MAPINDUZI makubwa ya kiuchumi
yaliyofanywa kimahiri na Jamhuri ya Watu wa China katika miaka ya 80 yamesaidia
kuziwezesha nchi nyingi zinazoendelea duniani kupiga hatua zaidi ya maendeleo,
kiuchumi na ustawi wa jamii.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika tafrija maalum
aliyomuandalia Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China hapa Zanzibar Balozi
Chem Qiman kwa ajili ya kumuaga rasmi akikaribia kumaliza muda wake wa utumishi
wa Kidiplomasia hapa Zanzibar.
Tafrija hiyo
mahsusi iliyoshirikisha pia baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Serikali na
baadhi ya watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanyika katika
Hoteli ya Serena Inn iliyopo Shangani Mjini Zanzibar na kuambatana na muziki
laini uliokuwa ukitumbuizwa na Kikundi maarufu cha kizazi kipya cha Akheri
Zamani.
Balozi Seif alisema mapinduzi hayo ya
kiuchumi ya China yametoa fursa kwa watendaji mbalimbali wa taasisi za umma na
hata zile binafsi sambamba na jumuiya za uzalishaji katika mataifa machanga kupata
taaluma tofauti nchini humo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imelazimika kumpa heshima kubwa Balozi Chen
kutokana na mchango wake mkubwa uliosaidia kuratibu uhusiano wa pande hizo
mbili hasa katika masuala ya taaluma,maendeleo na mwelekeo wa miradi ya
uwekezaji.
Akitoa
shukrani zake Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China Chen Qiman amewapongeza
Viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wake kwa
ushirikiano waliompa wakati akitekeleza majukumu aliyopangiwa na Taifa lake,
ambapo umemwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi na umahiri mkubwa wa hali ya
juu.
No comments:
Post a Comment