaonesha mfereji (kulia)
unaotoka Soko Kuu la Mji wa Bukoba ukiwa umebeba vinyesi kutoka maeneo
mbalimbali likiwemo Gereza la Bukoba, Uchafu unaotoka katika gereza hilo hupitia Shule ya Msingi Rumuli kabla ya kuungana na
mfereji huo ambao hukutana na Mto Kanoni, kama
inavyoonekana pichani.
Na Mwandishi Wetu
"
Kwa kweli hakuna moyo wa uzalendo katika suala la kutunza
mazingira ya Ziwa Victoria, kama leo hii ukiwauliza Magereza taka ngumu na
kinyesi wanamwaga wapi, huwezi kupata jibu, wanarukaruka tu,” Magongo-
Mfuatiliaji na Mtathmini Mradi wa KADETFU
SERIKALI imeweka sheria mbalimbali
zinazolenga kutunza mazingira ikiwemo Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka
2004
.Pia mwaka 2009, Serikali ilipitisha Sheria Namba 11 ya
rasilimali za maji na Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira
ambazo kwa pamoja zinalenga kulinda na kutunza nyanzo vya maji.Sheria hizi zinatoa adhabu, mfano katika kifungu cha 52(1) cha Sheria Namba 12 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, kinatoa faini ya kiwango cha shilingi milioni moja au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja kwa mtu yeyote atakayesababisha uchafuzi wa chanzo cha maji.
Hata hivyo, licha ya kuwepo sheria hizo bado kumekuwa na
uchafuzi mkubwa wa mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria unaofanywa na
wananchi, viwanda, mahoteli pamoja na taasisi mbalimbali za serikali na zile
zisizo za Kiserikali.
Jeshi la Magereza mjini Bukoba Mkoa wa Kagera ni miongoni
mwa taasisi za umma ambazo kwa kiasi kikubwa zinadaiwa huwa zinahusika katika
kuchangia kuchafua mazingira ya Ziwa Victoria
kupitia utiririshaji wa vinyesi katika Ziwa Victoria.
Kupitia gereza lililopo Bukoba Mjini, uchunguzi umebainisha
kuwa, gereza hilo limekuwa likitapisha kinyesi
kwenye mtaro unaotoka katika gereza hilo, ambao
unapita nyuma ya mfereji unaokatiza katika Kanisa la Kisabato la Seventh Day
Adventist kuja Barabara ya Uganda
iliyopo Mtaa wa Rumuli.
Kinyesi hicho, huwa kinaingia katika mfereji unaotoka katika
Shule ya Msingi Rumuli kupitia Soko Kuu na kuungana na Mto Kanoni ambao
unapeleka moja kwa moja taka hizo ziwani.
Katika uchunguzi uliofanywa na Majira katika mfereji
unaotoka Shule ya Msingi Rumuli na kuungana na mfereji unaotoka gerezani ni kama mita 200 hadi 300 kuingia ziwani kupitia mto Kanoni
ambapo umebainisha utiririshaji wa vinyesi ovyo.
Uchunguzi huo ulikuwa ni mwendelezo wa kuangalia uchafuzi wa
mazingira Ziwa Victoria
unaofanywa na Jeshi la Magereza kwa kumwaga vinyesi vya wafungwa na ongezeko la
magugu maji ziwani humo.
Ambapo katika makutano ya mfereji wa Rumuli na gereza, eneo hilo la makutano hayo
kumezibwa ili kusiweze kuonekana kwa urahisi wakati wa kutemesha kinyesi hicho.
Gazeti hili liliweza kufanya uchunguzi na kujionea mtaro
ambao uko pembezoni mwa Barabara ya Uganda
unaotokea gerezani karibu na Kanisa hilo,
ambao ulikuwa ukitiririsha na umejaa maji taka ambayo yalikuwa yakitoa harufu
kali, ambayo unaweza kuifananisha na mzoga wa mnyama aliyekufa kwa muda katika
maeneo hayo.
Baada ya kugundua hali hiyo gazeti hili liliweza kufanya mahojiano
na baadhi ya wananchi wakiwemo wadau wa mazingira wa maeneo hayo, ambao nao
walionesha kuguswa na tatizo hilo.
Tatizo ambalo wanasema linafanya hali ya hewa kuwa mbaya
wakati wa masika, ambapo gereza hilo
hutumia mwanya huo kutapisha kinyesi hicho jambo ambalo linaleta usumbufu
mkubwa kwa wakazi hao.
WANANCHI
WANENA
Mmoja wa waumini wanaosali katika Kanisa la Wasabato la
Seventh Day Adventist ambaye alijitambulisha kwa jina la Editha Rweyimamu
anasema, harufu mbaya inayotoka gerezani hapo hasa wakati wa mvua imekuwa
ikisababisha waumini kushindwa kupata usikivu wa neno la Mungu pindi wanapokuwa
kwenye ibada.
“Wakati huu wa kiangazi hali kidogo huwa shwari (nzuri),
lakini maji taka hayo huwa wanatiririsha kidogo sana ila wakati wa mvua unashindwa hata
kutafakari hii harufu ni ya kitu gani, kwa maana harufu huwa ni nzito na
inaenea kanisa zima,” alisema Rweyimamu.
Naye Jumanne Issa ambaye anajihusisha na biashara ya kuuza
vitabu kwenye eneo hilo
kwa miezi nane sasa anasema, amekuwa akishuhudia harufu ya vinyesi kutoka
katika mfereji unaotoka gerezani, huku kila mtu anayepita karibu na mfereji huo
akilazimika kufunga pua.
Wakati mwananchi huyo akisema hivyo, mwandishi wa makala
haya alifanikiwa kupita kila eneo ambalo linazunguka Gereza na kushuhudia maji
taka hayo yakitiririka kutoka mfereji wa Gereza kupitia Barabara ya Uganda, ambayo
yanakutana na mfereji wa Shule ya Msingi Rumuli na kuingia Mto Kanoni, ambao
unapeleka maji moja kwa moja ziwani.
“Harufu
inatuathiri sana,
tunashangaa kuona serikali imelifumbia macho, tunaomba watafute njia ya kumwaga
kinyesi hicho sio kupeleka ziwani mahali ambapo tunapata chakula na maji ya
kunywa,” alisema muuza vitabu huyo.
WADAU
WA MAZINGIRA
Wakizungumzia
suala hilo kwa nyakati tofauti, wadau wa
mazingira katika Manispaa ya Bukoba nao walisema kuwa, gereza hilo limekuwa likitiririsha kinyesi mwaka
mzima mfululizo na kuingiza Mto Kanoni ambao unapeleka maji ziwani.
Michael
Cleophans ambaye ni katibu mkuu wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya
mazingira ya Envirocoment mjini Bukoba anasema, gereza hilo
limekuwa likitiririsha kinyesi kupitia mfumo ambao si rasmi wa kunyonya vyoo
vilivyotitia, yakiwemo maji taka kutoka kwenye vyumba vya wafanyakazi na
kuyatiririsha kwenye mfereji kupitia kanisa hilo la Wasabato.
Anasema,
suala hilo wamekuwa wakilijadili mara kwa mara
katika vikao vyao vya mazingira, lakini limekuwa likichukuliwa sana kisiasa.
“Kutokana
na vitisho vikali kutoka kwao (gereza), watu wamekata tamaa na taasisi zingine
za kiserikali zinazoshughulika na mazingira, walisema watalifuatilia, lakini
hadi leo (mwishoni mwa wiki) zimeendelea kuwa kimya,” anasema mdau huyo.
Aidha,
anasema kuwa pamoja na kwamba hakuna miundombinu ya mfumo wa maji taka katika
Manispaa ya Bukoba isiwe sababu ya wao kukwepa gharama za kulipia magari ya
kunyonya maji taka hayo na kuyapeleka kumwaga katika eneo ambalo limetengwa na
Manispaa kwa ajili hiyo.
Naye
Justus Magongo ambaye ni Mfuatiliaji na Mtathmini Mradi katika Shirika la
Maendeleo Kagera (KADETFU) anasema kuwa, taasisi nyingi katika Manispaa ya
Bukoba ikiwemo Magereza zinahusika katika uchafuzi wa mazingira kutokana na
ukosefu wa miundombinu.
Anasema
kuwa, wao kama taasisi isiyo ya kiserikali
wanafanya kazi pale ambapo serikali haiwezi kufika.
“Tumeweza
kufanya semina kwa viongozi wa taasisi mbalimbali na Magereza wakiwemo, ili
kutoa hamasa katika kupunguza tatizo hili, lakini cha ajabu hakuna utekelezaji
wowote uliofanyika.
“Kwa
kweli hakuna moyo wa uzalendo katika suala la kutunza mazingira ya Ziwa
Victoria, kama leo hii ukiwauliza Magereza taka ngumu na kinyesi wanamwaga wapi
huwezi kupata jibu wanaruka ruka tu,” anasema Magongo.
MRADI
WA LVEMP II
Mratibu
wa Mradi wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili (LVEMPII) Manispaa ya Bukoba, Richard
Salu alikiri kufahamu kuwa kuna mtaro unaotoka Magereza kuingia Mto Kanoni
unaotiririsha uchafu ingawa bado hawajajua ni uchafu wa kiasi gani ambao
unaingizwa ziwani.
“Nafahamu
sana, ila hiki
ni kituo cha serikali, hivyo pindi itakapobainika tutakaa nao meza moja ili
kuwashauri maji taka hayo yaweze kutibiwa kabla hayajaingia ziwani au
waunganishe kwenye mfumo wa maji taka wa manispaa ambao bado haujajengwa,”
anasema Salu.
Hata
hivyo, uchunguzi wa gazeti hili ulibainisha kuwa licha ya kutokuwepo kwa mfumo
wa maji taka katika mji wa Bukoba mkoani Kagera, Manispaa imetenga eneo la
Nyanga nje kidogo ya mji huo kwa ajili ya kumwaga huo uchafu, lakini watu
wamekuwa hawatumii, badala yake wamekuwa wakisubiria mvua ikinyesha waruhusu
kinyesi hicho kiweze kutapishwa.
OFISA
MAZINGIRA BUKOBA
Ofisa
Mazingira katika Manispaa ya Bukoba , Hamza Kambuga alipohojiwa kuhusiana na
suala hilo
alikiri Magereza kutapisha kinyesi, japo kuwa wana makaro ya maji taka ambayo
yanadaiwa huwa yanazidiwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wafungwa.
Anasema
kuwa, wakati gereza linajengwa (mwaka 1937) lilikadiriwa kuwa na wafungwa
wachache ( wafungwa 360) hivyo gereza lilikuwa dogo.
Kwa
kuwa, wakati huo ilikuwa ni ngumu kujenga mfumo wa maji taka mkubwa wa kiasi
hicho kama inavyohitajika hivi sasa, hivyo
tangu wakati huo mfumo wa gereza haujapanuliwa na miundombinu iko vilevile na
wafungwa wakizidi kuongezeka.
Anasema
kuwa, tatizo hilo
wanaliona lakini changamoto yake ni kubwa hali hiyo inaweza kutatuliwa endapo
mfumo wa maji taka utajengwa ambapo wataweza kuunganisha moja kwa moja.
Hata
hivyo, Kamishna Msaidizi wa gereza hilo, ACP Nkonjelwa alipohojiwa na mwandishi
wa makala hii juu ya idadi ya lini gereza hilo lilianzishwa na idadi ya
wafungwa kipindi hicho hadi leo alisema kwa kifupi; “ lilianzishwa mwaka 1937,
likiwa na uwezo wa kuchukua wafungwa 360, kwa sasa hivi wapo 437 ambapo
wafungwa ni 213 na mahabusu 224,” alisema ACP huyo.
MAABARA
BUKOBA
Gazeti
hili liliweza kuonana na Mkuu wa Maabara katika Manispaa ya Bukoba, Marco Vitta
ambaye alithibitisha kuwa, gereza hilo
limekuwa likihusika katika utapishaji wa kinyesi hicho ziwani (kupitia maeneo
ambayo yametajwa hapo juu).
Anasema
kuwa, kwenye kipindi cha mvua maji taka hayo yanakuwa hayaonekani moja kwa moja
kutokana na kinyesi hicho kuchukuliwa na maji moja kwa moja ila wakati wa
kiangazi hali inakuwa ni mbaya zaidi, vinyesi vinakuwa vinatapakaa.
Anasema
kuwa, mwanzoni hali hiyo haikuwa mbaya sana
katika kipindi cha nyuma kutokana na Magereza kutokuwa na wafungwa wengi, lakini
hali imekuja kubadilika hivi karibuni katika miaka ya 2000 hali hii inaonesha
kuwa gerezani kuna msongamano wa wafungwa.
“Huenda
hapo awali katika kipindi cha nyuma, Magereza ilikuwa ikitapisha kwa mwaka mara
moja kutokana na idadi ndogo ya wafungwa waliokuwepo (360), lakini hivi sasa
kutokana na wingi wa wafungwa unakuta ‘septic’ (mfumo wa maji taka) zinajaa
ndani ya miezi mitatu hadi nne hivyo wanachofanya ni kutapisha kinyesi,”
anasema Vitta.
Anaongeza
kuwa, suala hili la gereza kutapisha kinyesi ziwani limekuwa ni gumu kupatiwa
ufumbuzi kutokana na kwamba hiyo ni taasisi ya kiserikali.
“Hivyo
ni jukumu la serikali kulitafutia suluhu japo hili, vipimo vya kimaabara
vinavyofanyika kila mara kwa maabara kuchukua sampuli za majitaka hayo kutoka
Magereza zinaonesha maji taka yanayotiririshwa kutoka kwao ni kinyesi kitupu,”
anasema Mtaalamu huyo.
MKUU
WA MAGEREZA
Gazeti
hili lilimtafuta Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kagera (RPO) ambaye pia ni Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Magereza Mkoa wa Kagera, Yusuph Kimanji (amestaafu tangu
Julai Mosi, mwaka huu) ili aelezee suala hili kwa upana zaidi.
Mkuu
huyo, alidai kuwa Manispaa ya Bukoba imekuwa ikishindwa kuweka mkakati wa muda
mfupi na mrefu wa jinsi gani ya kuwa na mfumo wa maji mjini Bukoba.
“Jambo
hili (kutiririsha vinyesi ziwani) si kweli, wanaisema Magereza kwa sababu
wanaichukia taasisi hii, lakini ukweli ni kwamba maji taka katika majengo yote
Bukoba yanapita katika Mto Kanoni na kuingia ziwani,” anasema Mkuu huyo wa
gereza.
Alipoulizwa
kuhusiana na maji taka yanayotiririka kutoka kwenye gereza hilo, alikana na kusema kuwa wao hawahusiki
na utiririshaji wa maji taka.
“Kama tungefanya hivyo, tusingehusika katika kuombea fedha
suala la kunyonya maji taka toka serikalini.
“Tangu
nimeingia katika ofisi hii mwaka 2007, mwezi Julai niliona kuna matatizo ya
mfumo wa maji taka, katika mji wa Bukoba na ndio maana niliamua kuweka
utaratibu wa kuombea fedha jambo hili,” anasema Kimanji.
Hata
hivyo, alimuonesha mwandishi wa makala hizi nyaraka ambazo zinazoonesha fedha
walizoomba katika kupindi cha mwaka 2010/2011 ambapo walipokea sh. milioni 6.5.
Mwaka
2011/2012 zilikuwa ni sh. milioni 7.1 ambazo zote zilikuwa kwa ajili ya
kunyonya maji taka kutoka katika maeneo ya Magereza na mwaka 2012/2013
walipokea sh. milioni 5.6.
Fedha
ambazo zilikuwa kwa ajili ya kukarabati mfumo wa maji taka ambao bado
wanautekeleza ili kuhakikisha kuwa hakuna maji yanayopotea na kwenda kuzagaa
nje.
Alipoulizwa
kuhusiana na hali aliyoikuta wakati anakabidhiwa gereza hilo, Mkuu huyo alikataa kuzungumza na kudai
kwamba hawezi kuongelea masuala ya nyuma kwani kwa wakati huo hakuwepo na
hawezi kujua kilichokuwa kinaendelea.
“Sitaki
kuongelea suala hilo,
ila anayestahili kubeba lawama ni manispaa, kwa nini haina nfumo wa maji taka
na pia haina magari ya kunyonya maji taka na badala yake tunaenda kukodi magari
ya watu binafsi,” anasema Kimanji.
Katika
kuthibitisha kauli yake kuwa, hawamwagi kinyesi ziwani kupitia Mto Kanoni,
gazeti hili liliamua kuwatafuta madereva waliopewa dhamana na Manispaa ya
Bukoba ya kunyonya maji taka katika mji huo ili waweze kuthibitisha kama huwa wanatumiwa na taasisi hiyo ya Magereza ili
kunyonya maji taka na vinyesi.
Lengo
ni kutaka kujua kama ni kweli Magereza hawahusiki au katika uchafuzi wa ziwa na
pia kuhakikisha kama kweli fedha ambazo wanaletewa na serikali kwa ajili ya
kunyonya maji taka kama zinatumika ipasavyo kama alivyosema.
SAUTI
ZA MADEREVA
Miongoni
mwa madereva ambaye hakutaka kutaja jina lake na
kampuni anayoiwakilisha gazetini kwa kuhofia kupoteza wateja wake alimweleza
mwandishi kuwa, taasisi hiyo ya Magereza huwa inawakodi kunyonya maji taka kwa
mwaka mara moja.
“Ni
kutoka katika makaro ya magereza hiyo,” anasema Dereva huyo.
Anasema
kuwa, mara ya mwisho kukodiwa na magereza ilikuwa ni Oktoba, mwaka jana hadi
leo hii hawajawahi kukodiwa.
Pia
Dereva huyo anasema kuwa, pindi wanapokodiwa huwa wanapewa mkataba wa kubeba
awamu 10 ambapo wao wanachaji kila moja sh. 120,000.
Anasema
kuwa, maji taka hayo huwa wanayanyonya katika makaro matano yaliyopo katika
gereza hilo na pindi wanapokuwa wananyonya huwa wanapunguza punguza kutoka
katika karo moja na huwa hawatoi yote ili kuhakikisha tripu 10 zinatimia na
mengine yanayobaki wakati wa mvua Magereza wenyewe huwa wanatapisha katika
mtaro, kwa kutumia ndoo ambapo kazi hiyo hufanywa na wafungwa.
“Mwaka
huu tangu uanze hatujawahi kukodiwa na Magereza, mara ya mwisho wametukodi
mwaka jana mwezi Oktoba na huwa wanatukodi mara moja kwa mwaka ambapo huwa
wanatupa mkataba wa tripu 10 tu, ambazo huwa tunapunguza punguza kutoka katika
makaro ya gereza hilo,”
anasema Dereva huyo.
Kutokana
na maelezo ya dereva huyo anasema kuwa, kila tripu moja huwa wanatoza sh.
120,000 hivyo kwa tripu 10 ni sawa na shilingi milioni 1.2 ndizo ambazo zinatumika
kutoka katika fedha ambazo Mkuu wa Magereza Bukoba alizitaja.
Kwa
kuwa, wanapatiwa kutoka serikalini kila mwaka jambo ambalo linaonesha kuwa
hazitoshelezi katika kukidhi mahitaji ya unyonyaji taka na yale yanayobaki
kwenye septank yanasubiri kutapishwa wakati wa mvua kama
ilivyothibitishwa na dereva huyo.
WAHUSIKA
NA WALINZI ZIWANI
Mratibu
wa Mradi wa Mazingira wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili (LVEMPII), Omary
Mwamuyanza anasema kuwa ni kweli Magereza huwa wanamwaga kinyesi cha wafungwa
ziwani japo si peke yao
wako wengi.
Anasema
kuwa, wao kama mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Victoria
pamoja na kujua kuwa Magereza na taasisi nyingine zinachafua mazingira hawana
mamlaka ya kuwachukulia hatua bali huwa wanawaeleza manispaa ili watekeleze
suala hilo.
“ S
i s i h a t u n a s h e r i a y a kuwachukulia hatua ila watu kama NEMC (Baraza
la Mazingira nchini) na Manispaa ndizo ambazo zinatakiwa kutusaidia katika
suala zima la kuwachukulia hatua, sisi tunasaidia katika kutekeleza mradi ikiwa
ni pamoja na kujenga mfumo wa maji taka katika mji huo ambao utagharimu zaidi
ya dola milioni1.5, ambao utakamilika ndani ya miezi 18 ijayo,” anasema
Mwamuyanza.
Anasema
kuwa, uchafuzi wa mazingira ya Ziwa Victoria
bado ni changamoto kubwa kwani wananchi pamoja na taasisi nyingi hawako tayari
kubadili tabia za kutiririsha vinyesi ziwani hadi inawalazimu mara kwa mara
kuwaelimisha na mradi unatumia gharama nyingi, lakini hawako tayari kupokea
ushauri.
MSIMAMO
WA NEMC
Gazeti
hili lilimtafuta Mratibu wa Kanda ya Ziwa katika Baraza la Taifa la Usimamizi
wa Mazingira (NEMC), Anna Mdamo ambaye ofisi zake zipo jijini Mwanza ili aweze
kujibu ni kwa nini Gereza la Bukoba limekuwa likichafua ziwa kwa kumwaga
kinyesi cha wafungwa ziwani na sheria za kulinda mazingira zikiwepo.
Mdamo
alisema kuwa, wao kama kanda hawajathibitisha kama
Magereza wanachafua ziwa alisema kuwa, mtu anayetakiwa kuthibitisha kuwa
Magereza wanachafua ziwa kwa kumwaga kinyesi ziwani ni Ofisa Mazingira wa
Manispaa ya Bukoba.
“Sina
taarifa zozote kuhusiana na gereza kutiririsha kinyesi ziwani, hatujafanyia
kazi na wala hatujaletewa malalamiko, ila pindi tutakapoambiwa na kuthibitisha
kuwa wanahusika katika suala zima la uchafuzi wa mazingira tutaenda kuonana nao
na kuwachukulia hatua,” aliongeza.
Uchunguzi
unaonesha kuwa, uchafuzi wa mazingira ndani ya Ziwa Victoria unaofanywa na wananchi zikiwemo
taasisi mbalimbali za serikali hasa Gereza la Bukoba kwa kutirisha kinyesi
ziwani ni tatizo ambalo linaathiri watumiaji wa ziwa pamoja na viumbe hai kwa
ujumla.
Inakadiriwa
kuwa, ziwa hilo linategemewa na wakazi zaidi ya
milioni 35 kutoka nchi za Kenya,
Uganda, Tanzania, Rwanda
na Burundi ambapo ziwa hilo lina ukubwa wa mita za mraba 194,000 huku Tanzania ikimiliki asilimia 44 ya eneo lake lote.
ITAENDELEA
fanya utafiti ndo mtoe hiki mnachokisema.huwezi dai heti mtalo unamwaga unatoka magereza hivyo na kinyesi kiko sambamba na mtaro.utafiti finyu.
ReplyDeletewe anonymous hapo juu mbona unajazba hivyo...tambua kuwa habari yoyote haiandikwai bila kufanyiwa utafiti.
ReplyDeleteSWALA SI MARUMBANO. HAPA HOJA TOA MCHANGO NAMNA YA KUDHIBITI HAYA MAJI TAKA
ReplyDeleteHi, my name is Ashraf, I am from India. I happened to study in Bukoba, Rumuli Shule ya msingi in 1968 in seventh grade.. I am trying to get in touch with my old classmates. If anybody remembers me please wirte to kalnad@gmx.com. I had a friend, his name was Leonidas Mayunge.
ReplyDeleteAfter 45years...I still miss the place. .Bukoba in Tanzania
ReplyDeleteAshraf K