26 August 2013

RIPOTI MAALUM - 2:UBAKAJI WAJANE



Na Reuben Kagaruki
SEHEMU ya kwanza ya makala hii ya Okosomboka, ilieleza kwa kina maana halisi ya mtu anayesombokwa na jinsi usombokaji unavyofanyika kwa wakazi waishio Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza hasa kwa Wakala na Wajita.

Makabila hayo yamekwenda mbali zaidi katika kutekeleza mila na watu maalumu wanaokodishwa kwa ajili ya kusomboka (kubaka).Pia makala hiyo ilielezea mazingira yanapofanyikia kitendo cha kusomboka na sifa za wasombokaji.
OKUSOMBOKA KWA SASA
Hivi sasa, kuna mabadiliko makubwa ya utekelezaji wa mila hiyo tofauti na miaka iliyopita. Hali hiyo inatokana na elimu inayotolewa kwa jamii ili kuutokomeza utamaduni huo.Elimu hiyo imeanza kutolewa baada ya kubainika mila ya kutakasa wajane yaani (Okusomboka) ni ubakaji na udhalilishaji mkubwa dhidi ya wanawake. Sababu nyingine iliyosababisha wahusika wabadili mbinu ya utakasaji ni kuadimika kwa watakasaji.
Watakasaji wa kukodiwa ambao ndio waliopo sasa, wanafanya vitendo hivyo kwa usiri mkubwa na kutoza gharama kubwa hali ambayo imesababisha jamii ya wana Ukerewe hasa Wakala na Wajita, kubuni mbinu nyingine ya utakasaji wajane.Mmoja wa wazee anayefahamu kwa undani mila hiyo Bw.Vedastus Kamalamo (75), mkazi wa Kata ya Nkilizi, anasema alizaliwa mwaka 1938 na kuikuta mila hiyo ya kutakasa wajane kwa kutumia watu maalumu ambao walikodiwa na kulipwa fedha kwa ajili ya kutakasa.
A n a s e m a k a d r i s i k u zinavyokwenda, watakasaji wa kukodiwa wanazidi kupungua hivyo waumini wa mila hiyo nao wamebadili mbinu ili kupata watakasaji kwa urahisi."Baada ya kuongezeka watetezi wa haki za binadamu ambao wamekuwa wakitoa elimu ya kupiga vita mila hii na watakasaji wa kukodiwa kupungua, kuna utakasaji mpya umeanza," anasema.
Anaongeza kuwa, wajane ambao hawapati watakasaji wa kukodi inabidi siku nne baada ya matanga aende mwenyewe maeneo ya starehe kama vile kwenye baa, magulio na kwenye madanguro kuvizia wanaume wa kumtaka kimapenzi aweze kufanya nao tendo la ndoa ili kutimiza sharti la kutakaswa.Kamalamo anasema, lazima afanye hivyo akiwa na wanawake wenzake kama wawili wa kumsindikiza ili washuhudie kama kweli amepata mwanaume wa kumtakasa.
"Ma s h u h u d a h a o n d i y o wanaotakiwa kuthibitisha kufanyika utakasaji kwa mjane waliyemsindikiza," anasema na kuongeza kuwa, wengine wanaenda mbali zaidi na kufunga safari hadi jijini Mwanza au visiwani walipo wavuvi kwa lengo hilo wakiwa na wasindikizaji."Akitokea mwanaume akamtaka kimapenzi, mtakaswaji na wasindikizaji wake wanakuwa tayari kumnunulia hata pombe iwe rahisi kufanikisha lengo la kutakaswa.
"Mwa n a ume a n a p o t a k a waende kufanya tendo la ndoa, wale wenzake (wasindikizaji) wanajifanya wana haraka ya kuondoka, hivyo wanamuhimiza awahi kurudi (kumaliza tendo mapema).An a s ema wa s i n d i k i z a j i wanafanya hivyo kumharakisha mjane ili mwanaume asiweze kurudia tendo hilo zaidi ya mara moja kwani sharti la kutakasa linahitaji mshindo mmoja tu.
"Akimaliza mshindo mmoja, mwanamke huondoka akiwa ameshatengeneza mazingira ya kutokaa na mwanaume huyo muda mrefu ili kuepuka kufanya tendo hilo zaidi ya mara moja na kuharibu maana ya kutakasa," anasema.
Kamalamo anapoulizwa kama tendo la ndoa linapofanyika bila mtakasaji kujua kama anatakasa linakubaliwa kwenye mila yao alisema kuwa; "Hiyo inakubalika kwani tendo la ndoa linafanyika ili kuhitimisha uhusiano ulioanzishwa kati ya marehemu na mjane," anasema.
Anapoulizwa kama tendo la kutakasa mjane halikushuhudiwa na mashuhuda linakubalika alifafanua kuwa, kutakasa lazima kuwe na mashuhuda wa kujiridhisha kuwa kweli tendo hilo limefanyika na kama lifanyika tofauti utakasaji huo haukubaliki.
Anaongeza kuwa, tendo la kutakasa linafanyika ndani ya kipindi cha matanga, hivyo mjane na wasindikizaji wanaondoka kwenda kutafuta mtakasaji na wakishampata wanarejea kwenye msiba na kutoa taarifa kwamba tayari ametakaswa.
BAADA YA KURUDI KUTAKASWA
Mtakaswaji baada ya kurudi nyumbani akiwa ametakaswa, watu wote waliokuwa kwenye matanga pamoja na yeye mwenyewe, wananyolewa vywele na nyasi walikuwa wakilalia wafiwa wakati wa matanga, zinakusanywa na kuchomwa moto ambapo hiyo ni ishara ya kumaliza msiba.
Kwa upande wake, Bw. Fabian Bihemo (66), mkazi wa Kitongoji cha Magereza, Kata ya Nkilizi, anasema baada ya kukamilisha taratibu za kumaliza msiba, wote hutawanyika na kurudi kwao.
Kwa mujibu wa Bihemo, baada ya kurudi nyumbani sharti moja wapo kwa waliokuwa msibani ambao wameoa na kuolewa, wanatakiwa kufanya tendo la ndoa na wenzi wao.
Kwa wale ambao wenzi wao watakuwa wamesafiri, kuna taratibu za mila ambazo wanatakiwa kuzifanya. Taratibu hizo ni muhusika kwenda kujisaidia haja ndogo kwenye kichuguu kisichokuwa na shimo au kwenye mti aina ya Mzungute au njia panda.
Muhusika anapokuwa anajisaidia haja ndogo, anapaswa kutaja jina la mwenzi wake ambapo kwa mujibu wa Bihemo, inapotokea mwanaume mmoja ana wanawake zaidi ya mmoja, anatakiwa afanye tendo la ndoa na mke mkubwa baada ya kurudi kutoka msibani.
Anasema kila mmoja inatakiwa ahakikishe anatimiza mila hiyo ili kuepuka kukiuka masharti.
Mila hiyo pia inathibitishwa na Mchungaji wa Kanisa la Africa Inland Church of Tanzania (AICT), wilayani Ukerewe, Paul Kashezo, ambaye anasema; "Baada ya mtakaswaji kurudi nyumbani na matanga kumalizika, wote wanaohusika na msiba ambao wameoa na kuolewa, lazima waende kulala na waume zao".
UTAKASAJI KWA WANAUME
Akielezea jinsi wanaume wanavyotakaswa, Juma Mtalo (83), mkazi wa Nkiliza, Kitongoji cha Mmakeke, anasema yeye ni miongoni mwa wanaume waliotakaswa baada ya kufiwa na mke wake mwaka 1990.
Anasema utaratibu wa kutakasa wanaume, mwanaume akifiwa na mke wake yanafanyika matanga na siku ya nne, wanafika waganga kwa wafiwa.
Waganga wakifika hutafuta mjane ambaye huenda kuchuma mboga za majani za aina nane, kununua samaki mmoja aina ya sato na kutengenezwa chakula.Unapofika usiku, mfiwa (mwanaume) anakula chakula na watoto ambao hawajaolewa. Pia kinatengenezwa kitanda kwa kutumia miti minne ambayo inachimbiwa chumbani na kuondoa kitanda ambacho mfiwa alikuwa akilala na marehemu mke wake.
Baada ya kumaliza kula, mtakaswaji analala chini na hapo anayeruhusiwa kumsemesha ni mjane ambapo inapofika saa nne usiku, mtakaswaji anaamshwa na kulazwa katika kitanda kilichotengenezwa akitakiwa kulala ubavu na akitaka kugeuka, hapaswi kuangalia juu.Anaongeza kuwa, ikifika saa tisa usiku, mtakaswaji huamshwa na kupewa dawa iliyohifadhiwa kwenye ghala maalumu ambayo mtakaswaji huitumia kujikuna.
Anasema wakati huo, kibuyu cha kutunzia maziwa kinawekwa tumbaku hivyo mtakaswaji anakuwa ananusa harufu.
"Asubuhi anaamshwa kisha huchukua jani la mgomba lililowekwa sahani wakati wa kula chakula, kibuyu chake na kusimama mlangoni ...anafunikwa ngozi ya mbuzi iliyokaushwa kichwani, anaweka kibuyu chake kichwani na kukipiga na fimbo mara tatu," anasema.
Kwa mujibu wa Mtala, baada ya hapo anapelekwa mtoni asubuhi na mapema kabla ndege au watu hawajaamka na baada ya hapo, anaoga akiwa amefuatana na mganga wake.
Wakati huo wanakuwa na kitanda chao maalumu ambacho kilitengenezwa kwa ajili ya kumtakasa muhusika, kurudi nyumbani, kukoka moto, kunyolewa nywele utosini, kisogoni na kuanza kusalimia waliobaki nyumbani.Baada ya hapo ndugu wengine wanaondoka kurejea majumbani ambapo kazi inayobaki kwa mwanaume ni kwenda kumtafuta mwanamke wa kufanya naye tendo la ndoa ili atakaswe.
"Kama mtakwaswaji umri wake ni mkubwa kiasi kwamba hana nguvu za kuweza kufanya tendo la ndoa, basi huenda kwenye mti aina ya Omuzunguti na akifika anaanza kuita jina la marehemu mke wake akisema; "Iza tukobe, iza tukobe", neno lenye maana kuwa, "Njoo tuungane, njoo tuungane".Anasema baada ya hapo anatakiwa kujisaidia haja ndogo na kurudi nyumbani ambapo kesho yake asubuhi anapelekwa na ndugu zake kwenye kichuguu kisichokuwa na tundu lolote na kujisaidia haja ndogo bila kumaliza mkojo wote na unaobaki anatakiwa kuumwaga pembeni.
Akimaliza mila hiyo, anarudi nyumbani na kama mtakaswaji atakuwa mzee, hatakiwi kuoa tena, ananyolewa nywele zote na mtu aliyefiwa na mwenzi wake.Kama mtakaswaji anategemea kuoa tena, ananyolewa nywele utosini na kisogoni. Kama ni mzee atapewa mkuki wenye dawa ambao atakuwa akilala nao kitandani au nje. Mkuki ambao unatakiwa ni uliowahi kutumika kuua mtu, fimbo au silaha yoyote.
Asubuhi anapaswa kunawa na dawa, kuimwaga kwenye nguo na baada ya kumaliza mila hiyo, utakasaji unakuwa umekamilika.Makala hii imeandikwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari nchini (TMF).
Itaendelea kesho

No comments:

Post a Comment