22 August 2013

POLISI 7 'FEKI' MBARONI DAR

  • WALIVALIA SARE,MMOJA ANA CHEO CHA MEJA
  • YADAIWA WALIKUWA 'DORIA' MAENEO YA BOKO
  • OFISA USALAMA BANDIA NAYE ABAMBWA

 Baadhi ya nyaraka alizokamatwa nazo ofisa usalama feki.
 Kushoto ni Ofisa Usalama feki, Bw. Alquine Masubo,akiwa polisi.

 
Sare za polisi walizokutwa nazo watuhumiwa wa ujambazi wakiwa wamezivua.

Neema Rajab na Flora Nkya-TUDARCO

SIKU chache baada ya trafiki feki mwenye cheo cha sajini kukamatwa jijini Dar es Salaam akiongoza magari, mapya yamezidi kuibuka baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kufanikiwa kuwakamata watu saba wanaotuhumiwa kuwa majambazi wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo wakiwa na vyeo tofauti.

Mbali watu hao, Polisi pia amemkata mkazi mwingine wa jijini Dar es Salaam akijifanya Ofisa wa Usalama wa Taifa, huku akiwa na nyaraka mbalimbali za Serikali kutoka Ofisi za Uhamiaji na kitambulisho chake cha kazi, ambacho alikuwa akikitumia kabla ya kustaafu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Pia alikamatwa na bastola mbili zikiwa na risasi 12 na baada ya kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake alibainika kumiliki bastola nyingine ya tatu ikiwa na risasi 19.

Kukamatwa kwa watu hao kulithibitishwa na Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana.Alisema katika tukio la kwanza Polisi walifanikiwa kukamata watu saba wanaodaiwa kuwa majambazi wakiwa wamevalia sare hizo, huku mmoja akiwa na cheo cha Meja ambapo sare yake ilionesha beji inayosomeka SSGT A.M Mduvike.

Alisema watuhumiwa wengine wengine walikuwa na vyeo vya kawaida, lakini hakuvitaja. Aliongeza kuwa watuhumiwa hao walikuwa na redio ya mawasiliano, bastola aina ya Browm B. 3901 ambayo ilikutwa na risasi nne na ganda moja.Alisema askari hao feki walikamatwa wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Cresta namba T546BWR rangi nyeupe maeneo ya Kiluvya, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Aliongeza kuwa askari hao feki baada ya kuona wamezingirwa na Polisi waliamua kufyatua risasi moja hewani, hatua iliyowezesha Polisi kupambana nao na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kassim Mkalikwa (40), Magila Werema (31), Nurdin Bakari (46), Materu Marco (32), Luis Magoda (34) Amos Enock (23) na Amir Mohamed (47). Alisema wakati wa purukushani za kuwakamata w a t u h u m i w a h a o , w a w i l i walijeruhiwa miguuni ambapo walipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu na kwamba watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka eneo la tukio, vinaeleza kuwa, watu hao polisi feki walikuwa wakijifanya wapo doria,bila kujua kuwa polisi wanafuatilia nyendo zao.

Kwa upande wa Ofisa Usalama feki, Kamishna Kova, alimtaja kwa jina Alquine Michael Masubo (42) mkazi wa Yombo. Alisema mtuhumiwa huyo baada ya kuhojiwa alikiri kuwa yeye si mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Kwa mujibu wa Kamanda Kova, mtuhumiwa huyo alikamatwa na vielelezo mbalimbali, bastola tatu, kitabu cha mmiliki wa bastola namba CAR 00071678 chenye jina la P.1827 LT COL Mohamed H Ambali, kitambulisho cha jeshi na Lap Top aina ya Toshiba. Alisema mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi linamshikilia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ramadhan Semsota (63) kwa kosa la kujeruhi kwa risasi fundi ujenzi, Fadhili Mkachino. Tukio hilo lilitokea maeneo ya Salasala jijini Dar es Salaam.
 

1 comment:

  1. maisha ni magumu sana now days, watu wanatafuta kila namna kujitosheleza na mahitaji yao lol..

    ReplyDelete